Simulizi hukumu kesi ya Sanga wa Chadema na wenzake- 1

Njombe. Haki imetendeka. Hii ndio kauli inayosikika vinywani mwa makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya wenzao, George Sanga na wenzake wawili, kuachiwa huru kwa tuhuma za mauaji.

Hii ni baada ya kukaa mahabusu siku 1,557 tangu walipokamatwa Septemba 26, 2020 kwa tuhuma za mauaji ya kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Emmanuel Mlelwa hadi walipoachiwa Desemba 31, 2024.

Mbali na George Menson maarufu Sanga, makada wengine walioachiwa huru ni Goodluck Oygen maarufu Mfuse aliyekuwa mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo na Optatus Elias Nkwera aliyekuwa mshtakiwa wa tatu.

Lakini swali ambalo wengi wamekuwa wakijiuliza, ni sababu zipi za kisheria zilizoishawishi mahakama chini ya Jaji Dunstan Ndunguru wa Mahakama Kuu kanda ya Njombe, kuwaona hawana hatia na kuwaachia huru?

Mlelwa alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kwa vyuo vikuu mkoa wa Njombe, alikutwa ameuawa Septemba 19, 2020 eneo la Kibera Estate katika Wilaya ya Njombe karibu na daraja la Mtege.

Taarifa ya daktari ya uchunguzi wa mwili wake, ilibaini sababu za kifo ilitokana na kuvunjika uti wa mgongo na kushindwa kupumua kutokana na kupooza kwa mishipa muhimu ya upumuaji (diaphragm) na kuvunjika mifupa ya shingo.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi 14 wa upande wa Jamhuri na vielelezo na mashahidi watano wa utetezi, Jaji Ndunguru alisema upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.

Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na wakili wa Serikali mkuu, Cecilia Mnongo akisaidiana na mawakili Genes Tesha, Tito Mwakalinga na Elise James, huku washtakiwa wakitetewa na mawakili Innocent Kibadu, Frank Ngafumika na Dickson Matata.

Jaji alisema mashahidi wawili muhimu wa Jamhuri ambao walidai kumsikia mshtakiwa wa kwanza akikiri kwa mdomo kushiriki mauaji hayo, akiwemo Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) wa Njombe kutoitwa kutoa ushahidi.

Pia kulikuwa na dosari za kisheria na hoja za kiushahidi katika uchukuaji wa sampuli za damu kwa ajili ya upimaji wa vinasaba (DNA) katika fulana ambayo ni sare ya Chadema na kitambaa cha kujifutia jasho.

Maelezo ya Jamhuri kwa ujumla wake, ulieleza siku ya tukio saa 5:00 usiku, Mlelwa alikuwa na mtu aliyetajwa ni Thadei Mwanyika, wakiwa na mazungumzo katika baa ya Tale iliyopo wilayani Njombe.

Baada ya kumaliza mazungumzo yao, waliondoka eneo hilo pamoja na wakiwa njiani wakitembea kwa miguu, walitekwa nyara na washtakiwa na kuingizwa kwa nguvu kwenye gari aina ya Toyota Gaia yenye namba T457 DAB.

Baada ya kuingizwa katika gari hilo, ilidaiwa na Jamhuri kuwa walianza kuteswa na washtakiwa wakiulizwa ni kwa nini wanapanga njama mbaya za kununua wagombea udiwani wa Chadema katika Uchaguzi Mkuu 2020.

Gari hiyo iliendeshwa kutoka katika eneo hilo, huku washtakiwa wakidaiwa kuendelea kuwatesa na baadaye washtakiwa walidaiwa kumnyonga Mlelwa hadi kufa na mwili wake kuutupa kwenye daraja la mto Mtege.

Baada ya kumaliza kazi hiyo, washtakiwa walidaiwa kuondoka wakiwa na Thadey Mwanyika na Septemba 21, 2020 mwili wa marehemu ulipatikana unaelea katika maji ambapo polisi waliuopoa.

Shahidi wa kwanza, Lufingo Mtweve ndiye aliyekuwa wa kwanza kuuona mwili wa marehemu wakati anapita katika daraja la Mtege, huku shahidi wa pili, Robert Kinyamagoha ambaye ni daktari aliyeleza kiini cha kifo cha marehemu.

Shahidi wa tatu, Polycarp Mlelwa ambaye ni ndugu na marehemu, alieleza namna alivyoitwa na polisi kuutambua mwili wa ndugu yake kabla ya uchunguzi (postmorterm) wa mwili huo kuanza.

Kwa upande wake, shahidi wa nne, Koplo Mrisho mwenye namba G.9783 alieleza namna Septemba 26, 2020 akiwa katika majukumu yake, alimuona RCO Njombe akimpigia simu Thadey Mwanyika na kumtaka afike ofisini kwake.

