Sababu ZRA kuvuka lengo makusanyo Julai-Desemba

Unguja. Wakati Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) katika kipindi cha nusu ya kwanza cha Julai hadi Desemba 2024 ikikusanya Sh429.033 bilioni sawa na ufanisi wa asilimia 102 ya makisio, sababu 10 zimetajwa kuchangia hali hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamishna wa ZRA, Said Ali Mohamed kwa vyombo vya habari leo Januari 4, 2025 imesema miongoni mwa sababu hizo ni uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa miundombinu na huduma za kijamii na kuimarika shughuli za kiuchumi Zanzibar.

Katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/25, ZRA ilikadiriwa kukusanya Sh225.171 bilioni na imekusanya Sh228.098 bilioni, ambao ni ufanisi wa asilimia 101.30.

“Kwa kulinganisha na makusanyo ya robo ya pili ya mwaka uliopita wa 2023/24, ambayo yalikuwa Sh189.937 bilioni, yanaonyesha ongezeko la makusanyo ya Sh38.161 bilioni sawa na ukuaji wa makusanyo ya asilimia 20.09,” amesema.

Taarifa hiyo imesema kwa Desemba 2024 pekee, ZRA imekusanya Sh75.582 ambao ni ufanisi wa asilimia 100.11 ya kiasi kilichokadiriwa cha Sh63.513 bilioni. Hilo ni ongezeko la makusanyo ya Sh12.069 bilioni sawa na ukuaji wa makusanyo wa asilimia 19.

Kaimu Kamishna Said amesema kuimarika kwa uhusiano na ushirikiano kati ya ZRA na wafanyabiashara pamoja na wadau wengine wa ndani na nje ya Zanzibar ni sababu mojawapo ya kuongeza kwa ulipaji kodi wa hiari.

Pia, kuimarika kwa miundombinu ya bandari, hususan Bandari ya Mkoani, Pemba na kuongezeka uwajibikaji wa walipakodi katika matumizi ya mifumo ya ukusanyaji wa mapato wa Zidras katika kulipa kodi na mfumo wa kutolea risiti za kielektroniki (VFMS).

Katika mipango ya kuendelea kufanya vizuri kwa kipindi kijacho, ZRA imesema itakuwa karibu na wafanyabiashara kuwasaidia katika kurahisisha mazingira ya biashara kisheria, kutoa msaada wa karibu na kuwajengea mazingira ya kustawisha biashara zao, hususani walipakodi wapya.

“Kuweka kambi maalumu za walipakodi katika maeneo mbalimbali zenye lengo la kutoa huduma za kodi kwa karibu na kuongeza wigo wa kusajili wafanyabiashara,” amesema.

Baadhi ya wafanyabiashara wamesema mfumo au utaratibu ulioanzishwa na mamlaka hiyo kuwatembelea na kusikiliza changamoto zao umetoa hamasa ya kulipa kodi bila kusukumwa.

“Angalau kwa sasa unaona ukaribu wa mamlaka na wafanyabiashara, lakini zamani ilikuwa ukisikia maofisa wanakuja biashara zinafungwa, hata kauli zilizokuwa zinatumika hazikuwa rafiki. Sasa tumeanza kuchukuliana kama watu wenye nia moja,” amesema Abdukadir Shah, mfanyabaishara eneo la Mlandege.

Related Posts