WIKIENDI ya kibabe. Unaweza kusema ni Super Weekend kutokana na leo na kesho kuanzia hapa nyumbani hadi kule Ulaya kuna mechi za kibabe.
Kwa leo, Jumamosi, kuanzia saa 9:30 alasiri hadi saa 5:00 usiku ni mwendo wa burudani tu kwa mtindo wa bandika bandua kutokana na mechi zilizopo kisha kesho Jumapili itamaliizwa kwa utamu mwingine.
Kwa wale wanaopenda kucheki soka katika vibanda umiza ni muhimu kuaga kabisa nyumbani, ili usije ukatafuta kesi.
Ndio! Kule England kuna mechi saba za kibabe kuanzia saa 9:30 alasiri pale Tottenham Hotspur itaikaribisha Newcastle United kwenye Uwanja wa Tottenham jijini London ikiwa ni nusu saa tu kabla ya mashabiki wa soka hapa nchini kuishuhudia Yanga ikivaana na TP Mazembe ya DR Congo pale Kwa Mkapa.
Mara baada ya mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, saa 12:00 jioni uhondo utahamia tena England kwa mechi tano tofauti ikiwamo ile ya Man City dhidi ya West Ham, Crystal Palace dhidi ya Chelsea, Aston Villa itakayovaana na Leicester City na kadhalika.
Lakini kama unadhani kazi itakuwa imeishia hapo umekosea, saa 1:00 usiku katika Ligi ya Mabingwa Afrika kuna mechi nyingine ya kibabe kati ya Orlando Pirates dhidi ya Stade d’ Abidjan itakayoenda sambamba na mechi za Ligue 1 ya Ufaransa na Serie A ya Italia na saa 2:30 usiku itakuwa ni zamu ya kurudi tena England.
Arsenal itakuwa ugenini dhidi ya Brighton na ikiisha mechi hiyo kuna michezo miwili ya michuano ya CAF. FAR Rabat na Raja Casablanca zote za Morocco zitakuwa nyumbani kuzikaribisha AS Maniema ya DR Congo na Mamelodi Sundowns kabla ya Ligue 1 na Serie kufunga pazia kwa mechi za mwisho za saa 5:00 usiku.
Kisha uhondo utahamia kesho, Jumapili, kwa mechi za maana sana katika Kombe la Shirikisho Afrika ikiwamo ile ya CS Sfaxien itakayokwaruzana na Simba jijini Tunis, wakati England kutakuwa na kipute kikali cha vinara wa EPL, Liverpool itakayoikaribisha Manchester United. Sasa kwa utamu huo kwa nini isiwe Super Wikiendi?
Huu ni mchezo ambao umekaa kimtego zaidi kwa timu zote, kwani kila moja inahitaji matokeo mazuri kufufua matumaini ya kuitafuta robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na ukweli kwamba hazichekani katika Kundi A zikitenganishwa kwa tofauti ya pointi moja.
Yanga yenye pointi moja mkiani inaikaribisha TP Mazembe iliyopo juu yake kidogo ikimiliki pointi mbili, huku kila moja ikipiga hesabu ya kutaka kumgeuza mwenzake kama ngazi ya kujisogeza eneo la juu katika kundi hilo linaloongozwa na Al Hilal yenye pointi tisa na kufuatiwa na MC Alger yenye alama nne.
Mchezo huu utapigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni. Kumbuka kesho, Jumapili vinara wa kundi hilo, Al Hilal yenye pointi tisa itakuwa nyumbani kuikaribisha MC Alger waliokusanya pointi nne wakishika nafasi ya pili.
Baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza dhidi ya Al Hilal na MC Alger, wababe hao wa Tanzania, Yanga walizinduka ugenini mbele ya TP Mazembe kwa kupata pointi moja katika sare ya 1-1 hali ambayo imewapa morali ya kufanya vizuri, leo, Jumamosi.
