Wenje ataja kiini mtifuano Mbowe, Lissu Chadema

Mwanza. Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje amesema wapambe wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na wa makamu wake (Bara,) Tundu Lissu ndiyo chanzo cha mtifuano ndani ya chama hicho.

Wenje amesema hayo leo Ijumaa Januari 3, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari, viongozi na wanachama wa Chadema jijini Mwanza baada ya kurudisha fomu.

Amesema kinachoendelea kwa sasa ni chama hicho kujaribiwa lakini wanaoleta shida ni wapambe wa viongozi hao ambao kila upande unatukana upande mwingine.

“Lazima chama kiwe tested (kijaribiwe). Wanaoleta shida ni wapambe wa Mbowe na Lissu, hautasikia Mbowe amemtukana Lissu wala Lissu amemtukana Mbowe, ni wapambe,” amesema Wenje

Ameongeza “ukimtukana sana Lissu kesho utakutana naye, ukimtukana Mbowe kesho utakutana naye…ukimtukana Wenje leo, sisi sio milima tutakutana.”

Amewataka wanaomuunga mkono kuacha kutukana wengine kwa kuwa hawawezi kumsafisha kwa matusi, bali kwa hoja.

“Chama chetu ni kikubwa kuliko mtu yeyote. Hii dunia tunapita, tuweke akiba ya maneno. Kuna maisha baada ya uchaguzi,” amewaambia wanachama waliofika kwenye mkutano wake na waandishi wa habari

Katika hatua nyingine, Wenje amechukua fomu ya kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama hicho, kuijaza na kuirejesha leo katika ofisi za Kanda ya Victoria.

Amesema licha ya kuonekana kama kuna kutoelewana na Tundu Lissu anayegombea uenyekiti wa chama hicho, ila akichaguliwa na Lissu akachaguliwa, wataangalia namna bora ya kufanya kazi kwa pamoja.

“Mimi Tundu Antipas Lissu ni mtu ninayemuheshimu, amekuja kwetu kijijini, mimi kwao na Tundu Lissu ni sehemu ya familia yangu, tutayavuka salama, lazima niangalie namna gani tutatengeneza mahusiano na kufanya kazi kwa pamoja,” amesema Wenje.

Hata hivyo, Wenje amesema: “Nipo tayari kuwa msaidizi wa mwenyekiti yeyote atakayechaguliwa na watu wa Chadema katika shughuli yoyote.

“Naamini nina uvumilivu wa kutosha, hekima, subra ya kuwa makamu mwenyekiti wa chama chetu. Nilitia nia lakini leo natangaza rasmi kugombea nafasi hiyo. Kuanzia leo na kuwa mgombea rasmi wa nafasi ya makamu mwenyekiti,” amesema.

Wenje amesema miongoni mwa mambo atakayoyafanya atakashinda nafasi hiyo ni kusimamia maadili, akieleza siku za hivi karibuni baadhi ya wanachama na makada wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuwatukana wengine wakidhani ndio siasa kinyume na maadili yao.

Pia amesema atasimamia Chadema Digital kuhakikisha wanakusanya mapato ya kutosha yatakayotumika kuendeleza chama, kutoa mafunzo kwa viongozi na posho kwa makatibu wa chama hicho, akidai wanafanya kazi kubwa ya kukijenga lakini hawalipwi kitu.

Makamu Mwenyekiti Chadema Kanda ya Victoria, Khalid Swalehe amempongeza Wenje kwa kutombeza mtu yeyote wakati akizungumza na waandishi wa habari, akisistiza kipindi cha uchaguzi ndani ya chama chao ni cha kuongea na kutenda kwa busara.

Related Posts