Polisi yaanza kufuatilia kupotea kwa Mutajura, gari yake yadaiwa kutelekezwa Buza

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linafuatilia taarifa za madai ya kutekwa kwa Dastan Mutajura na watu wasiojulikana jana Jumamosi Januari 4, 2025.

Mutajura anadaiwa kutekwa saa 4 asubuhi jana, maeneo ya Sigara, Tanesco, Buza jijini Dar es Salaam wakati akitokea nyumbani kwake, eneo la Kitunda.

Taarifa iliyoambatana na picha ya Mutajura iliyosambaa mitandaoni inaeleza watu hao wasiojulikana walilizuia kwa mbele gari aina ya Mercedes Benz C300 alilokuwa akiliendesha.

Kwa mujibu taarifa hiyo gari hilo lilikutwa  limetelekezwa eneo la Buza Sigara.

Katikati ya mjadala huo, asubuhi ya leo Jumapili, Januari 5, 2025, Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam inayoongozwa na Kamanda Jumanne Muliro imetoa taarifa ikisema inalifuatilia.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Januari 4, 2025 saa 8:00 mchana lilipokea taarifa toka kwa wananchi ya kuonekana kwa gari aina ya Mercedes Benz lenye namba za usajili T 109DVY likiwa limetelekezwa eneo la Buza Sigara. Taratibu zilifanyika na gari hilo kuvutwa hadi kituo cha Polisi Buza,” imesema taarifa hiyo.

“Ufuatiliaji zaidi wa kutoonekana kwa Dastan Daud Mutajura unaendelea,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Related Posts