Championship ngoma inogile | Mwanaspoti

WAKATI ukibaki mchezo mmoja kuhitimisha mzunguko wa kwanza wa Ligi ya Championship kwa msimu huu wa 2024-25, tayari yapo matukio mengi yaliyojitokeza, kuanzia ushindani kwa timu zenyewe, wachezaji na vioja mbalimbali vilivyojitokeza.

Ligi hii ambayo kwa sasa imeendelea kuonyesha ushindani na kuvutia wachezaji wakubwa kuicheza tofauti na ilivyokuwa hapo mwanzoni, Mwanaspoti imefanya tathimini kutokana na kilichotokea katika michezo yote iliyopigwa hadi mzunguko huu wa 14.

Timu ya Biashara United imeandamwa na majanga tangu msimu huu umeanza baada ya kupokonywa pointi 15 na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), kufuatia kushindwa kufika Mbeya, katika mchezo wake wa Ligi ya Championship dhidi ya Mbeya City Desemba 3, 2024.

Biashara inayokabiliwa na ukata, ilitakiwa kucheza na Mbeya City Desemba 1, 2024, ingawa iliiandikia Bodi ya Ligi (TPLB) barua ya kuomba mchezo huo namba 87, uchezwe Desemba 3, japo siku hiyo pia haikutokea uwanjani bila ya sababu za msingi.

Kitendo hicho kikaifanya Bodi kuipoka pointi 15 na kuipa Mbeya City ushindi wa mabao matatu na pointi tatu, huku pia kwa upande wa Biashara ikapigwa faini ya Sh3 milioni kwa mujibu wa kanuni ya 31:1 ya Championship kuhusu kutofika uwanjani.

Ukata huo umefanya baadhi ya mastaa wakiwamo, Ditram Nchimbi, Sadala Lipangile, Fredson Elisha, Faustine Kulwa na Elias Maguri kuondoka na kuiacha mkiani na pointi moja tu baada ya kucheza michezo 14, ikishinda minne, sare minne na kuchapwa sita.

Wakati timu mbili zitakazomaliza nafasi ya kwanza na ya pili zikipanda Ligi Kuu Bara moja kwa moja huku zitakazomaliza ya tatu na nne zikicheza ‘Play-Off’, ushindani umekuwa mkubwa kwao kutokana na kutopishana kwa pointi nyingi hadi sasa.

Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja msimu uliopita, inaongoza ikiwa na pointi 35, ikifuatiwa na Mbeya City inayotafuta tena tiketi ya kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu wa 2022-23, inayoshika nafasi ya pili kwa kukusanya pointi 31.

Geita Gold iliyoshuka daraja msimu uliopita na Mtibwa Sugar, iko nafasi ya tatu na pointi 30, ikifuatiwa na ‘Chama la Wana’ Stand United yenye pointi zake 29, inayojitafuta tena kurejea Ligi Kuu Bara, baada ya kushuka msimu wa 2018-2019.

Msimu huu umekuwa mgumu kwani hadi sasa imefungwa ‘hat-trick’ moja tu iliyofungwa na mshambuliaji wa Mbeya City, Faraji Kilaza Mazoea, katika mchezo wa timu hiyo dhidi ya maafande wa Polisi Tanzania, walioshinda mabao 4-0, Desemba 13, 2024.

Hii ni tofauti na msimu uliopita wa 2023-24, ambapo hadi kufikia raundi ya 14, zilikuwa zimefungwa ‘hat-trick’ tatu, huku akiongoza aliyekuwa nyota wa Biashara United anayeichezea Tusker FC ya Kenya, Mganda Boban Zirintusa aliyefunga mbili.

Kocha wa Makipa wa Geita Gold, Augustino Malindi amefungiwa michezo 16 na kutozwa faini ya Sh1 milioni na Bodi ya Ligi (TPLB), kwa kosa la kumshika sehemu za siri mwamuzi wa akiba, baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu dhidi ya Mbeya City.

