Anti habari, naomba unisaidie mawazo na mbinu maana hili limenishinda kabisa.
Sijisifii, ila ni mzuri wa sura, umbo la kuvutia na nina kazi nzuri inayonipatia kipato cha kukidhi mahitaji yangu na kusaza.
Pia sijifichi ndani kama utumbo, najua kujichanganya kwenye kupoteza mawazo kama wafanyavyo wengine.
Changamoto niliyonayo sipati mwanamume anayeonyesha nia ya kwenda mbali na mimi kimaisha.
Kila ninayempata kwenye mazungumzo tu ninajua hana mpango wa kwenda na mimi mbali. Pamoja na kwamba napenda wanaume wenye umri kama wangu, yaani kati ya miaka 28 wasizidi 30 ila sijapata mwenye nia njema.
Awali nilikuwa nawapata ninapokwenda kupoteza mawazo (kwenye starehe) nikaona huku sitotoboa, nikahamia kwenye nyumba za ibada nako sikuona mwelekeo.
Sasa nimempata anayefanya kazi kama yangu, lakini kwenye kanda nyingine, naye licha ya kunipenda na kusifia, kushauri kwa wema kila ninachokifanya, ikiwamo kusimamia baadhi ya miradi yangu sijawahi kumsikia akizungumzia kunioa wala kutaka tupate mtoto pamoja.
Akipata nafasi ananipeleka kila mahali, lakini siyo kufikiria maisha yetu kama wanafamilia wajao. Hiki kitu kinaniuma sana. Huko siku za nyuma kuna mmoja niliyedumu naye miaka minne alinipeleka kwao, ilikuwa sikukuu za mwisho wa mwaka kama hivi.
Tulipofika baada ya muda ndugu zake walimwita ndani, sikujua walizungumza naye nini, lakini baada ya hapo sikuona tena ile kasi ya kutaka niwe karibu naye na familia yake. Nikaamua kujitoa.
……..Duh! Mtihani kidogo huu. Ila kwanza kabisa inaonekana ukikutana na mtu unawaza akuambie mambo ya kuoana ndiyo maana umeishia kuwa nao wengi. Pia unachagua sana, wenye umri huo unaosema wengi wao (siyo wote), nao wanajitafuta hawajajipanga kuoa.
Jitulize, tulia kabisa mumeo anakuja tena hatokuja na mbwembwe kama hao waliopita, ndoa ni mipango ya Mungu hivyo wakati wa Mungu ni wakati sahihi.
Mambo uliyonayo kama pesa, kazi, elimu si vigezo vya kupata mwenza wa kukuoa, ukijipima kwa hayo, kila atakayekuja utamuona hana nafasi ya kwenda mbali na wewe.
Kukosa mume wa kukuoa licha ya kuwa mzuri ni mada inayoweza kuleta hisia tofauti kwa watu wengi, na inaweza kutajwa kama changamoto katika maisha ya kijamii. Katika jamii nyingi, uzuri unachukuliwa kama njia ya kwanza ya mafanikio katika uhusiano wa kimapenzi.
Hata hivyo, ukweli wa hali halisi unadhihirisha kwamba uzuri pekee hautoshi kuleta mahusiano thabiti. Wanaume wana vigezo vya mke wa kuoa na vinatofautiana wakati wengine wanaona uzuri wa kimwili, wengine wanathamini uzuri wa ndani kama vile tabia njema, hekima, na uaminifu.
Katika muktadha huu, mtu anayeonekana mzuri katika muonekano wa nje anaweza kuwa na mapungufu katika tabia au maadili ambayo yanaweza kuathiri uhusiano wake na wengine.
Hivyo, uzuri wa ndani ni muhimu zaidi na mara nyingi hujenga msingi wa mahusiano mazuri. Ninachomaanisha hapa ni kuwa unapotafuta uhusiano wa kudumu hadi kufunga ndoa mambo ya uzuri, nina hiki nina kile achana nayo.
Soma tabia za uliyenaye anapenda nini na hapendi nini.
Pia si vibaya ukianzisha wewe mijadala ya ndoa ukiwa na umpendaye, pengine unaokuwa nao wanakuogopa kutokana na sababu mbalimbali, wanahisi wakikuambia wanataka kukuoa watakupoteza.
Kisha sifa ya mwanamke ni kujituliza pamoja na kutafuta wa kufunga naye ndoa, hakikisha hutaingia kwenye uhusiano na wanaume wengi, mwisho wa siku utapata anayetaka kukuoa akupeleka kwao kumbe ulishatoka na kaka yake, uikose ndoa.
Mwisho lakini si kwa umuhimu acha kufikiria sana ndoa, kuchagua wanaume, kujizururisha kwenye kumbi za starehe (sijasema usiupe pole mwili ila kwa kiasi), kisha muombe Mungu atakupa mume bora, kwani bila yeye haya mengine mi mazungumzo tu.