Stendi ya mabasi Kijichi kubadilishwa matumizi

Dar es Salaam. Stendi ya Kijichi iliyojengwa kwa ajili ya mabasi yaendayo mikoa ya Kusini sasa inatarajiwa kubadilishwa matumizi, baada ya malengo ya ujenzi kutotekelezeka.

Mradi huo uliogharimu Sh3.9 bilioni kupitia Miradi ya Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP) ukijumuisha soko, maduka makubwa na stendi, umekimbiwa na wafanyabiashara. Mradi huo ulianza kazi Oktoba 17, 2022.

Hata hivyo, stendi hiyo ilishindwa kutumika baada ya kutokea malalamiko ya wadau, ukiwamo Umoja wa Madereva wa Mabasi Kanda ya Kusini, waliosema barabara za kuingia stendi ni ndogo hali inayofanya magari kusubiriana kupishana.

Baadhi ya abiria walisema eneo hilo ni mbali kufikika, wakishauri wabaki  stendi ya Mbagala Rangi Tatu.

Kwa muda mrefu mabasi yanayoenda mikoa ya Kusini yamekuwa yakitumia stendi ya muda iliyoko Mbagala Rangi Tatu na hata baada ya kusitisha matumizi ya stendi ya Kijichi, yalirejea kwenye stendi hiyo iliyokuwa ya muda.

Alipoulizwa na Mwananchi Desemba 24, 2024 kuhusu kukwama kutumika stendi ya Kijichi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Jomary Satura alisema badala ya kuwa stendi ya mabasi ya mikoani, itakuwa stendi ndogo kwa ruti za magari ya ndani na wameamua kuweka vitu ambavyo vitashawishi watu kwenda huko, ikiwamo michezo ya watoto na maduka makubwa.

“Mwanzoni stendi ya Kijichi ilidhaniwa ingekuwa ni kituo kikubwa, lakini kwa sasa itabaduilishwa matumizi.

“Ili kushawishi watu kwenda kule ni lazima uweke vitu vya kuvutia na moja ya mambo tunayoyafikiria kuyafanya ni kuweka michezo ya watoto. Mpaka sasa tunaendelea kukusanya mawazo kufanya uwekezaji ambao hautasababisha gharama, bali uwe na faida,” amesema.

Satura amesema tayari wataalamu wa Manispaa ya Temeke wameanza kuleta baadhi ya michoro.

“Nia yangu tufanye uwekezaji mkubwa utakaoleta tija kwa watu wetu na wakati huohuo kuiingizia halmashauri mapato,” amesema.

Stendi yarudi Temeke Sudan

Akizungumzia upatikanaji wa stendi mbadala ya mabasi yaendayo mikoa ya Kusini, Satura amesema wameamua kuirejesha ilipokuwepo zamani, Temeke Sudan, kwa kuwa tayari kuna ofisi nyingi za kampuni za magari eneo hilo.

“Japokuwa tunaamini bado haitatosha, tunaendelea kutafuta eneo kwa ajili ya kujenga stendi kubwa zaidi,” amesema.

Urejeshwaji wa stendi hiyo yalikuwa miongoni mwa maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoyatoa alipofanya ziara Temeke Oktoba 6, 2024.

Katika ziara hiyo, Majaliwa alikagua miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kwa fedha za Serikali.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara baada ziara, Majaliwa aliagiza mchakato wa ujenzi wa stendi hiyo uendelee ulipoishia ili wananchi wawe na eneo zuri la kupata huduma za usafiri baada ya stendi ya Kijichi kushindwa kufanya kazi.

“Eneo hili mlipewa mkachelewa kuliendeleza mkanyang’anywa, lakini mwaka 2021 niliwakutanisha na TBA (Wakala wa Majengo) ili muweze kujenga stendi, lakini naambiwa tangu mfanye vikao vitatu mwaka huo hamjakutana tena, sasa nataka kuona stendi ikijengwa pale kwani hii inayotumika kwa sasa haina hadhi ya stendi ya manispaa,” alisema Majaliwa.

Akizungumzia utekelezaji wa agizo hilo, Satura amesema bado wapo kwenye majadiliano na TBA.

“Baada ya hapo kitakachokubaliwa kitapelekwa kwenye Baraza la Madiwani na kisha Bodi ya TBA kwa ajili ya kuupitisha mradi, halafu ndipo utekelezaji uanze,” amesema.

Kuhusu stendi ya daladala wilayani humo, amesema wanatarajia kupanga bajeti ya mwaka ujao.

