Saido atoa masharti ya kutua KenGold

WAKATI mabosi wa KenGold wakipigia hesabu za kumsainisha aliyekuwa kiungo wa Yanga na Simba, Mrundi Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’, nyota huyo ameweka masharti mapya kwa viongozi wa timu hiyo ya jijini Mbeya ili akaitumikie kwa miezi sita.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo, zimeliambia Mwanaspoti ‘Saido’ anahitaji pesa ya usajili Sh50 milioni na mshahara wa Sh12 milioni kwa mwezi, ingawa viongozi bado hawajafikia makubaliano rasmi juu ya kiasi hicho cha fedha anachokihitaji.

“Kwenye pesa ya usajili sio ishu sana ingawa mshahara ndio changamoto kwa sababu viongozi wanataka wampe Sh4 milioni na hii ni kutokana na kutocheza kwa muda mrefu, bado wanaendelea na mazungumzo juu ya suala hilo,” kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho ambazo kiliomba kuhifadhiwa jina lake, kilisema viongozi wanaamini uwezo wa mchezaji huyo kwa kushirikiana na nyota wengine, utaleta chachu ya kukinusuru kikosi hicho na janga la kushuka daraja hivyo wanapambana kuinasa saini yake.

Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kengold, Benson Mkocha alisema kwa sasa asingependa kuzungumza jambo lolote juu ya usajili kwa sababu bado hawajakamilisha, ingawa ni kweli taratibu hizo zimeanza kutokana na matakwa ya benchi la ufundi.

“Tukikamilisha taratibu zote tutaweka wazi kwa sababu bado mchakato unaendelea na kama unavyojua hiki ni kipindi ambacho ushindani ni mkubwa kutokana na mahitaji ya kila timu, endeleeni kuvuta subira tukikamilisha mtaona mambo yote,” alisema.

Nyota huyo aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara 2022-23 aliyoanza kuyafunga akiwa na Geita Gold na kumaliza msimu na Simba. Dili lake likitiki ataungana na nyota wa Yanga na Simba, Bernard Morrison.

Related Posts