Barabara za njia nne kujengwa Moshi – Arusha kupunguza foleni

Moshi. Uboreshaji na ujenzi wa barabara za njia nne kwenye baadhi ya maeneo ya miji ya Moshi na Arusha unanukia baada ya Serikali kueleza usanifu na mchakato wa kuwapata makandarasi watakaotekeleza jukumu hilo, unakwenda vizuri.

Mchakato huo utakwenda sambamba na ujenzi daraja jipya la Mto Kikafu ili kuwaondolea adha ya ajali za mara kwa mara watumiaji wa Barabara ya Arusha – Holili.

Daraja la Mto Kikafu changamoto yake kubwa ikitokea ajali, njia hiyo haipitiki, hali inayosababisha foleni kubwa ya magari kwa watumiaji wa barabara hiyo inayounganisha mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na nchi jirani ya Kenya.

Akizungumza leo Jumapili Januari 5 2025, mbele ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega aliyekwenda kukagua eneo litakalojenga daraja hilo, Meneja wa Uboreshaji wa Barabara ya Arusha-Holili, Manger Rajab amesema mradi huo utagharimu Sh 488.667 bilioni ambazo ni mkopo nafuu kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Japan (Jica).

Rajab amesema fedha hizo zitahusisha usanifu wa kina, usimamizi, ununuzi, ujenzi na uboreshaji wa Barabara ya Arusha- Holili kwa baadhi ya maeneo ya mikoa yenye jumla ya kilomita 22.67.

Rajab amesema kwa upande wa Moshi zitajengwa njia za barabara nne zenye kilomita 11.3 itakayoanzia maeneo ya Kiborloni hadi Maili Sita, wakati Arusha itaanzia Tengeru hadi USA River kilomita 11.35.

“Sehemu ya pili itakuwa ujenzi wa daraja jipya la Mto Kikafu litakalokuwa la kisasa ambalo litakuwa na barabara unganishi za kilomita 4.7. Lakini kutakuwa na maboresho ya daraja hili la zamani ili kuimarisha usalama wake,” amesema Rajab.

Amesema taratibu za kuwapata makandarasi zinaendelea, hivi sasa wameshafanya maandalizi ya awamu ya kwanza ya barabara za Moshi na Arusha.

“Timu za kupitia makabrasha ya makandarasi imeshafanyika, sasa hivi kuna hatua ya kupitisha kwenye bodi ili kuwapata makandarasi hawa. Usanifu wa kina kwa barabara za Moshi na Arusha umekamilika,” amesema Rajab.

Pia, amesema makandarasi wa mradi wataanza kuwa eneo la mradi Mei 2025 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa ujenzi huo.

Hata hivyo, Ulega amesema Mei ni mbali akiwataka kuangalia namna ya makandarasi hao kuwa eneo la mradi ifikapo Machi kwa ajili ya kuanza kazi hiyo.

“Nisikilizeni hakuna sababu ya kusubiri hadi Mei kwa yale ambayo yana uwezo wa kufupishwa. Yale yaliyo ndani ya uwezo wenu fanyeni usiku na mchana, ikiwezekana ujenzi uanze Machi, hakuna sababu ya kuweka mlolongo mrefu,” amesema Ulega.

Amesema ameelezwa ajali mbalimbali zinatokea katika Daraja la Kikafu akisema kwa niaba ya Serikali, wanatoa pole kwa ndugu waliopoteza wapendwa wao ikiwamo iliyohusisha watu 14 kufariki dunia.

“Rais Samia Suluhu Hassan ametupa maelekezo zile ajali zinazoweza kuzuilika, lazima tufanye kila njia kuboresha miundombinu yetu ili kuepuka changamoto hizi zinazosababisha vifo na majeruhi.

“Hapa Kikafu tuna mradi wa ujenzi wa daraja hili, sambamba uboreshaji wa Barabara ya Arusha-Holili ili kuondoa msongamano wa maeneo yote ya mijini, tutaweka barabara mbili zinatoka, mbili zinaingia hapa Moshi,” amesema Ulega.

