Mtalii afariki dunia, watano wajeruhiwa ajalini Ngorongoro

Arusha. Mtalii mmoja raia wa Israel ambaye jina lake halijafahamika (mwanamke) amefariki dunia huku wengine watano wakijeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumapili Januari 5, 2025 na Kaimu Meneja wa Uhusiano wa Umma wa NCAA, Hamis Dambaya imeeleza ajali hiyo imetokea jana Jumamosi Desemba 4, 2025 saa 8:45 mchana.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa ajali hiyo ilihusisha gari ya utalii inayomilikiwa na kampuni ya Wakali Safaris lililokuwa na namba za usajili T 450 APB.

“Ajali hii imetokea kati ya viewpoint na lango kuu la Loduare ambapo gari hilo lilikuwa na watu saba ambao kati yao sita ni raia wa Israel na mmoja ni Mtanzania ambaye ni dereva wa gari hilo,” imeeleza taarifa hiyo.

“Ajali hiyo imesababisha majeruhi watano na mmoja amefariki (mwanamke), hali ya dereva ni mzima na anaendelea vizuri,” imeongeza kueleza taarifa hiyo.

Dambaya amesema baada ya ajali hiyo kutokea majeruhi wa ajali hiyo walipelekwa katika Hospitali za Lutherani na Fame zilizopo wilayani Karatu kwa huduma ya kwanza na baadaye kusafirishwa kwenda Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC), maarufu Selian kwa matibabu zaidi.

NCAA imewakumbusha madereva wote wa magari ya utalii kuzingatia sheria za barabarani na za hifadhi ili kuendelea kuwa salama kwa wageni na vyombo wanavyotumia wakati wote wanapokuwa hifadhini.

“Mamlaka itaendelea kutoa taarifa kadri inavyowezekana, tunaomba Mungu awawezeshe majeruhi wapone haraka,” ameeleza Dambaya katika taarifa hiyo.

Related Posts