Simba yatanguliza mguu mmoja robo fainali

BAO pekee lililofungwa na kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ahoua limeipa Simba ushindi wa kwanza ugenini msimu huu katika mechi za Kombe la Shirikisho Afrika  baada ya kuichapa CS Sfaxien ya Tunisia na kutanguliza mguu mmoja kufuzu robo fainali.

Ushindi huo wa kihistoria kwa Simba katika ardhi ya Afrika Kaskazini ulipatikana usiku huu kwenye Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi, jijini Tunis na kuifanya ifikishe pointi tisa baada ya kucheza mechi nne za Kundi A.

Ahoua alifunga bao hilo kiufundi dakika ya 34 baada ya kupokea pasi ya Leonel Ateba kisha kutuliza kifuani akiwa ndani ya 18 na kufumua shuti kali lililomshinda kipa Aymen Dahmen.

Hilo ni bao la pili kwa Ahoua kwani alifunga pia katika mechi ya kwanza ya kundi hilo dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola, mbali na asisti alizonazo akiwa ndiye kinara wa klabu.

Licha ya ushindi huo muhimu ikiwa Tunisia ikifuata nyayo za watani wao wa jadi, Yanga iliyoishinda Club Africain pia ya nchini humo katika mchezo wa play-off ya michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2022 na kutinga makundi hadi kufika fainali ikilikosa taji kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2.Yanga ililala nyumbani katika mechi ya awali ya fainali kwa mabai 2-1 kisha kushinda ugenini kwa bao 1-0.

Katika mchezo huo wa leo, kocha wa Simba, Fadlu Davids alimuanzisha Ellie Mpanzu kwa mara ya kwanza kwa mechi za Caf tangu aliposajiliwa kupitia dirisha dogo la usajili na kumtumia kwa dakika 77 kabla ya kumtoa ili kumpisha Debora Mavambo.

Simba itajilaumu kwa kushindwa kutoka na ushindi mnono mbele ya Sfaxien inayoburuza kundi hilo, ikowa haina pointi hata moja kutokana na kupoteza mechi zote nne ilizocheza na kujiondoa katika mbio za kutaka kutinga robo fainali.

Simba ilitengeneza nafasi nyingi katika kila kipindi kulinganisha na wenyeji waliocheza nyumbani bila mashabili baada ya kuadhibiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutokana na fujo walizofanya mashabiki katika mechi dhidi ya vinara wa kundi hilo, CS Constantine ambayo ipo uwanjani muda huu kuumana na Bravos.

Simba sasa inajitaji ushindi mmoja katila mechi mbili ilizonazo dhidi ya Bravos wikiendi ijayo ugenini au ile ya nyumbani dhidi ya Constantine itakayopigwa Januari 19 Kwa Mkapa.

Related Posts