BAADA ya Simba Queens kumtambulisha golikipa, Wilfrida Seda kutoka Get Program, timu hiyo imemvuta tena straika Janet Mpeni kutoka timu hiyo.
Kama usajili huo utakamilika, Simba Queens hadi sasa itakuwa imefikisha nyota watatu, Seda, Mpeni na Zawadi Khamis kutoka Fountain Gate Princess ambaye hajatambulishwa kikosini hapo.
Nyota huyo kwa sasa yuko kwenye majukumu ya timu ya taifa chini ya miaka 17 inayojiandaa na mashindano ya wasichana ya Integrated Football Tournament (GIFT) yatakayofanyika Dar es Salaam kuanzia Januari 7-18.
Mtu wa karibu wa mchezaji huyo aliliambia Mwanaspoti, kinda huyo alimalizana na Simba muda mrefu kabla ya kujiunga na kambi ya timu ya taifa.
“Ni kweli kila kitu kimemalizika amesaini mkataba wa mwaka mmoja kinachosubiriwa ni utambulisho tu hata hivyo kwa sasa yuko kambini na timu ya taifa, atarejea klabuni Januari 19,” alisema.
Mshambuliaji huyo alihusishwa kuhitajika na timu mbalimbali katika dirisha hili ikiwamo JKT kabla ya Simba kuelezwa ndio imefanikisha dili hilo.
Inaelezwa Simba ilimuhitaji straika huyo kuja kuziba pengo la Aisha Mnunka ambaye hadi sasa hajaripoti kambini na huenda asiendelee na mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Wanawake.