Yao atangaza vita mapema | Mwanaspoti

WAKATI mashabiki wakianza kujiuliza mtaani na mtandaoni itakuwaje mara beki wa kulia ya Yanga, Yao Kouassi atakaporejea kutoka kwenye majeruhi kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na Kibwana Shomary aliyewashika kwa sasa, lakini beki huyo kutoka Ivory Coast amevunja ukimya na kusema anaukubali uwezo wa mwenzake, huku akisititiza anaamini akipona atarejea katika eneo hilo kama kawaida.

Yao yupo nje ya uwanja akiuguza jeraha la nyama za paja na nafasi yake imezibwa vyema na Kibwana ambaye awali hakuwa akipewa nafasi enzi za kocha Miguel Gamondi aliyekuwa akimtumia Dickson Job au Denis Nkane, jambo lililoibua maswali kwa mashabiki kwamba akipona hali itakuwaje katika eneo hilo la kulia.

Hata hivyo, Yao amevunja ukimya kwa kuzungumza na Mwanaspoti, akisema anafurahi namna Kibwana alivyokomaa wakati yeye akiendelea kujiuguza, akiifanya Yanga iendelea kuwa imara zaidi eneo la ulinzi na anamkubali mwenzake huyo ila anaamini muda si mrefu atarajea katika eneo hilo.

Beki huyo alisema anaendelea kujiuguza, lakini anaamini atakapokuwa sawa na kurejea uwanjani, bado atakuwa na nafasi ya kuendelea pale alipoishia kabla ya kuumia.

Yao alisema anaukubali uwezo wa Kibwana, kwani ni beki mzuri na anayejituma kitu ambacho kimeifanya Yanga isiwe na pengo lolote kutokana na kukosekana kwake.

“Niseme wazi, Kibwana ni beki mzuri na wala sina tatizo naye, lakini nikipona majeraha nitarudi kwenye nafasi yangu. Naujua uwezo wangu ila namuachia kocha ndiye atakayeamua nani acheze wapi, kwa kuwa jambo la msingi ni wachezaji wote kuisaidia timu kufanikiwa,” alisema Yao na kuongeza:

“Sio jambo jepesi kwa mchezaji yeyote kuwa nje, hivyo natamani kupona na kurejea kuipambania timu yangu katika michuano yote tunayoshiriki.”

Beki huyo alionekana mara ya mwisho katika mechi za ligi wakati Yanga ikishinda mabao 3-2 dhidi ya Mashujaa, kisha kukosa michezo mitatu mfululizo dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji ilizozifunga mabao 4-0 kila moja na ile ya ushindi wa 5-0 mbele ya Fountain Gate na kuifanya ivune mabao 13-0.

Related Posts