Amesema kwa sasa wanaendelea kupata maoni kutoka kwa wadau.

Taboa, Darcoboa wapaza sauti

Ubadilishaji wa matumizi ya stendi ya Kijichi umeelezwa ni matokeo ya kutoshirikisha wadau.

Akizungumza na Mwananchi, Desemba 30, 2024 Msemaji wa Wamiliki wa Mabasi yaendayo Mikoani (Taboa), Mustapha Mwalongo, amesema hawakushirikishwa katika ujenzi wa stendi ya Kijichi, bali waliiona ilipokamilika na kuelekezwa kupelekwa mabasi huko.

Amesema kwa muda mrefu wamekuwa hawashirikishwi kwenye masuala ya yanayowahusu, yakiwamo ya ujenzi na uhamishaji wa stendi.

“Nakumbuka kabla ya kuhamishwa stendi ya Ubungo na kupelekwa Mbezi, tulishauri isihamishwe badala yake iongezwe kwa nyuma kwa sababu kulikuwa na eneo kubwa, lengo ikiwa kuwarahisishia wananchi kupata huduma katikati ya mji, lakini tulipuuzwa.

“Ni kutokana na hilo unaona hivi sasa ofisi nyingi za mabasi zipo Shekilango jambo linaloifanya Serikali kuingia gharama ya kufanya ukaguzi stendi ya Magufuli na stendi ya Shekilango. Kama mawazo yetu yangezingatiwa yasingetokea haya leo,” amesema.

Amesema walishawahi kupendekeza kuwe na stendi maeneo tofauti pembezoni mwa mji, yaani ya magari ya Nyanda za Juu Kusini ingekuwa Mbezi, mikoa ya Kaskazini Bunju na mikoa ya Kusini iliyopo Mbagala iboreshwe na kumlipa mmiliki fidia aiachie Serikali, lakini nayo yalipuuzwa.

Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwaya Lema, amesema watendaji huwashirikisha wadau baada ya kujenga miradi, badala ya tangu kufanya hivyo awali ili watoe mawazo yao ya nini wangependa kifanye.

“Tulishaanza kupeleka magari kule lakini mwisho wa siku tulikuwa tukipata hasara, kwani mtu anaenda na abiria anarudi mtupu,” anasema.

Licha ya kusudio la kubadilishwa matumizi stendi ya Kijichi, anasema bado haoni kama yanaweza kuleta tija kwa kuwa mwisho wa siku daladala zitakwenda kubeba watoto, ambao hawatakuwepo kila siku.

Ameshauri ni vema kukawekwa soko la jumla akisema: “Wakiweka soko la jumla huku, mtu anayetoka Kigamboni, Mbagala Chamazi na maeneo mengine ya jirani hataona haja ya kuingia gharama ya kwenda Temeke Stereo au Tandika kwa kuwa anajua akifika Kijichi atapata kila kitu na baada ya hapo atapata usafiri wa daladala wa kumpeleka anapokwenda,” amesema.

Mkazi wa Chang’ombe, Agnes Ruta amesema hatua ya kuacha stendi ya Mbagala iendelee ni jambo zuri, akitaka pia uharakishaji wa uendelezaji stendi ya Sudan.

Enock Shitundu, mkazi wa Tandika ameishauri Serikali kupunguza michakato mirefu katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuwaharakishia huduma wananchi.

“Hii stendi tumeisikia hapa Temeke Sudan kuna mpango wa kujengwa siyo leo wala jana, hatuelewi kwa nini utekelezaji umechukua muda. Tunahitaji mambo yaende haraka ili kuwasogezea wananchi huduma,” amesema.

Akizungumzia hali hiyo, mtaalamu Profesa wa uchumi Abel Kinyondo amesema mabadiliko hayo yanatokana na tatizo la kukosekana utawala bora katika kuanzisha miradi.

“Tatizo la watendaji wetu wengi wanadhani wao wanaelewa sana kuliko watu wengine na kujifanyia mambo vile wanavyoona, kwa kuona wataweza kuwaambia watu wafuate maagizo yao.

“Mfano mzuri wa miradi ya aina hii iliyoazishwa na kushindwa kufanya kazi vizuri ni ule wa Machinga Complex. Watu walikataa kupanda ghorofa za juu, pia mikoani huko masoko mengi yaliyojengwa yameshindwa kufanya kazi,” amesema.

Profesa Kinyondo ameshauri ni vema kukawepo ushirikishaji wa watu wakati wa kuanzisha miradi badala ya watendaji kujiamulia.

Related Posts