Sera ya uchumi wa buluu kutekelezwa kisayansi

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imedhamiria kuitekeleza kisayansi sera ya uchumi wa buluu, hivyo itaweka nguvu katika tafiti za rasilimali za bahari.

Dk Mwinyi amesema hayo leo Jumapili, Januari 5, 2025 wakati uwekaji wa jiwe la msingi katika jengo la taaluma na utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS) inayojengwa chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET) unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Dk Mwinyi amesema tukio hilo linafanyika katika sherehe za miaka 61 za Mapinduzi ya Zanzibar, hivyo SMZ itaendelea kutoa ushirikiano.

“Sera yetu kuu ni sera ya uchumi wa buluu ambayo ndani yake kuna sekta ya utalii, uvuvi, ukulima wa mwani na nyingine kadhaa, hivyo taasisi hii ina umuhimu wa pekee, itatupatia wataalamu kwenye sekta mbalimbali za uchumi wa buluu.”

“Matarajio yetu, chuo hiki kitatupatia matokeo ya tafiti mbalimbali zinazofanywa katika uchumi wa buluu. Kwa kuwa sera yetu ni uchumi wa buluu tunataka kuwa na sera zinazotokana na matokeo ya kisayansi ili kutengeneza sera zitakazoleta maendeleo,”amesema Mwinyi.

Mkuu wa UDSM, Rais mstaafu Jakaya Kikwete ametoa shukrani kwa Serikali zote mbili kwa kuwezesha ujenzi huo.

“Bila uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kukubali taasisi ya IMS iingizwe kwenye mradi wa HEET, tusingefika hatua hii, haikuwa rahisi kujumuisha taasisi hii kwenye mradi huu. Ilibidi kwenda kuiona mamlaka nikazungumza na Rais Samia akaniambia nisiwe na wasiwasi, taasisi ikaingia kwenye mradi. 

“Tunashukuru pia, uamuzi wa busara wa Rais Mwinyi uliotuwezesha kupata hati miliki ya ardhi ya eneo hili la Buyu. Bila uamuzi wa Rais nafikiri hadi sasa jambo hili lingekuwa halijakamilika maana limechukua miaka mingi,” amesema Kikwete.

Amesema kwa mujibu wa utaratibu wa Benki ya Dunia, fedha za ujenzi zisingeweza kutolewa kama Serikali haina hati miliki ya ardhi ya eneo husika.

“Ilitubidi tutafute hati katika maeneo yote ambayo tunajenga kampasi kwa kufuata taratibu, tulipozipata ndipo tukapeleka kwa wakubwa, Benki ya Dunia wakatupatia fedha hatimaye ujenzi ukaanza,” amesema Kikwete.

“Binafsi najituma sana kuhakikisha nasimama kikamilifu kwenye kazi yangu ya ukuu wa chuo, wenzangu waliniamini wakanipa jukumu hili kwa sababu nisipofanya hivyo, wataona kama sichukulii kwa umakini.”

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Profesa Adolf Mkenda amesema katika mradi wa HEET kampasi mpya 16 zinajengwa mikoa 16 nchini ili kusogeza elimu ya juu.

Profesa Mkenda amevielekeza vyuo vikuu na kampasi zinazoanzishwa kutoa shahada za mafunzo ya kazi ili kuwezesha wahitimu wengi kujiajiri ikiwa ni sehemu ya jitihada na changamoto ya ukosefu wa ajira.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa amesema mitalaa ya elimu ya SMZ kuanzia ngazi ya msingi na sekondari imeandaliwa kuhakikisha inawatengeneza wanafunzi wenye sifa za kujiunga katika vyuo vya uvuvi na sayansi za bahari ili wawe na ushiriki imara kwenye  uchumi wa buluu.

“Tunataka wazawa wapate fursa za kujiunga na vyuo hivi ili wawe na utaalamu wanapofanya shughuli zozote za kiuchumi zinazohusu bahari. Watoto wanaozaliwa Zanzibar tayari wana stadi za uvuvi tunachokifanya ni kuwaongezea misingi ya kitaaluma katika eneo hili kuziba pendo lililopo.

“Mtoto aliyezaliwa Kojani, Tumbatu na ukanda huu wa Forodhani huwafundishi kupiga makachu wala kuvua, tunachokifanya ni kuwaongezea ujuzi wa kitaalamu ili waweze kuvua kitaaluma na waingie kwenye shughuli kibiashara,” amesema Lela.

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Wiliam Anangisye amesema lengo la ujenzi huo ni kuongeza uwezo wa taasisi na idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kutoka 140 wa sasa hadi kufikia 300.

Amesema  kukamilika kwa ujenzi huo kutakifanya chuo kuongeza  fursa ya kuambatanisha wanataaluma kwenye sekta kulingana na programu zinazofundishwa.

Profesa Anangisye amesema matarajio ya taasisi hiyo ni kuongeza uwezo wake wa kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu kwenye eneo la uchumi wa buluu na sayansi za bahari.

“Hatua ya ujenzi imefikia asilimia 50 na mkandarasi ameshalipwa Sh4.2 bilioni na kazi inaendelea. Tumejipanga kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati ili matunda yake yaanze kupatikana hasa kwenye eneo la uchumi wa buluu,” amesema Profesa Anangisye.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia ambayo ndiyo wafadhili wa mradi wa HEET, Martin Kachingwe amesema taasisi hiyo inajivunia kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwekeza kwenye elimu kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi elimu ya juu.

“Lengo la mradi wa HEET ni kuifikisha elimu kwa watu wengi, hasa wale walio maeneo ya pembezoni na wenye mahitaji maalumu. Tunaona hili linafanyika kampasi zinajengwa ili kuongeza wigo wa vijana wengi kujiunga na elimu ya juu.

“Tunaamini kupitia ushirikiano kati ya Serikali, vyuo vikuu, sekta na wadau wa maendeleo, tunaweza kuwawezesha wanafunzi kwa ajili ya maendeleo ya baadaye,” amesema Kachingwe.

Related Posts