WAKATI mabosi wa Fountain Gate wakiendelea kusaka kocha mpya baada ya kumtimua Mohamed Muya, pia wako katika hesabu za kumpata aliyekuwa kiungo wa Mbeya City, Yanga na Singida Black Stars (zamani Ihefu), Rafael Daud Loth.
Hesabu za mabosi hao zinajiri baada ya dili la Nassor Kapama kutoka Kagera Sugar kuonekana linaleta shida kutokana na uongozi wa ‘Wanankurunkumbi’ kugoma kumuachia, licha ya kocha mkuu wa kikosi hicho, Melis Medo kudaiwa kumpa ruhusu ya kuondoka.
“Kipaumbele cha kwanza ni kumpata Kapama na tayari tulishampa mkataba wa miezi sita, shida imetokea baada ya uongozi wa Kagera Sugar kugoma kumpa barua ya kumuachia, ikishindikana tutamsajili Loth kama mbadala wake,” kilisema chanzo.
Mwanaspoti linatambua nyota huyo amefanya mawasiliano na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate, Kidawawa Tabitha katika ofisi zake zilizopo jengo la Mwanga, Makumbusho jijini Dar es Salaam, ingawa hakuna makubaliano yaliyofikiwa.
Mabosi wa Fountain wanaona Loth ni mbadala sahihi ikiwa dili la Kapama litashindikana, huku ikichagizwa kwa sasa nyota huyo yupo huru baada ya kuachana na ‘Wauaji wa Kusini’ Namungo, jambo linalotengeneza mazingira rahisi ya kupatikana.
Tayari timu hiyo imenasa saini ya Said Mbatty na Faria Ondongo waliotokea Tabora United, Jackson Shiga (Coastal Union), Mtenje Albano (Dodoma Jiji), Jimmyson Mwanuke (Singida Black Stars) na winga, Kassim Haruna ‘Tiote’ akiwa mchezaji huru.
Wengine ni Shabani Pandu Hassan, Mudrik Abdi Shehe ‘Gonda’ (JKU), Daniel Joram ‘Gustavo’, Kelvin Nyanguge, Paulo Godwin Ulomi kutoka Pamba Jiji na mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Coastal Union, Yusuph Athuman aliyesajiliwa akiwa mchezaji huru.