Tanga. Wanachama wa Umoja wa Wamiliki wa Waendesha Pikipiki na Bajaji Wilaya ya Tanga (Uwapibata) wamechanga Sh1 milioni kwa ajili ya Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua fomu ya kugombea urais kwa mwaka 2025.
Fedha hizo wamezikabidhi leo Januari 4, 2025, wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Tanga, Ummy Mwalimu, jijini hapa.
Akizungumza wakati akikabidhi fedha hizo, Mwenyekiti wa Uwapibata, Mohamed Chande amesema lengo la kumchangia Rais kuchukua fomu ni baada ya kuwawezesha kupata mikopo ya asilimia 10 na kushusha faini kutoka Sh30, 000 hadi Sh10,000.
“Sisi bodaboda na bajaji kwa umoja wetu tumeamua kuchanga fedha hizi lengo ni kumtia moyo Rais Samia sababu kwa mapenzi yake ameamua kututhamini na ametubadilisha jina kutoka bodaboda na kuwa maafisa usafirishaji,” amesema Chande.
Madereva hao pia wamemwomba Mbunge wao, Mwalimu, kuwatunishia mfuko wao wa kukopeshana ili wapate leseni.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwalimu amesema alishakutana na viongozi wa Uwapibata nyumbani kwake mara mbili hivi ambapo walijadili changamoto zao.
Katika utatuzi wa changamoto hizo, amesema amewashirikisha wadau ili kupata fedha za kujenga vituo vya bodaboda ambavyo vitakuwa kitega uchumi na atahakikisha anaweka intaneti.
“Ndoto yangu nataka kuacha alama ya kujenga vituo vya bodaboda katika mitaa yote 181 iliyopo jijini Tanga na nihakikisha naviweka katika mfumo wa satelite ili wateja hata wakiwataka wanapiga simu tu,” amesema.
Kuhusu changamoto wa mfuko wao, Mwalimu ametoa Sh10 milioni kwa ajili ya bodaboda zaidi ya 1,000 kupata leseni za udereva ili waache kukimbizana na askari polisi, huku pia akiwawekea lita mbili mbili za mafuta katika bodaboda na bajaji 500 za jijini Tanga.