WADAU Wa Sekta ya Urembo na Mitindo wameihimiza serikali kuweka Mazingira bora ya uwakala wa bidhaa za kimataifa za vipodozi ili kupunguza changamoto ya bidhaa bandia zinazosambazwa nchini.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa tawi jipya la Duka la Dawa baridi na Vipodozi Mkurugenzi wa CAICA Pharmacy, Jackson John, amesema Kampuni yake inalenga kuwa mfano wa kuigwa katika sekta ya vipodozi kwa kuhakikisha bidhaa bandia zinadhibitiwa.
“Mbali na huduma za maduka ya dawa, sisi pia ni mawakala wa bidhaa za vipodozi za kimataifa tunataka kuhakikisha bidhaa bandia zinatokomezwa kwa kuweka uwakilishi bora wa bidhaa halisi nchini,” alisema.
John ameongeza kuwa makampuni makubwa ya kimataifa yanategemea uwepo wa mawakala wa kuaminika ili kuingiza bidhaa zao katika masoko mapya, na ukosefu wa mawakala nchini ni moja ya sababu zinazokwamisha ujio wa bidhaa hizo.
“Haya makampuni yanahitaji mawakala wa uhakika tunataka Tanzania iwe na mawakala wengi zaidi ili kuvutia bidhaa hizi kubwa kuja nchini.”
Hata hivyo ameongeza kuwa Kampuni hiyo imeweka ubunifu wa kuhakikisha wanendana sanjari na utandawazi kwa kuweka Mfumowezeshi (app) ya kuhakikisha Mteja anafanya Manunuzi mtandaoni bila kufika dukani hapo.
Nae Mshindi wa pili wa Miss Tanzania 2023/24, Amina Jigge, amesema kuwa wajasiriamali wana nafasi kubwa ya kuboresha sekta ya vipodozi ikiwa serikali itapunguza vikwazo vinavyowakabili.
“Wajasiriamali wetu wana uwezo wa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya urembo, lakini wanakabiliwa na changamoto nyingi. Serikali ikirahisisha taratibu za uwakala wa bidhaa, tutaweza kupunguza uingizwaji wa bidhaa bandia na kuwasaidia wateja kupata bidhaa bora na salama.”
Kwa upande wake Miss Grand Tanzania 2024, Fatma Suleiman, amesema bidhaa bandia zimekuwa chanzo cha madhara kwa watumiaji, akisisitiza umuhimu wa mawakala wa kuaminika kama CAICA Pharmacy.
“Kuna bidhaa nyingi bandia ambazo zimekuwa zikileta madhara kwa watumiaji. Tunashukuru CAICA kwa kuhakikisha wanaleta bidhaa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji. Serikali inapaswa kuwasaidia wafanyabiashara kama hawa ili kuhakikisha bidhaa halisi zinapatikana nchini.”
Mkurugenzi wa CAICA Pharmacy akizungumza na Wanahabari,Wadau Wa Urembo Katika Hafla ya Ufunguzi wa Tawi jipya lililopo Mikocheni Jijini Dar es Salaam
Miss Grand 2024 Fatma Suleiman akizungumza na Wanahabari machache huku akisisitiza Warembo kutumia bidhaa zilizo na ubora na Viwango ili kuepukana na uharibu wa Afya ya Ngozi zao