Mechi 10 zaishtua Simba Tunisia

Simba imetazama historia ya mechi zake 10 zilizopita za kimataifa ilizocheza ugenini na kugundua ina kazi kubwa ya kufanya katika mechi ya kesho jijini Tunis, Tunisia itakapocheza na CS Sfaxien ya huko.

Katika mechi hizo 10 zilizopita za kimataifa ambazo Simba imecheza ugenini, haijapata ushindi huku ikitoka sare tano na kupoteza michezo mitano.

Na mechi dhidi ya timu za Kaskazini mwa Afrika zimeonekana kuwa mtihani mkubwa kwa Simba kwani katika mechi saba zilizopita, imepata sare mbili na kupoteza tano ikifunga mabao mawili na kufungwa mabao 11.

Kiungo wa Simba, Mzamiru Yassin amesema kuwa wanafahamu ugumu wa kucheza ugenini hivyo wanapaswa kufanya kazi ya ziada katika mechi ya kesho.

“Mechi za ugenini huwa zinakuwa ngumu haijalishi tunacheza na timu gani. Tunatakiwa kupambana kuhakikisha tunapata pointi tatu ili mechi zinazokuja ziwe rahisi. hatuitaji kusubiri mechi ya mwisho.

“Tunajitahidi kurekebishana kila siku kwamba tunatakiwa tuwe makini na kuhusu mechi kima mtu anapopata dakika za kucheza azitumikie ipasavyo. Tunapambana mechi hii tupate pointi tatu ili mechi inayokuja mbele iwe rahisi zaidi,” amesema Mzamiru.

Wakati Simba ikiwa na historia isiyovutia ugenini, wenyeji CS Sfaxien imekuwa na matokeo ya wastani katika mechi za mashindano ya klabu Afrika inayocheza nyumbani.

Katika mechi 10 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika ambazo Sfaxien ilikuwa mwenyeji, timu hiyo imepata ushindi mara tano, kutoka sare mbiili na kupoteza michezo mitatu.

Ushindi kwa Simba dhidi ya Sfaxien kesho, utaiweka katika nafasi nzuri ya kusogea hadi nafasi ya pili au ya kwanza katika msimamo wa kundi A la Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa sasa, Simba inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi sita sawa na Onze Bravos na CS Constantine ambazo kila moja ina pointi sita huku Sfaxien ikishika mkia ikiwa haina pointi.

Related Posts