SMZ yajibu hoja za ACT-Wazalendo kuhusu Kisiwa cha Fungu Mbaraka

Unguja. Wakati ACT- Wazalendo ikidai kuwa, Kisiwa cha Fungu Mbaraka kipo katika mchakato wa kutolewa leseni kwenye vitalu vipya vitano na Serikali ya Tanzania Bara kinyume na utaratibu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema hakuna eneo lolote lililopo Zanzibar litakalotangazwa na mamlaka tofauti.

Katika taarifa iliyotolewa na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman kuhusu hoja hiyo leo Jumapili Janauri 5, 2025, amesema taarifa hiyo ni ya upotoshaji.

Awali, msemaji wa kisekta wa ACT- Wazalendo, Said Ali Mbarouk aliitaka SMZ kuwaeleza wananchi kuhusu masuala ya uchimbaji na utafutaji wa mafuta na gesi akisema kugawa leseni katika kisiwa hicho ni kuingilia mipaka.

Hata hivyo, Waziri amesema:  “Ni kweli Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia taasisi zake ina mpango wa kutoa vitalu vya uwekezaji wa mafuta na gesi asilia katika duru ya tano ya utoaji wa vitalu vya mafuta na gesi asilia kwa Tanzania Bara.”

“Hata hivyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inapenda kuwaeleza wananchi kuwa, hakuna eneo lolote la Zanzibar litakalotangazwa katika duru hiyo kinyume na taarifa zinazosambaa,” amesema Shaaban.

Amesema Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 ambayo imeunda taasisi za Tanzania Bara imeweka wazi mipaka ya taasisi hizo na eneo la Zanzibar halishughulikiwi na taasisi hizo. 

Kuhusu madai ya kushindwa kuendeleza eneo la kisiwa hicho, Waziri amesema uendelezaji wa maeneo unategemea na soko la dunia na kanuni bora za uendelezaji wa maeneo husika. 

Amesema Serikali zote duniani huendeleza maeneo kwa awamu na hadi sasa, SMZ imeshatenga vitalu 10 kwa lengo la uwekezaji. 

“Eneo la Fungu Mbaraka na baadhi ya maeneo ya bahari kuu ambayo bado hayajaendelezwa yataendelezwa baada ya kufanyiwa uhakiki wa kina, kama ilivyofanywa kwa maeneo mengine na hali ya soko la dunia itaporuhusu kutangazwa kwa maeneo mapya,” amesema Shaaban.

Kuhusu kuonekana maeneo ya Zanzibar katika ramani ya marejeo ya Tanzania Bara ya mwaka 2024, Waziri amesema kwa kawaida ramani za marejeo za nchi yoyote huwa zinachorwa na taasisi husika zikiwa zinajumuisha maeneo mengine ya jirani ambayo taasisi haina mamlaka nayo.

“Ushahidi wa suala hilo umo katika ramani yenyewe ya mwaka 2024 ambayo mbali ya kuonyesha eneo lote la Tanzania, ramani hiyo pia imeonyesha maeneo ya nchi za jirani ikiwamo Rwanda, Burundi na maeneo makubwa ya Kenya, Somalia, Uganda, Zambia, Malawi, Jamhuri ya Demokrasi ya Congo (DRC) na Msumbiji,” amesema Shaaban.

Amesema hata ramani rejea ya Zanzibar ya mwaka 2024 inaonyesha maeneo ya Zanzibar, Tanzania Bara na Kenya.  

Awali,  ACT-Wazalendo iliitaka Serikali kuweka wazi mipaka ya kitaalamu baina ya vitalu vya Zanzibar vilivyotangazwa na vile vya Tanzania Bara vinavyotarajiwa kutangazwa Machi mwaka huu katika duru ya tano. 

“Kuna taarifa za kuturejesha tulipotoka, Serikali itoke hadharani iseme kuhusu jambo hili maana kufanya hivyo ni kuingilia mipaka,” alisema Mbarouk. 

Related Posts