Gaza. Kundi la Hamas limevujisha kipande cha video kinachomwonyesha mwanajeshi wa Israel wanayemshikilia mateka katika eneo la Gaza tangu lilipotekeleza shambulizi la kushtukiza nchini Israel Oktoba 7, 2023.
CNN imeripoti kuwa, Liri Albag, ambaye ameelezwa na vyombo vya habari nchini Israel kama mwanajeshi mwenye umri wa miaka 19 sasa, wakati anatekwa alikuwa na miaka 18.
Alitekwa na wapiganaji wa kundi hilo akiwa karibu na Kambi ya Kijeshi ya Nahal Oz iliyoko karibu na mpakani mwa Gaza, akiwa na wanawake wenzake sita, watano kati yao bado wanashikiliwa mateka eneo la Gaza.
Video hiyo ambayo haionyeshi tarehe ya kurekodiwa, ina urefu wa dakika tatu na nusu, inamuonyesha, Albag, ambaye ametimiza miaka 19, akiomba msaada wa taifa lake kumrejesha uraiani.
Kundi la familia ambazo wapendwa wao walitekwa na Hamas, limesema familia ya mwanajeshi huyo haijaruhusu kipande cha video ya mtoto wao kichapishwe kwenye mitandao.
Familia hiyo imesema, “Ile video imeukata moyo wetu vipande vipande,” huku ikiongeza “huyu siyo binti na dada yetu tunayemjua. Anaonekana amepitia mateso makubwa ya kisaikolojia.”
“Tunamuomba Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, viongozi wa dunia na watu wanaofanya uamuzi, wakati umefika kufanya uamuzi kama vile wanaoshikiliwa mateka Gaza ni watoto wenu,” imesema taarifa ya familia hiyo.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Nwtanyahu akizungumzia video hiyo, alisema vikosi vya jeshi la nchi hiyo (IDF) vinafanya kila viwezalo bila kuchoka ili kuwarejesha mateka nyumbani kwao.
“Kila atakayejaribu kumdhuru raia wetu wanayemshikilia mateka atawajibishwa kwa matendo yake,” alisema Netanyahu.
Netanyahu yuko kwenye msukumo mkubwa hususan kutoka kwenye familia ambazo ndugu zao wamechukuliwa mateka ambazo zinamshinikiza kuingia makubaliano na kundi la Hamas ili kufanikisha kuachiwa kwa wapendwa wao.
Israel imekuwa chini ya maandamano makubwa yaliyoratibiwa na ndugu wa waliotekwa na Hamas wakishinikiza kufanyika mazungumzo ya kuachiwa mateka hao. Maandamano yaliyotikisa zaidi yalifanyika nje ya makazi ya Natanyahu jijini Tel Aviv nchini humo.
Wakosoaji wake wamekuwa wakimtuhumu Netanyahu kwa kukwamisha makubaliano ya kuachiwa kwa mateka hao.
Hamas na kundi washirika la Islamic Jihad wamekuwa wakivujisha video za mateka wa Israel wanaowashikilia eneo la Gaza katika kipindi cha miezi 15 ya mapigano kati ya pande hizo.
Kundi hilo, liliwachukua raia 251 wa Israel kama mateka mwaka 2023, hadi sasa takriban raia 96 wanaendelea kushikiliwa eneo la Gaza. Israel inasema 34 kati yao wamefariki na hivyo kufanya ambao bado wanashikiliwa kuwa 62.
Kipande cha video hiyo kimevuja wakati ambao mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya pande hizo yameanza nchini Qatar ambapo wapatanishi kutoka Qatar, Egypt na Marekani wamekuwa wakipambana kwa miezi sasa kumaliza vita hiyo.
Wakati hayo yakiendelea, Wizara ya Afya ya Palestina imesema takriban watu 70 wameuawa katika mashambilizi ya Israel eneo la Gaza tangu Ijumaa Januari 3, 2025.
Kati yao, watu 17 waliuawa katika shambulizi lililotekelezwa kwenye nyumba ya makazi mjini Gaza katika familia ya Al-Ghoula.
“Wengi wa waliofariki ni wanawake na watoto, wote ni raia, hakuna hata mmoja aliyewahi kushika silaha wala kurusha kombora ama kuonyesha upinzani dhidi ya Israel,” alisema jirani wa familia hiyo, Ahmed Ayyan alipozungumza na Shirika la Reuters.
Hadi sasa, Jeshi la Israel halijatoa kauli yoyote kuhusiana na madai ya kutekeleza mauaji hayo.
Katika hatua nyingine, Kitengo cha Dharura cha Palestina kimesema, shambulizi lingine la IDF lililenga nyumba ya makazi eneo la Mji wa Gaza na kuuwa watu watano wa familia moja Jumamosi Desemba 4, 2025.
Kitengo hicho pia kimesema watu takriban 10 wanahofiwa kuwa chini ya kifusi kilichosababishwa na shambulizi hilo huku kikisema jitihada za kuwatoa zinaendelea.
Jeshi la Israel, wiki iliyopita, lilitoa taarifa kuwa linaendeleza mashambulizi eneo la Beit Hanoun Kaskazini mwa Gaza ambako limekuwa likifanya operesheni zake kwa wiki tatu mfululizo na limefanikiwa kulisambaratisha kundi hilo.
Israel ilianzisha operesheni dhidi ya Hamas eneo la Gaza Oktoba 7, 2023, muda mfupi tangu Hamas ivamie eneo la mpakani mwa mataifa hayo na kuwaua watu takriban 1,200 huku likiwakamata zaidi ya 250 kama mateka.
Al Jazeera imeripoti kuwa hadi leo Jumapili, idadi ya vifo vya Wapalestina wa Gaza waliouawa katika mashambulizi ya Israel imefikia watu 45,658 wengi wao ni wanawake na watoto na watu 108,583 wamejeruhiwa.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika