MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Aisha Masaka anayekipiga Brighton & Hove Albion ameondoka nchini baada ya likizo ya wiki moja na anatarajia kurejea uwanjani mwishoni mwa Februari kuuwahi mchezo wa Ligi dhidi ya Chelsea utakaopigwa Machi 02.
Masaka alipata jeraha la bega kwenye mchezo wa Ligi Kuu England (W) dhidi ya Arsenal Novemba 9 mwaka huu uliomuweka nje kwa takribani miezi mitatu.
Akizungumza kuhusu jeraha hilo, Masaka alisema kwa sasa anaendelea vizuri na ripoti ya daktari inaonyesha maendeleo mazuri.
“Nimefanya operesheni nina kama wiki ya nne sasa inaenda
mwishoni mwa mwezi Februari nitarejea uwanjani, naamini utakuwa msimu mzuri na wenye ushindani kwangu,” alisema Masaka.
Hadi sasa Masaka amecheza dakika 10 tangu ajiunge na Brighton, dakika tatu dhidi ya Arsenal ambapo hakumaliza baada ya kuumia.
Dhidi ya Birmingham alitumika kwa dakika saba.
Brighton inapochapisha picha ya Masaka kwenye mtandao wa kijamii Watanzania wanajaa kwenye ukurasa huo kila mmoja akitoa maoni yake na hapa mshambuliaji huyo anajibu.
“Huo ni upendo wa Watanzania kwa wachezaji wao wanaocheza Ligi kubwa, muda mwingine inakuwa sio nzuri na huwezi kulimit upendo wa mashabiki lakini kwangu nina furaha sana.”