Benchikha aitema JS Kabylie | Mwanaspoti

MUDA mchache baada ya JS Kabylie kufuzu hatua ya 16 Bora ya Kombe la FA la Algeria, kocha wa timu hiyo aliyewahi kuinoa Simba, Abdelhak Benchikha ameachia ngazi, ikielezwa ni presha kubwa aliyokutana nayo tangu ajiunge nayo msimu huu licha ya timu kuongoza msimamo wa Ligi Kuu ya nchi hiyo.

Benchikha ameomba mwenyewe kuondoka klabuni hapo baada ya kuiongoza timu hiyo kwenye mechi 14 ameshinda saba, sare tatu na vipigo vinne inaongoza msimamo baada ya kukusanya pointi 24.

Akizungumza na Mwanaspoti, amesema ameamua kuachia ngazi kutokana na presha kubwa iliyopo ndani ya timu hiyo ambayo licha ya kuiacha kwenye nafasi ya kwanza hakuwa na amani.

“Ilikuwa ni kama naishi mtaani, sikuwa napata amani pale timu iliposhinda au kufungwa, nimechoka,” amesema Benchikha.

Alichofanya Benchikha akiwa na JS Kabylie sawa na alichofanya Simba ambapo aliomba kuachana na timu hiyo baada ya mchezo wa fainali wa Kombe la Muungano, ambao Simba iliifunga Azam kwa bao 1-0 ikitwaa taji.

Mbali na kubeba taji, Simba ilitwaa tuzo zote za michuano ikiwamo Mchezaji Bora iliyokwenda kwa Fabrice Ngoma, Kipa Bora iliyobebwa na Ayoub Lakred na Nyota wa Mchezo huo alikuwa ni Saido Ntivazonkiza.

Kocha huyo pia aliachana na USM Alger ya kwao Algeria baada ya kuipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika na Super Cup alitua Dar es Salaam usiku wa kuamkia Novemba 28 na kujiunga na Simba.

Timu hiyo ya Kabylie juzi jioni ilipata ushindi wa mabao 2-0 ikiwa ugenini dhidi ya Guelma katika mechi ya 32 Bora ya Kombe la Algeria na kutinga 16 Bora.

Related Posts