Jaji Mkuu aongoza maziko ya Werema, azungumzia mchango wake

Butiama. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ameongoza mamia ya watu katika mazishi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Frederick Werema katika mazishi yaliyofanyika katika Kijiji cha Kongoto kilichopo Wilaya ya Butiama mkoani Mara.

Jaji Werema (69) alifariki dunia Desemba 30, 2024 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla.

Akizungumza katika mazishi hayo yaliyofanyika Butiama mkoani Mara leo Jumamosi Januari 4,2025, Profesa Juma amesema maisha ya Jaji Werema yana mchango mkubwa kwa Taifa.

Amesema sio rahisi kueleza kwa muda mfupi mchango wa Jaji Werema katika ustawi wa taifa hasa katika sekta ya sheria kwani katika kpindi chake cha utumishi ameweza kufanya mambo mengi ambayo yamekuwa na matokeo chanya kwa ustawi wa taifa na watu wake.

Amesema nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni nyeti ambayo pia ina majukumu mengi yanayopaswa kufanyika kwa wakati mmoja na kwamba nafasi hiyo inahitaji mtu mwenye uwezo mkubwa majukumu ambayo  marehemu wakati wa utumishi wake aliyamudu na kuyatenda kwa ufanisi mkubwa.

“Hii kazi naweza kuifananisha na samaki aina ya pweza, wababa wengi kule Dar es Salaam wanamfahamu vizuri samaki huyu, ana mikono mingi na mikono ile inaweza kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja, ndivyo ilivyokuwa kwa  Jaji Werema aliweza kufanya kazi hii kwa mikono mingi kwa wakati mmoja na mafanikio yanaonekana,” amesema Profesa Juma.

Amesema enzi za uhai wake, Jaji Werema alitekeleza majukumu yake kwa ujasiri mkubwa huku akizingatia misingi ya sheria na haki na kwamba pale alipotakiwa kutoa ushauri aliweza kufanya hivyo bila woga wala upendeleo.

“Mtakumbuka alipotoa taarifa bungeni juu ya operesheni tokomeza ujangili, sote tunajua baada ya ile taarifa yake nini kilifuata, Jaji Werema alikosoa kazi zilizofanywa chini ya kiwango lakini pia hakusita kusifu kazi zilizofanywa kwa viwango na kuzingatia misingi ya sheria na utawala bora,” amesema.

Profesa Juma amesema marehemu alisistiza juu ya mapambano dhidi ya uhalifu na jinai huku akitoa angalizo kuwa mapambano hayo hayapaswi kuwa sehemu ya uvunjaji wa sheria na taratibu.

Amesema marehemu aliamini kuwa kazi ya uwakili ni huduma bora na ya heshima, hivyo inapaswa kufanyika kwa umakini na weledi na kwamba ili mtu aweze kuwa wakili msomi ni lazima afanye kazi zenye viwango.

“Alikuwa akisema hakuna sababu ya kujiita wakili msomi wakati kazi zako sio za viwango na yeye binafsi alikuwa akijiamini sana na ndio maana kuna watu walikuwa wanasema anaringa lakini kiuhalisia alisimama na kufuata misingi ya sheria,” amesema.

Akizungumza katika hafla hiyo ya mazishi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na sekta ya sheria nchini imepata pigo kubwa kufuatia kifo hicho.

Johari amesema wakati wa uhai na utumishi wake, marehemu Jaji Werema alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha sheria na haki vinatumika katika kuleta maendeleo endelevu nchini.

Amesema umahiri, weledi na kujituma kwa marehemu Jaji Werema enzi za uhai na utumishi wake kulipelekea kupatikana kwa mafanikio mengi katika majukumu mbalimbali aliyopewa wakati wa utumishi wake.

“Jaji Werema alikuwa mtu mwenye maono, mtaalamu na mbobezi mfano mzuri ni pale alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Katiba na Haki za Binadamu mwaka 1998 katika Wizara ya Katiba na Sheria na miongoni mwa mambo aliyoyafanya katika nafasi hiyo ni kuanzisha mchakato wa uanzishwaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora pamoja na mifumo ya uchaguzi na sheria za uchaguzi ilianzishwa kipindi hicho chini ya usimamizi wake,” amesema.

Johari amesema weledi na umahiri wa Jaji Werema katika utendaji wake umesababisha uwepo wa maboresho makubwa katika suala zima la utawala bora.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema Jaji Werema alikuwa kiongozi jasiri na mwadilifu na kwamba katika maisha yake hakupenda kuzungumzia watu bila uwepo wao.

“Huwezi kuwa kiongozi halafu unafanya kazi ya kuteta watu, hili kwa Werema halikuwepo, alikuwa muwazi, kama kuna jambo umelifanya anakuita anakwambia, hakuwa na makandokando nadhani sisi viongozi tunapaswa kujifunza kwake,” amesema Mtaka.

Akihubiri katika misa ya mazishi, Naibu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Padri Julius Ogolla amesema wanadamu wanapaswa kumwamini Mungu na kumtanguliza katika kila jambo huku akiwataka wanafamilia kuendelea kubaki na matumaini Mungu.

Amesema kifo ni daraja la kurudi kwa Mungu, hivyo kila mtu anapaswa kuishi maisha ya kumpendeza Mungu ili siku ya mwisho kila mtu aweze kufufuliwa katika wafu.

“Tumtazame marehemu Jaji Werema kwa mema aliyoyafanya yatusaidie katika majukumu yetu na huku tukijiandaa kwa zamu zetu, kama kuna mabaya aliyoyafanya hayo tumuachie Mungu,” amesema.

Akisoma wasifu wa marehemu, mtoto wa marehemu, Edwin Werema amesema watamkumbuka baba yao kwa hekima, busara na utanashati wakati wote wa maisha yake, vitu amedai ni miongoni mwa urithi ambao amewaachia na wao wanajivunia kwayo.

Amesema baba yake alizaliwa katika Kijiji cha Kongoto wilayani Butiama mwaka 1955 ambapo alipata elimu ya msingi katika shule ya Nyegina wilayani Musoma kabla ya kuendelea na masomo kwa ngazi tofauti.

Edwin amesema mbali na kuwa wakili wa serikali, jaji wa Mahakama Kuu, pia, baba yake aliwahi kuwa mwalimu wa shule ya sekondari Shaban Robert na kwamba marehemu ameacha mjane, watoto watatu na wajukuu watatu.

“Baba yetu alianza kujisikia vibaya Desemba 29, 2024 ambapo alikimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, madaktari pale walijitahidi kuokoa maisha yake lakini mwisho wa siku alikutwa na mauti,” amesema.

Jaji Werema aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 2009 na aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, nafasi aliyoitumikia hadi mwaka 2014 alipojiuzulu.

Related Posts