Unguja. Wakati nyumba mpya za kisasa za makazi zikijengwa, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi imeelekezwa kuandaa mpango maalumu wa sheria au kanuni kuzilinda zisiharibiwe.
Maelekezo hayo yametolewa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi leo Januari 4, 2025 alipofungua nyumba za makazi na biashara eneo la Kwa Mchina Mombasa, ambazo zimejengwa na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) kwa gharama ya Sh9.5 bilioni na kuuzwa kwa wananchi.
Dk Mwinyi amesema Zanzibar inajitahidi kujenga nyumba lakini hakuna utunzaji, kwa hiyo lazima wizara iwe na sheria, akiwataka wanunuzi wa nyumba hizo pia kuwa na kamati maalumu ili kuzitunza zidumu kwa kipindi kirefu.
“Tunajua sisi ni mabigwa wa kujenga lakini hatuna utaratibu wa kutunza, kwa hiyo wizara anzisha kamati maalumu za matunzo na mje na utarataibu wa kikanuni au sheria kuhakikisha nyumba hizi zinatunzwa. Tukiziacha hivihivi utakuta zinaharibiwa na kuchakaa kwa muda mfupi,” amesema.
Amesema Serikali imeamua kujenga nyumba za makazi na kuziuza kwa wananchi bila faida, lengo ni kuondoa nyumba ambazo hazina viwango.
“Tumeona kuna mahitaji makubwa, nyumba hapa zinajengwa lakini hazina viwango. Nyumba inajengwa kwa muda mrefu kisha inachakaa hata kabla haijaisha, tumeamua kuja na utarataibu huu wa kujenga nyumba tena mtu ananunua kwa mfumo wa kukopeshwa bila hata Serikali kupata faida,” amesema.
Hata hivyo, amesema pamoja na kutaka kujenga nyumba za kisasa na kuondoa chakavu, wamekuwa wakikutana na vikwazo, hususani katika nyumba za makazi za Kilimani na Michenzani.
Hata hivyo, amesema watahakikisha wanaondoa zote zilizochakaa.
“Tunakutana na vikwazo, nyumba zimejengwa zimeshachakaa, hata ukisema uzifanyie ukarabati zingine haziwezekani utapiga rangi ila mifumo yake ya maji na umeme ishakuwa mibovu, sasa tunataka kujenga nyumba za kisasa lakini unaona vikwazo, hata hivyo tutajenga tu,” amesema.
Dk Mwinyi amesema mpango wa Serikali ni kuhakikisha wananchi wanakaa kwenye makazi bora.
Amesema wameshajenga nyumba 300 Chumbuni, hivyo mpango huo utaendelea katika maeneo mbalimbali kwa kuwa wamebaini mahitaji ni makubwa.
Awali, akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Khadija Khamis Rajab amesema mradi huo wenye nyumba katika vitalu vinne ukiwa na vyumba 82, umetumia Sh9.5 bilioni.
“Nyumba zimewekewa utaratibu wa malipo na zote zimeshauzwa, 29 tayari wameshamaliza malipo na wengine 43 wanaendelea na malipo katika utaratibu maalumu,” amesema.