Kipindupindu chaitesa Mbeya, RC atoa maagizo

Dar/Mikoani. Wakati ugonjwa wa kipindupindu ukitajwa kuwapo katika halmashauri tatu za Mkoa wa Mbeya, mkuu wa mkoa huo, Juma Homera ametoa maelekezo kwa wakuu wa wilaya na kamati za afya.

Pia amesema wakati mkoa huo ukiendelea kujipanga kukabiliana na ugonjwa huo, tayari maofisa wa Wizara ya Afya wametua mkoani humo kuongeza nguvu kuokoa maisha ya wananchi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Januari 5, 2025, Homera amesema halmashauri zilizokumbwa na mlipuko wa ugonjwa huo ni Mbeya Jiji ambayo hali yake iko juu, Chunya na Mbeya Vijijini.

Amesema kutokana na hali ilivyo, amewaelekeza wakuu wa wilaya hizo kuketi haraka na kamati za afya kuhakikisha wanakabiliana na ugonjwa huo, ikiwamo shuleni na vyuoni.

“Hatua tulizochukua ni kufunga migahawa ambayo haina viwango, usitishaji vyakula maeneo ya mikusanyiko, ikiwamo harusini, kuwatenga wagonjwa maeneo maalumu, kamati za afya zijipange kudhibiti ugonjwa huu na kuzuia bidhaa kupangwa chini na kueleza kuwa wanaohusika na uzoaji taka lazima waongeze kasi kwa kuzoa kwa wakati.

“Katika kikao cha Januari 3, nimeelekeza wakuu wa wilaya zote pamoja na maofisa afya wakae kikao na wakuu wa shule zote binafsi na Serikali ndani ya siku saba kujadili namna ya kukabiliana na hali hiyo kwa kuwa shule zinakwenda kufunguliwa” amesema Homera.

Amesema ametoa maelekezo kwa mamlaka ya maji kuongeza kasi ya uzalishaji, huku akipiga vita wananchi kujichimbia visima bila kibali, ikiwamo maeneo ya machimbo.

Kuhusu kuwapo vifo, amesema kama taarifa hizo zipo, bado hazijaripotiwa.

 “Kama kuna vifo basi havijaripotiwa, nashukuru Wizara ya Afya imefika Mbeya kuongeza nguvu, visima vya kienyeji tumepiga marufuku hadi kuwepo vibali” amesema Homera.

Mara ya mwisho, Desemba 19, mwaka jana, taarifa ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dk Yesaya Mwasubila ilieleza kuwa wagonjwa kufikia 46.

Alieleza maeneo yaliyoathirika na ugonjwa huo ni kata 18 kati ya 32 za jiji hilo, ikiwamo maeneo ya vyuoni, huku akiomba wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Siku tatu baadaye, taarifa zilizothibitishwa na Serikali ya mtaa wa Ilolo kulitokea vifo vya watu watatu, wakiwamo wawili wa familia moja wanaodaiwa kufariki dunia kwa ugonjwa wa kipindupindu.

Kauli za wenyeviti iwa mitaa

Mwenyekiti wa Mtaa wa Makunguru, Sheyo Thabiti amesema hali si nzuri, akieleza kwa sasa wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi namna ya kujikinga na kuchukua tahadhari.

Amesema mtaani kwake tayari yupo mgonjwa mmoja ambaye alipata huduma na kurudi nyumbani, kuhimiza ushirikiano kutoka kwa wataalamu wanaofika maeneo ya mtaa huo kutoa huduma.

“Alikuwepo mgonjwa mmoja, lakini alipata huduma, japokuwa nilipata changamoto kwa wataalamu waliofika mtaani kwangu kupulizia dawa na hawakunipa ushirikiano. Hili suala si la kisiasa wala mzaha,” amesema Thabiti.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilolo, Ezekiel Mwasandube, amesema wameendelea kutoa elimu tangu kutokea vifo hivyo, akieleza kuwa wanakagua maeneo machafu na kuyafungia.

“Sehemu zilizokuwa na changamoto tulifikiria kuzifunga kwa kutoa saa 48, hali hii haiwezi kukubalika lazima kila mmoja achukue tahadhari na hatua kukabiliana na ugonjwa huu,” amesema Mwasandube.

Munira Jamilu, amesema kwa sasa wanapata hofu kwa kuwa shule zinakwenda kufunguliwa, akieleza huenda kukawapo muitikio mdogo kwa wananchi kupeleka watoto shule.

“Hatujasikia kauli yoyote ya Serikali kama maeneo ya shuleni kuna tahadhari gani, kimsingi inatupa hofu kwa kuwa mara ya mwisho walitaja maeneo ya vyuo kuwapo ugonjwa huu,” amesema Munira.

Victoria Njema, amesema changamoto kubwa ni uhaba wa maji safi akieleza Serikali iboreshe miundombinu hiyo kuondokana na tatizo hilo.

“Maji ni ya visima na hatuna uhakika na usalama wake, watoto wetu hata huko shuleni hatujui hatima yao, kipindupindu kinaenezwa, sasa tupate kauli ya viongozi” amesema Victoria na kuongeza;

“Yaani tunaishi kwa mashaka makubwa, kumekuwa na maeneo taka zinakaa muda mrefu haziondolewi na kusababisha mazalio ya wadudu na harufu nyakati za mchana,” amesema Athanas John.

Naye Peter Daniel, amesema kumekuwepo na adha ya chemba za maji taka kuzidiwa na kutiririshwa kwenye mito ambayo baadhi ya wananchi hutumia kwa matumizi ya majumbani.

“Kuna chemba ipo hapo makaburi ya Sabasaba inapasuka kila wakati na kutiririshwa kwenye maji Mto Meta ambayo maji yake wananchi wa mitaa inayopitiwa na mto huo hutumia kwa matumizi mbalimbali,” amesema.

Related Posts