Waziri Ulega amesema Arusha zitajengwa eneo la Tengeru hadi USA River, barabara hizo zitakuwa za viwango ikiwamo kuweka njia ya waenda kwa miguu ili kuondoa mwingiliano na magari.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema katika eneo Kikafu wamepoteza watu wengi waliofariki dunia kwa ajali za magari, hata hivyo wanapata faraja kwa ujio wa waziri huyo wa ujenzi.

Babu amesema uboreshaji wa Barabara Arusha – Holili ni muhimu kwa sababu wingi wa watu wakiwamo watalii wanaomimika kutoka mataifa mbalimbali.

Mkazi wa Kwa Sadala ambako kuna Daraja la Mto Kikafu, Hussein Mwanga hatua ya kujenga upya kwa daraja hilo utasaidia kupunguza foleni za magari na ajali zinazotokea mara kwa mara katika eneo hilo.

“Hapa ni balaa kwa ajali kutokana mteremko mkali na ufinyu wa daraja hili ambalo gari likapata ajali mnaweza mkaa hata saa tano hadi lije kutolewa.Nimefurahi ujenzi wa njia nne utapunguza foleni pia eneo la Kiborloni kuingia Moshi Mjini,” amesema Mwanga.

Changamoto ya usafiri na usafirishaji hasa wa mazao ya tangawizi na mpunga yanayotoka tarafa za Mamba Myamba na Gonja wilayani Same, inakwenda kuwa historia.

Hii ni baada ya Serikali kuanza ujenzi wa kipande cha barabara kwa kiwango cha lami kutoka Ndungu hadi Mkomazi yenye kilomita 36.

Wakati mkandarasi akikabidhiwa jukumu la ujenzi wa barabara hiyo, pia Serikali imetangaza kuwa mchakato wa kumpata mkandarasi atakayejenga takribani kilomita 50 kutoka Same hadi Ndungu umeshakamilika.

Ujenzi wa njia ya Ndungu hadi Mkomazi ni sehemu ya barabara ya kilomita 100 inayoanzia Same -Kisiwani hadi Mkomazi ikiunganisha mikoa ya Tanga na Kilimanjaro.

Mchakato huo utakwenda sambamba na kuifungua hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.

Tarafa za Mamba Myamba na Gonja zinasifika kwa kulima tangawizi kwa asilimia 70 inayosafirishwa kwenye mikoa mbalimbali pamoja na mpunga. Huku, wakulima na wananchi wakilalamikia ubovu wa barabara wakati wa kusafirisha mazao hayo hasa nyakati za mvua.

Juzi Waziri Ulega aliwapa matumaini akiwaambia kero au changamoto zinazowakabili zinakwenda kupata ufumbuzi baada ya kumkabidhi mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi na Mawasiliano ya China (CCCC) itakayotekeleza mradi huo kwa miezi 18.

Kabla ya kumkabidhi mkandarasi huyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mohamed Besta amesema zabuni ya sehemu ya tatu kutoka Same hadi Mahole yenye kilomita 56.8 kwa kiwango cha lami, mkandarasi ameshapatikana na wakati wowote mkataba utasainiwa ili kumaliza kilomita 100 za barabara hiyo.

Besta amesema barabara hiyo ni mojawapo ya mtandao muhimu katika mikoa ya Kilimanjaro hasa tarafa za Gonja, Ndungu, Bendera ambazo ni maarufu kwa uzalishaji wa tangawizi na mpunga hivyo ni kiungo cha usafirishaji wa mazao hayo.

Akimkabidhi mradi huo, Ulega amesema wakazi wa maeneo hayo ni wachapakazi wa  kulima tangawizi na mpunga ndiyo maana Serikali imeamua kuijenga barabara hiyo ili kuzalisha kwa wingi na kufikisha kwenye masoko kwa uharaka.

Waziri Ulega alisema lengo la ujenzi wa barabara hiyo ni kuondoa kero kwa kuboresha mtandao wa njia hiyo  sambamba ujenzi wa madaraja ili kuongeza ufanisi kwenye sekta ya usafirishaji na usafiri.

“Matumaini yangu, ujenzi wa barabara hii utaondoa kero ya usafiri na usafirishaji, ikakamilika pia itashusha gharama za usafiri kwa wananchi,” amesema Ulega.

Pia, amesema barabara hiyo ikakamilika itakuza utalii katika hifadhi ya Mkomazi sambamba na kusafirisha kwa uhakika mazao hayo.

Related Posts