BALOZI WA JAPAN ASIFU UTENDAJI KAZI WA TRA

 

Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa leo tarehe 03/01/2025 amekutana na kufanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda alipomtembelea ofisini kwake Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumuaga baada ya kumaliza muda wake.

Katika mazungumzo yao  yaliyojikita kwenye masuala ya Kodi, Uwekezaji, kubadilishana uzoefu na Biashara, Balozi Misawa ameipongeza TRA kwa kufanya makusanyo makubwa ya Kodi kistarabu jambo ambalo linachochea uwekezaji.

Balozi Misawa amesema wataendelea kudumisha uhusiano uliopo baina ya Tanzania na Japan kwa kushirikiana na TRA katika masuala ya biashara na uwekezaji.

Balozi huyo pia amegusia suala la kubadilishana uzoefu katika masuala ya Kodi baina ya TRA na Mamlaka ya Mapato nchini Japan ili kuongeza ufanisi zaidi.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema wanathamini uhusiano na ushirikiano uliopo baina ya TRA na Japan katika masuala mbalimbali ya kikodi na uwekezaji.

Bw. Mwenda amesema zipo sheria zinazoiongoza TRA katika kushughulikia masuala ya kidiplomasia na uwekezaji ambazo wamekuwa wakizitekeleza kikamilifu ili kuweka mazingira mazuri katika ufanyaji biashara kimataifa na uwekezaji.

“Tunaishukuru sana Serikali ya Japan kwa kuwa na mahusiano mazuri na Tanzania ambayo yamekuwa na manufaa chanya na tunaahidi kama TRA tutaendeleza mahusiano hayo yenye tija kidiplomasia” amesema Kamishna Mkuu Mwenda.

= = = = =

Related Posts