Rekodi zinaonyesha kwamba leo itakuwa ni mara ya sita kwa Yanga na TP Mazembe kukutana katika michuano ya CAF, huku matokeo ya mechi tano zilizopita zikionyesha hakuna mbabe kutokana na mechi mbili za kwanza. Mwaka 2016, TP Mazembe ilishinda zote kwa matokeo ya 1-0 (ugenini) na 3-1 (nyumbani).
Yanga ikajibu mapigo msimu wa 2022-2023 kwa ushindi unaofanana na huo, nyumbani ilishinda 3-1 na ugenini ikashinda 1-0. Mechi zote hizo nne ni za Kombe la Shirikisho Afrika, lakini msimu huu katika Ligi ya Mabingwa – ile ya kwanza nyumbani kwa TP Mazembe imemalizika kwa sare ya bao 1-1.
Wakati ule ambao Yanga ilionekana bado inaendelea kujitafuta chini ya Kocha Sead Ramovic, hivi sasa inatajwa kwamba imekaa sawa huku ikitamba na msemo wao wa Gusa Achia Twende Kwao, iliyowatesa vilivyo Mashujaa waliochapwa 3-2, Tanzania Prisons (4-0), Dodoma Jiji (4-0) na Fountain Gate (5-0) kwenye ligi.
Mbali na hivyo, katika mchezo uliopita dhidi ya TP Mazembe, Yanga iliutawala kwa asilimia 56.6 dhidi ya 43.4 za wenyeji wao.
Pia, Yanga ilipiga mashuti mengi (18) na matano yakilenga lango la wapinzani ambao wenyewe mashuti yalikuwa 12 huku mawili pekee yalilenga lango. Takwimu hizo zilionyesha kitu ambacho Yanga ilikuwa ikikitafuta.
Merceil Ngimbi Vundi, Zemanga Soze na mfungaji wa bao Cheick Fofana walionekana kuwa hatari zaidi wakiongoza mashambulizi ya TP Mazembe. Hao ni wachezaji wa kuangaliwa zaidi katika mchezo wa leo kwani muda wowote wanaweza kufanya balaa.
Ukuta wa Yanga ukiongozwa na nahodha, Dickson Job na Ibrahim Bacca unaonekana kuimarika huku urejeo wa Chadrack Boka aliyekosekana mechi iliyopita dhidi ya TP Mazembe unaongeza kitu, ikielezwa kwamba kuna uwezekano kipa namba moja Djigui Diarra anaweza kudaka kwani tangu alipoumia na kutolewa dakika ya 45 dhidi ya TP Mazembe ugenini hakucheza mechi yoyote.
Hesabu za Yanga hapa ni kushinda ili kufikisha pointi nne ambazo zitawapandisha juu ya TP Mazembe kisha kubakiwa na mechi mbili, ugenini dhidi ya Al Hilal wenye nafasi kubwa ya kufuzu kisha kumalizia nyumbani dhidi ya MC Alger.
Tangu Yanga itoke kucheza na Al Hilal, imeshacheza mechi nne za ligi ikifunga jumla ya mabao 16 huku yenyewe ikiruhusu mawili jambo ambalo limeonekana kuwatisha TP Mazembe ambao mechi tatu za nyumbani haijashinda yoyote.
Kocha msaidizi wa Mazembe, Pamphil Mihayo ameliambia Mwanaspoti kuwa wanatambua wanakuja kukutana na Yanga iliyoimarika baada ya kucheza mechi nne za Ligi ya nyumbani na kushinda zote kwa idadi kubwa ya mabao huku ikicheza kwa kasi kubwa tofauti na waliyokutana nao kwenye Uwanja wa Mazembe.
“Tuna taarifa zao za kutosha, kuna watu wetu wapo hapo, ukweli ni kwamba tutakuja kucheza mechi ngumu, unaona jinsi timu yao ilivyoimarika, wanafanya vizuri kuliko ilivyokuwa kabla ya kukutana nao kwetu.
