Kocha Yanga afichua siri ya Mpanzu

KOCHA wa zamani wa Yanga na AS Vita ya DR Congo aliyewahi kumfundisha, winga mpya wa Simba, Elie Mpanzu amefichua kama Wekundu wa Msimbazi wanataka kumfaidi vilivyo nyota huyo basi kocha Fadlu Davids anapaswa kumtumia tofauti.

Kocha huyo,  Raoul Shungu aliyasema hayo jana alipozungumza na Mwanaspoti kutoka DR Congo akieleza namna Simba ilivyolanda dume kumsajili Mpanzu ambaye usiku wa leo anatarajiwa kuwepo katika kikosi kitakachovaana na CS Sfxaien ya Tunisia kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Shungu aliyewahi kuingoza Yanga katika Nane Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika 1998, alisema Mpanzu anakuwa mtamu zaidi akicheza kama mshambuliaji namba 10.

Winga huyo Mkongomani alitua Simba akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na AS Vita kumalizika – baada ya kufeli majaribio katika Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.

Mkongomani huyo tangu atue Simba amecheza mechi tatu za ligi akifikisha jumla ya dakika 186, huku akiwa hana rekodi ya kufunga bao wala kutoa asisti, lakini Shungu alisema hana wasiwasi na winga huyo na kwamba akishazoea kidogo tu mabao yatakuja.

Alisema kocha wa Simba kama anataka kuona ubora wa haraka wa Mpanzu asimchezeshe pembeni, lakini akimuweka kama namba kumi hapo ataona ubora wake wa haraka kwa kuwa ni hatari anapokuwa karibu na uso wa lango.

“Simba bado hakuna mtu bora anayetumia mguu wa kushoto kumshinda Mpanzu, hivyo ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri. Jambo zuri ni kwamba Simba inacheza soka la kutengeneza nafasi nyingi kitu ambacho kitamsaidia Mpanzu,” alisema Mpanzu.

Mpanzu katika nafasi  anayocheza kwa sasa yupo pamoja na Kibu Denis, Edwin Balua, Ladaki Chasambi na Joshua Mutale, lakini kama akitumika namba 10 atakuwa na kibarua mbele ya Jean Ahoua na Awesu Awesu ambao wamekuwa na rekodi ya kucheza katika kikosi cha kocha Fadlu.

Nyota huyo aliingizwa katika usajili wa Simba mechi za ndani na zile za kimataifa hivi karibuni kupitia dirisha dogo la usajili lililofunguliwa Desemba 15, licha ya kutambulishwa mapema mara tu baada ya kufungwa kwa dirisha kubwa la usajili akitokea Genk alikoenda kufanya majaribio na kuchemka.

Related Posts