Gadiel aitosa Chippa United | Mwanaspoti

BEKI wa kushoto wa kimataifa wa Tanzania, Gadiel Michael ameachana na Chippa United ya Afrika Kusini huku sababu za kuondoka klabuni hapo hazijulikani.

Nyota huyo wa zamani wa Simba na Yanga ambaye wakati mwingine amekuwa akitumika kama kiungo ndani ya timu hiyo ya Chippa, alijiunga na timu hiyo msimu huu kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Cape Town Spurs ya nchini humo.

Akizungumza na Mwanaspoti, msimamizi wa Abdi Banda aliyewahi kucheza Ligi hiyo, Fadhili Omary Sizya alisema sababu za kusitisha mkataba hazijajulikana hadi sasa.

“Sijapata zaidi sababu ni nini lakini taarifa nilizopata ni makubaliano ya pande zote mbili, wameelewana na hata hivyo mkataba wake ulibaki muda mchache,” alisema Sizya.

Hata hivyo, Mwanaspoti lilipomtafuta beki huyo wa kushoto huyo ambaye aliwahi kucheza Azam FC, hakupokea simu.

Chippa ilikuwa na Watanzania wawili na baada ya kuondoka kwa Gadiel amesalia Baraka Majogoro akiwa Mbongo pekee anayecheza katika ligi hiyo baada ya Abdi Banda kuondoka Baroka FC.

Banda alipita Chippa na msimu 2022 alifunga bao pekee lililoipa pointi tatu timu hiyo dhidi ya Orlando Pirates.

Related Posts