Shahidi huyo alidai Thadey alikutana na RCO mbele yake na alimuuliza ratiba yake ya siku ya tukio, alijieleza kuwa alikuwa katika majukumu yake ya kila siku eneo la Utalingolo na saa 10:00 alasiri alihudhuria mkutano wa Chadema.

Baadaye aliondoka eneo hilo na kwenda kwa kaka yake ambako alilala huko na hapo ndipo RCO aliamuru Thadey akapekuliwe nyumbani alipokuwa amelala, lakini akawapeleka maeneo tofauti na ndugu wakamkana kulala huko.

Wakiwa ofisini, Thadey alimwambia alikuwa amefikia nyumbani kwa Sanga, lakini hakwenda kulala huko kwa kuwa kilikuwa ni kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani 2020.

Siku hiyo hiyo saa 12:00 jioni, akiwa kituo cha polisi, walifika kituoni Rose Mayemba, George Sanga (mshtakiwa wa kwanza) na Emmanuel Masonga ambapo RCO aliagiza wawekwe mahabusu na kunyang’anywa simu.

Akaeleza katika ushahidi wake huo kuwa George Sanga alipelekwa ofisini kwa RCO na RCO alimhoji kuhusiana na kifo cha Mlelwa ambapo kada huyo wa Chadema alikana kuhusika kwa namna yoyote ile.

Hapo ndipo Thadey aliletwa mbele ya Sanga na kuelezea nini kilitokea na kwamba Mlelwa alikuwa akimsumbua akimtaka ajitoe kugombea udiwani katika kata ya Utalingolo kwa tiketi ya Chadema na ajiunge CCM.

Kulingana na shahidi huyo, alitoa taarifa kwa viongozi wa Chadema akiwamo mshtakiwa wa kwanza na baada ya kutoa taarifa, walimtaka aendelee kumfutilia Mlelwa (marehemu), na alimfuatilia na kuwaambia yuko FM Hotel.

Shahidi huyo alidai Thadey alipewa maagizo amwelekeze Mlelwa afike eneo la kuosha magari ambalo liko nyuma ya hoteli hiyo na walisimama hapo ambapo ilikuja gari na kuwachukua na walianza kupigwa hadi umauti ukamkuta.

Kulingana na shahidi huyo, baada ya mshtakiwa wa kwanza kusikiliza simulizi ya Thadey, anadaiwa kusema “Ni kweli tumefanya” na baada ya kukiri aliwataja Ashery Machela, Nkwera na XB.

Shahidi huyo akadai Septemba 27, 2020 saa 11:00 jioni baada ya Optus kukamatwa, alihojiwa na RCO mbele yake na kudai katika mahojiano hayo alikiri kuhusika na kuhojiwa XB ni nani akajibu ni mshtakiwa wa pili.

Baada ya mahojiano hayo, yeye na Koplo Haruna na Inspekta Mapuga walienda kumkamata mshtakiwa huyo wa pili na kumkabidhi kituoni kwa hatua nyingine za kiupelelezi kwa mujibu wa taratibu za Jeshi la Polisi.

Shahidi wa tano, Charles Bugoya ambaye ni mkemia kutoka ofisi ya mkemia mkuu wa Serikali katika idara ya DNA, alieleza namna alivyochunguza sampuli za fulana ya Chadema na kitambaa cha kufutia jasho.

Sampuli hizo zilikuwa na maandishi “mpanguso wa damu kutoka kwenye mwili wa marehemu Emmanuel Mlelwa” na nyingine ikiandikwa “Mpanguso wa damu kutoka kitambaa alichokuwa nacho Goodluck Mfuse”

Sampuli nyingine ilikuwa imeandikwa “mpanguso wa wa kinywa kutoka kwa George Sanga” na nyingine ikaandikwa “mpanguso wa kinywa kutoka kwa Optatus Nkwera” na nyingine kutoka kwa Mfuse na Sanga.

Shahidi huyo alisema kupitia uchunguzi wa kimaabara, alithibitisha kuwa matone ya damu yaliyokuwa kwenye fulana ambazo ni sare ya Chadema na kitambaa cha kufutia jasho, ilikuwa ni damu halisi kutoka kwa mwanadamu.

Katika uchunguzi wake, alibaini kuwa sampuli ya DNA kutoka katika fulana ile ya Sanga ilishabihiana na sampuli ya DNA kutoka kwenye sampuli ya damu kutoka kwa marehemu ilishabihiana pia na kitambaa cha Goodluck Mfuse.

Baada ya kukamlisha uchunguzi wake huo, aliandaa taarifa ambayo alimkabidhi Koplo Isaya nakala halisi ya taarifa hiyo na Februari 15, 2024, polisi waliwasilisha ombi la kupatiwa nakala ya taarifa hiyo kwa kuwa nakala halisi imepotea.

Related Posts