“Timu yao inafunga mabao mengi na kwa sasa ukiangalia mechi tatu za makundi ilifunga bao moja tu dhidi yetu lakini tunajua mechi tatu zilizopita imefunga mabao zaidi ya 10, bila kuruhusu wavu wao kuguswa. Tunatakiwa kuwazuia vizuri wasiendelee na utulivu huu kwa kuipanga safu yetu ya ulinzi,” alisema kocha huyo huku akibainisha kuwa Mazembe haijacheza mechi yoyote ya ushindani tangu wakutane na Yanga wakati wapinzani wao hao wakicheza mechi nne.
“Ni kweli hatujacheza mechi yoyote tangu tulipokutana na Yanga, kuna mechi za kirafiki tu mbili tulizitumia kuwaimarisha vijana ila wenzetu wamecheza mechi za Ligi, nadhani wachezaji wetu watakuwa wamepata mapumziko ya kutosha,” alisema.
Kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua, alisema mchezo dhidi ya TP Mazembe wataucheza kwa sura mbili, kufa au kupona kwani ndiyo umeshikilia hatma yao.
Pacome aliongeza kwamba, wanafahamu kwamba wamebakiwa na mechi tatu ambazo kwao ni fainali wakianza na TP Mazembe, kisha Al Hilal na mwisho dhidi ya MC Alger hivyo wamejiandaa na hilo.
“Kwa namna soka tunalocheza huku morali yetu ikiwa juu lazima tukafanye maamuzi mazito mbele ya Mazembe.
“Haitakuwa mechi rahisi lakini kikosi chetu sasa kina sura ya kupigania ushindi kwa kuwa kuna mwanga unaonekana,” alisema Pacome.
Kwa upande wa mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize, amesema: “Hatujaanza vizuri lakini bado tuna nafasi ya kufanya vizuri, timu chini ya kocha Sead Ramovic ilikuwa inajitafuta, tayari wachezaji tumeanza kuzoea mfumo wake tutaendelea tulipoishia kwenye ligi ili tuendane na kasi ya Ligi ya Mabingwa.
“Tutaingia kwa kumuheshimu mpinzani wetu bila kujali ubora tulionao sasa kwenye ligi kwani ni michuano miwili tofauti, natamani kuwa mmoja wa wachezaji watakaokuwa bora kwenye mchezo huo ikiwa ni pamoja na kufunga.”
Mchezo wa Yanga dhidi ya TP Mazembe utachezeshwa na waamuzi watatu kutoka Mauritius wakiongozwa na Ahmad Imtehaz Heeralall atakayekuwa mwamuzi wa kati akisaidiwa na Ram Babajee na Aswet Teeluck huku mwamuzi wa nne akiwa Noris Aaron Arissol kutoka Seychelles.
Kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi uliopo Radès jijini Tunis, Tunisia, Simba itaipeperusha bendera ya Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika ikisaka pointi za kuisogeza katika robo fainali ya michuano hiyo kwa mara nyingine.
Kibu Denis ndiye aliyefanya maajabu katika mchezo wa hapa nyumbani akifunga mabao mawili baada ya wageni kutangulia mapema dakika ya tatu kupitia Hazem Haj Hassen. Kibu alisawazisha dakika ya 7 na kuweka la ushindi dakika ya 90+8 yote kwa kichwa.
Mchezo wa leo utapigwa bila ya mashabiki kufuatia Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kuishushia rungu CS Sfaxien kwa kuitoza faini na kuzuia mashabiki wake kuingia uwanjani katika mechi mbili za Kombe la Shirikisho Afrika.
Adhabu hiyo imekuja kutokana na vurugu za mashabiki wa timu hiyo katika mchezo wa kwanza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa nyumbani dhidi ya CS Constantine ya Algeria uliopigwa Novemba 27, huku Sfaxien ikilala nyumbani kwa bao 1-0. Kucheza mechi bila ya mashabiki inaweza kuwa nafuu kwa Simba katika kuifukuzia rekodi yao ya kucheza robo fainali kwa mara ya sita katika kipindi cha misimu saba kuanzia 2018/19.