Katika mchezo huo uliopigwa Desemba 22, 2024, kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya ambao wenyeji walishinda bao 1-0, Malindi alienda tena vyumbani na kumshika kifuani mratibu wa mchezo huo ambaye ni mwanamke jambo ambalo ni kinyume cha maadili.

Pia kocha huyo amefungiwa michezo mingine mitatu na kutozwa faini ya Sh500,000 kwa kosa la kumtukana mwamuzi msaidizi namba moja, huku adhabu hiyo ikitolewa kwa kuzingatia kanuni ya 45:2(2.11) ya Ligi ya Championship kuhusu udhibiti kwa makocha.

Tukio la aina hiyo lilitokea pia msimu uliopita ambapo nyota wa Cosmopolitan, Gilbert Boniface alifungiwa michezo 10 na Bodi ya Ligi (TPLB), kutokana na kile kilichoelezwa kumshika sehemu za siri mwamuzi, katika mchezo wao dhidi ya KenGold.

Katika mchezo huo ambao KenGold inayoshiriki Ligi Kuu Bara kwa sasa ilishinda mabao 2-0, Oktoba 21, 2023, nyota huyo alitozwa pia faini ya Sh500,000, huku akikiri mwenyewe kupitia gazeti hili ilimuharibia taswira yake kwa jamii nzima.

Makocha wanane kati ya timu 16, wameondoka na kutafuta changamoto sehemu nyingine wakiwamo, Melis Medo aliyekuwa Mtibwa Sugar ambaye amejiunga na Kagera Sugar, Mussa Rashid wa Biashara United na Twaha Beimbaya aliyekuwepo Kiluvya United.

Meja Mstaafu, Abdul Mingange aliondoka Stand United, japo kwa sasa amejiunga na Songea United ya Ruvuma.

Wengine ni Ivo Mapunda aliyekuwa Songea United ambaye alisema ameondoka ili kujiendeleza na masomo, Ally Ally (Transit Camp), Mohamed Kijuso (Cosmopolitan) na Amani Josiah aliyekuwa Geita Gold ambaye kwa sasa amejiunga na Prisons.

Ni michezo miwili tu iliyoshuhudiwa vipigo vizito hadi sasa huku ikiwa ni timu moja tu ya Geita Gold iliyoifunga mabao 5-1, Green Warriors Novemba 30, 2024, na ushindi pia wa 5-0, dhidi ya Biashara United, mechi iliyopigwa Desemba 27, 2024.

Katika raundi hizi 14, ni mchezo mmoja tu uliozalisha mabao mengi ambao ulikuwa namba 38, baina ya Mbeya City dhidi ya TMA ya Arusha, ulioisha kwa miamba hiyo kufungana mabao 4-4, mechi iliyopigwa Uwanja wa Sokoine Mbeya Oktoba 20, 2024.

Sehemu nyingine yenye msisimko ni katika vita ya ufungaji ambapo hadi sasa anayeongoza ni mshambuliaji wa Mtibwa, Raizin Hafidh mwenye mabao 11, akifuatiwa na Abdulaziz Shahame wa TMA na Andrew Simchimba wa Geita Gold wenye tisa kila mmoja. Wengine ni Naku James (Mbuni FC) mwenye saba, Seif Adam (Mbeya Kwanza) sita, huku Said Fundi (Cosmopolitan), Msenda Msenda (Stand Utd), Ramadhan Kapera (TMA FC) na Andrew Chamungu wa Songea Utd wakifunga 5.

Kocha wa Bigman, Zubery Katwila anasema hadi sasa ushindani umekuwa mkubwa kutokana na mahitaji ya kila timu ingawa Ligi itakaporejea itakuwa ngumu zaidi, huku akitabiria mzunguko wa pili utakuwa mgumu kwani ndio lala salama kwa msimu huu.

“Tunapoenda ndio pagumu zaidi kwa sababu hata ukikutana na timu za chini nazo pia zinahitaji kujinasua, ushindani ni mzuri na unaongeza msisimko wa Ligi hivyo, kwetu bado tunaendelea kuimarisha kikosi kutokana na mapungufu yaliyokuwapo.”

Related Posts