VIJANA WATAKIWA KUENDLEZA UMOJA NA MSHIKAMANO KUJENGA NCHI

Mjumbe wa Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla amewataka vijana
kuendeleza umoja na mshikamano pamoja na kuwa na dhamira njema ya kuijenga nchi
ili kila mmoja  aweze kunufaika na
matunda ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Akizungumza na Vijana
wa Umoja wa Vijana wa CCM Zanzibar ( UVCCM ) kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti wa
CCM Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati wa Uzinduzi wa Matembezi ya Miaka 61 ya
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Katika Uwanja wa Mpira wa Tumaini Mkwajuni, Mkoa
wa Kaskazini Unguja.

Amesema katika kujenga
Nchi yenye maendeleo ni lazima kuwepo na misingi Imara itakayolisaidia Taifa kufikia
malengo yake, ni lazima jamii iweze kuepukana na vitendo viovu vya dhulma,
chuki, rushwa na ufisadi kwa mustakbali mwema wa vizazi  vya sasa na  baadae.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu
ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema
vijana watakaposhikamana vizuri na kusaidiana katika kutafuta na kutengeneza
ajira wanaweza kutatua kwa kiwango kikubwa changamoto mbali mbali za kimaendelo
zinazoikumba jamii katika kufikia Mapinduzi ya kiuchumi na kimaendelo.

Sambamba na hayo amefahamisha
kuwa Serikali imedhamiria kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa makundi yote
ya vijana kwa lengo la kuhakikisha inawapatia fursa za ajira kwa namna iliyo
bora na sahihi kwa mujibu wa taratibu za nchi ikiwa ndio fikra na falsafa za
muasisi wa Mapinduzi matukufu ya Mwaka 1964.

Mhe Hemed amesema
kutokana na mchango mkubwa unaotolewa na vijana katika kujenga jamii yenye
maendeleo amewahakikishia kuwapatia mashirikiano na kuwapa kipao mbele katika
kukikuza Chama Cha Mapinduzi na Taifa kwa ujumla.

Nae Mwenyekiti wa Umoja
wa Vijana wa CCM Taifa Comred MOHAMED ALI
KAWAIDA
amesema watahakikisha watayatumia matembezi hayo kwa kuwahamasisha
Vijana na wananchi wote kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la
kudumu la mpiga kura ili Chama cha Mapinduzi kiweze kushinda kwa kishindo  katika uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025
ili  CCM iendelea kushika Dola.

Mwenyekiti Kawaida
amesema kuwa Vijana watahakikisha wanalinda na kudumisha Umoja, Amani na
Mshikamano ambao ndio fikra na falsafa ya muasisi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar
ambayo ndio chachu ya maendeleo nchini .

Kwa upwnde wake Naibu
Katibu Mkuu wa UVCCM anaefanyia kazi zake Zanzibar Ndugu ABDI MAHMOUD ABDI amesema Matembezi hayo yatakayojumuisha vijana zaidi
ya Elfu  nne(4000) yana lengo la
kuadhimisha Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar amabayo yameifanya zanzibar
kuwa nchi yenye na Amani na Utulivu.

ABDI
amesema kupitia Matembezi hayo vijana watatoa elimu kwa wananchi wa Zanzibar
juu ya umuhimu wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambayo yamemkomboa Mzanzibari
kutoka katika madhila ya Wakoloni pamoja na kusambaza kauli zenye kuhamasisha
Amani na Upendo kwa maendeleo endelevu ya Zanzibar.

Amefahamisha kuwa Vina
wa UVCCM wameandaa matembezi hayo kuudhihirishia Umma wa Kitanzania na Dunia
kwa ujumla kuwa vijana wapo tayari kuyalinda, kuyaenzi na kuyatetea Mapinduzi
kwa nguvu na gharama yoyote ile na hawatokuwa tayari kuchokozeka kwa kauli za
wapinzani zisizo na mustakbali mwema wa Taifa.

Matembezi hayo
yaliyozinduliwa leo yatapita katika Mikoa 
na Wilaya zote za Unguja na Pemba ambayo yanatarajiwa kufikia kikomo
Januari 10, 2025 katika Mkoa wa Kaskazini Pemba na kufungwa rasmi na Mwenyekiti
wa CCM Taifa ambae pia ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania Dkt. Samia
Suluhu Hassan.

Mjumbe
wa  Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman
Abdulla akimkabidhi Bendera  Kiongozi wa Matembezi ya Umoja wa Vijana wa
CCM Zanzibar ( UVCCM )Komred Juma Usonge kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti
wa CCM Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi nikiashiria Uzinduzi wa
Matembezi ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Katika Uwanja wa
Mpira wa Tumaini Mkwajuni, Mkoa wa Kaskazini Unguja na kupitia katika
Wilaya na Mikoa yote ya Unguja na Pemba na kufikia tamati tarehe 10
Januari 2025 katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.

 

Related Posts

en English sw Swahili