Russia yaidungua ndege ya Ukraine, Blinken aikatia tamaa

Moscow. Vikosi vya Russia vimedungua ndege ya kivita ya Ukraine aina ya MiG-29, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumapili Januari 5, 2025 na Wizara ya Ulinzi ya Russia.

Wizara hiyo imesema vikosi vya Ukraine, pia, vimepoteza makombora kadhaa yaliyotengenezwa katika mataifa ya magharibi ikiwemo gari ya kivita aina ya Bradley.

“Mashambulizi 17 yaliyorushwa na adui yetu Ukraine yamedhibitiwa. Vikosi vyao vimepoteza zaidi ya wanajeshi 410, vifaru viwili aina ya Leopards vilivyotengenezwa Ujerumani, gari la kurushia makombora na magari matatu ya kubebea wanajeshi ikiwemo gari aina ya M113 iliyotengenezwa Marekani,” taarifa hiyo imesema kutokea Mkoa wa Donetsk unaoshikiliwa na vikosi vya Russia.

Ukraine, pia, imepoteza kombora aina ya L-119 lenye kipenyo cha milimita 105 lililotengenezwa nchini Uingereza,” imeeleza taarifa ya wizara hiyo.

Tovuti ya Russia Today, imeripoti kuwa katika moja ya kambi, Ukraine imepoteza wanajeshi 230 katika mashambulizi ya kushtukiza yaliyofanywa mapema leo Januari 5, 2024 na vikosi vya Russia.

Idadi kubwa ya ndege za Kisovieti aina ya MiG-29 zimepelekwa Kiev nchini Ukraine na washirika wake ambao ni kutoka mataifa ya Jumuiya ya Ulaya tangu Februari 2022, Russia ilipotangaza kuanza operesheni zake za kijeshi nchini humo.

Tovuti hiyo pia iliripoti kuwa Poland iliipatia Ukraine ndege kadhaa za kivita za Kisovieti mwaka 2023, hata hivyo, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Poland, Pawel Zalewski alisema ndege za kivita aina ya F-35  zilizotengenezwa nchini Marekani utakuwa mbadala wa ndege hizo.

Hata hivyo, Desemba 2024, Zalewski alisema Poland haitopeleka ndege zake za kivita zilizobaki nchini Ukraine ili kutohatarisha usalama wake.

Hadi sasa Marekani na Umoja wa Ulaya umeshaipatia Ukraine misaada ya kijeshi, kifedha na silaha inayokadiriwa kufikia Dola za Marekani 100 bilioni tangu kuanza kwa mzozo huo Februari 2022, huku yakisisitiza kuwa yanatoa msaada huo siyo kwa lengo la kuchochea mzozo huo.

Wakati Russia ikidungua ndege hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken amesema kwa jinsi hali ilivyo katika mzozo huo, haoni nafasi ya Ukraine kuyarejesha maeneo yaliyotwaliwa na vikosi vya Russia.

Tangu kuanza operesheni hiyo, vikosi vya Russia vimeutwaa Mkoa wa Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporizhia, sehemu ya Pokrovisk na Crimea iliyotwaliwa tangu mwaka 2014.

Blinken ambaye leo Jumapili Desemba. 5, 2024, ametoka nchini Korea Kusini kuzungumza na uongozi wa taifa hilo kuhusu mzozo wa kisiasa unaendelea nchini humo, alitoa kauli hiyo jana alipokuwa Uarabuni.

Alisema: “Hadi sasa vikosi vya Russia vilipofika nchini Ukraine katika ramani sioni kama kuna kitu kitabadilika, japo Ukraine itapoteza maeneo yake ila yatasalia kuwepo,” 

Kuhusu kukomesha vikosi vya Russia kuendelea kutanua wigo wa uvamizi huo, Blinken alisema namna pakee ya kuilinda Ukraine ni kuiruhusu na kuitambua kama mwanachama wa Jumuiya ya Kujilinda wa NATO.

Alisema hadi sasa Marekani haioni mwanga kuhusiana na suala la kufanyika mazungumzo ya amani na ya kidiplomasia kati ya Russia na Ukraine kuhusu vita hiyo. 

“Bado hatujaona njia nzuri inayoweza kumaliza vita hii kwa amani na ndani ya muda uliopo,” alisema.

Ukraine na Russia zilifikia makubaliano ya amani kuhusiana na mzozo huo kwa mara ya kwanza mwaka 2022 jijini Instanbul, Uturuki.

Mazungumzo hayo yaliratibiwa na Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo, Boris Johnson ambapo Ukraine ilijiondoa baada ya kugomea kushindwa na kusema itashirikiana na mataifa ya Ulaya kuishambulia Russia.

Hata hivyo, Russia bado inaamini nafasi ya kumaliza mzozo huo bado ipo ambapo inashinikiza masharti yake yazingatiwe ikiwemo kuitaka Ukraine kuachana na mpango wa kujiunga na NATO, Rais Volodymyr Zelenskyy kuitisha uchaguzi utakaomweka madarakani kwa kura halali kwa kile alichodai yuko madarakani sasa hivi kwa sheria ya kijeshi (Martial Law).

Pia, Vladimir Putin anaitaka Ukraine kuachana na matumizi ya silaha na makombora iliyopewa na NATO na Marekani kuishambulia Russia la sivyo, Russia haitosita kupeleka mashambulizi kwa taifa lolote lile ambalo silaha yake itatumiwa na Ukraine kuishambulia sehemu ya Russia.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika

Related Posts