Rekodi zinaonyesha Simba katika mara tano ilizocheza makundi huko nyuma kabla ya msimu huu, haijawahi kushindwa kufuzu robo fainali. Msimu huu itakuwaje?
Simba inakutana na Sfaxien, timu ambayo haijashinda mechi yoyote katika kundi hilo baada ya kupoteza michezo mitatu ikishika mkia bila pointi yoyote. Kundi hilo linaongozwa na CS Constantine yenye pointi sita sawa na Simba na Bravo ya Angola.
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, anasema: “Naijua Sfaxien na aina ya soka inalocheza ikiwa nyumbani, tulipata alama tatu kwetu ni vivyo hivyo ili kukamilisha hesabu nzuri kwenye kundi hili. Wachezaji wote wako timamu na tayari nimeshawaambia kuwa jambo la muhimu ni alama tatu tu, ili kuipa heshima timu na kuwa nafasi nzuri.”
Naye kipa namba moja wa Simba, Moussa Camara, anasema: “Hapa Tunisia tunataka heshima kwa kutafuta ushindi wa kwanza ugenini, kwani timu yetu imeimarika sana na kila mmoja anaridhishwa na namna maandalizi ya mchezo huo.”
Jeshi la Fadlu limeongezeka baada ya Elie Mpanzu usajili wake katika michuano ya Caf kukamilika kwani alikosekana mechi zote zilizopita lakini sasa anaruhusiwa kucheza.
Simba imefikia katika Hotel Royal ASBU Tunis ambayo ni hoteli ya kifahari iliyoko katikati mwa eneo la biashara liitwalo Center Urbain Nord Tunis.
Hoteli hiyo ina vyumba 142, inapatikana umbali wa takribani kilomita kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Tunis Carthage. Pia ni kilomita 10 kutoka Medina eneo la kihistoria la Tunis na msikiti wa Zeitouna, huku ikiwa ni kilomita tano kutoka Jiji la Utamaduni. Kwa usiku mmoja, gharama ya juu zaidi kwa chumba ni Sh2,381,669 huku ile ya chini ni Sh364,211. Pia kuna cha Sh728,423 na Sh409,582. Kila chumba wanaweza kulala watu wawili.
Mbali na vyumba vya kulala, ukumbi wa mikutano na sehemu za kuogelea na gyma, pia kuna eneo la huduma ya SPA ambayo ni kwa ajili ya kumfanya mtu kuimarisha afya yake kwa kufanya mazoezi na ulaji wa vyakula maalum ambapo humo wanaoruhusiwa kuingia ni wenye umri kuanzia miaka 15 kuendelea juu.
Michezo ya wiki ya nne ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, inakwenda kushuhudiwa huku baadhi ya timu zikiwa bado hazijaonja ladha ya kipigo kabisa.
Katika Kombe la Shirikisho, timu tatu pekee kati ya 16 ndiyo hazijapoteza mechi zao hadi sasa ambazo ni vinara wa kundi B, RS Berkane yenye pointi tisa baada ya kushinda michezo yote mitatu.
Kuna vinara wa kundi C, USM Alger wenye pointi saba, nayo imeshinda mechi mbili na sare moja. Wapo vinara wa kundi D, Zamalek wenye pointi saba nao ni kama USM Alger wameshinda mbili na sare moja.
Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa, ni timu saba kati ya 16 hazijapoteza mechi zao ambazo ni vinara wa kundi A, Al Hilal walioshinda mechi zote tatu, vinara wa kundi B, Mamelodi Sundowns na wanaowafuatia AS FAR Rabat kila mmoja akishinda mechi mbili na sare moja, huku Maniema ambaye naye yupo kundi hilo akitoka sare zote tatu, hajashinda wala kupoteza.
Al Ahly na Orlando Pirates kutoka kundi C nao hawajapoteza kama ilivyo kwa Esperance waliopo kundi D.