KIUNGO aliyekuwa anatajwa kujiunga na Yanga na ghafla dili lake kukwama, Kelvin Nashon ametoa sababu za kukwama kuwa ni kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha Singida Black Stars, huku akidai kuwa muda mwingine ikitokea nafasi atacheza.
Yanga ilituma ofa ya kumtaka Nashon kwa mkopo dilisha hili la usajili na mambo yalikwenda vizuri, lakini ghafla hakukamilisha dili na baadaye aliibuka beki Israel Mwenda wa klabu hiyo kujiunga na watetezi hao wa Ligi Kuu kwa mkopo, japo hajaanza kutumika.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nashon alisema sababu kubwa ya dili kukwama Yanga ni kutokana na kutocheza mara kwa mara, na Yanga ilikuwa inahitaji mchezaji ambaye ataingia moja kwa moja kikosini kuonyesha ushindani.
“Ni kweli dili la kujiunga na Yanga limekufa, sitaweza kucheza tena sababu kubwa ni viongozi kuogopa kunipa presha ya kuwapa kile walichokuwa wanatarajia na ukizingatia kipindi wananihitaji timu ilikuwa kwenye presha ya kukosa matokeo, hivyo walihitaji mchezaji ambaye atawapa matokeo ya ubora moja kwa moja,” alisemamchezaji huyo.
“Baada ya kufika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumalizana na Yanga ili niweze kusaini mkataba ndipo nilipokutana na viongozi kuniambia kuwa wananiamini, lakini sijacheza muda wanahofia kuniongeza kikosini nitashindwa kuwapa kitu kizuri kwa uharaka, hawataki mtu wa majaribio.”
Nashon alisema viongozi wanaamini katika uwezo wake, lakini hawataki kumuingizia presha ambayo itamtoa mchezoni, kitu ambacho kama mchezaji alikubali na kukipokea licha ya kujiamini kuwa ni mshindani, hivyo ameona bora ajitafute.
Akizungumzia sababu ya kukosa nafasi, alisema hakuwa majerahi ni mzima lakini changamoto ni ongezeko la wachezaji na benchi la ufundi jipya ndivyo vitu vilivyomtoa mchezoni huku akikiri pia kuwa maingizo mapya yalikuwa na nyota wengi wazoefu na nafasi yake anayocheza imejaa mastaa wengi wa kigeni.