YANGA ikiwa inapambana uwanjani leo jioni ikiizamisha TP Mazembe kwea mabao 3-1, jukwaani akaonekana mshambuliaji mpya, Jonathan Ikangalombo, ambaye Mwanaspoti liliwaripotia kwamba yupo hatua ya mwisho kumalizana na klabu hiyo ya Jangwani.
Ikangalombo anyemudu kucheza winga zote mbili anayetokea AS Vita alionekana jukwaa Kuu la VVIP akiwa na maofisa wa Yanga wakithibitisha wazi kwamba yupo hatua za mwisho kujiunga na Mabingwa hao wa Soka Tanzania Bara.
Nyota huyo alikuwa kivutio katika jukwaa hilo ambapo vigogo mbalimbali walionekana kumsalimia akiwa amevalia kaptula na shati huku kichwani akiwa amevaa kofia.
Yanga inataka kuboresha safu ya ya kiungo kwa kumuongezea mshambuliaji huyo mwenye kasi na nguvu katika dirisha dogo la usajili.
Taarifa kutoka kwa mabosi wa Juu wa Yanga ni kwamba winga huyo atasaini mkataba wa miaka miwili wakati wowote kuanzia leo.
Bosi mmoja wa Yanga ambaye aligoma winga huyo asipigwe picha alisema waliamua kumshusha haraka nchini kufuatia kuanza kupata taarifa kwamba zipo klabu zilianza kumfuata winga huyo.
“Tumeona tumlete hapa nchini haraka ndio maana tunaomba msimpige picha tunataka tumalizane naye haraka mara baada ya mchezo huu (dhidi ya Mazembe) au kesho mapema,” alisema bosi huyo.
“Unajua zipo klabu ambazo baada ya taarifa ya usajili wake kujulikana zilianza kumsumbua kwa kutaka kumtumia tiketi ili wamsajili Sasa tukaona tumlete haraka nchini.”