Dar es Salaam. Ikiwa imebaki miezi takribani tisa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye ametaja mambo matano yanayoweza kuchangia kuvuruga amani katika uchaguzi huo.
Akizungumza na Mwananchi mwishoni mwa wiki iliyopita kujua anachokiona kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2025, Sumaye amesema mambo hayo yana histori ya kuchafua amani kwenye chaguzi nyingi za Afrika, huku akisisitiza Tanzania kuyaepuka kama uonevu baina ya mgombea na mgombea au chama na chama.
Kauli ya Sumaye aliyewahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imekuja ukiwa umepita mwezi mmoja tangu Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba kuonya kile kilichotokea katika uchaguzi Serikali za mitaa 2024.
Baada ya uchaguzi huo wa mitaa, Jaji Warioba aliyepata kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alibainisha kasoro zilizojitokeza na kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua.
Jaji Warioba akizungumza na wahariri na waandishi wa habari Desemba 4, 2024 alitaka Chama cha Mapinduzi (CCM) na vyama vya upinzani kuweka masilahi yao pembeni na kujadili changamoto zilizojitokeza.
Miongoni mwa malalamiko kuhusu uchaguzi huo ni wagombea wa upinzani kuenguliwa na baadhi ya makada wa vyama hivyo na wa CCM kudaiwa kuuawa na wengine kujeruhiwa.
Jaji Warioba alizungumzia uchaguzi huo, akigusia na wa mwaka 2025 akieleza anachokiona mbele iwapo hatua hazitachukuliwa kwa pande zote hasa kukubaliana jinsi ya kuendesha uchaguzi.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, licha ya changamoto hizo zilizoibuka katika uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2019, bado zimejirudia akionya zisiposhughulikiwa ipasavyo zinaweza kuleta machafuko ya kisiasa kama yaliyotokea mwaka 2000 Zanzibar.
Akizungumza na Mwananchi Sumaye aliyewahi kuwa Waziri Mkuu (1995-2005) enzi za utawala wa Benjamin Mkapa, amesema uchaguzi kutofanyika vizuri kunachochewa na mambo matano, aliyotaja ni uonevu baina ya mgombea na mgombea au chama na chama.
“Unapotokea uonevu baina ya chama kimoja dhidi ya chama kingine ni mbaya zaidi na huu ndiyo unaoleta vurugu,” amesema Sumaye akitolea mfano baadhi ya chaguzi za Afrika.
“Mfano ni jirani zetu wa Kaskazini (Kenya) na wale wa Kusini (Msumbiji), tunaona kilichowatokea, lakini chanzo cha yote ni manung’uniko yaliyoanzia wakati wa uchaguzi, baadaye yakaendelea hadi pale walipofikia, mzizi wa fitina wa migogoro yao ulianzia wakati wa uchaguzi,” amesema.
Mambo mengine ni wananchi kutompata mtu wanayemtaka, kukosekana kwa haki, uwazi sambamba na polisi kuwa na upande.
Katika hilo la polisi, hata Jaji Warioba aliyewahi kuwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania aliwahi kugusia tatizo hilo akionya vyombo vya ulinzi kuhusishwa na siasa, akidai kwa sasa Jeshi la Polisi limeingizwa kwenye siasa.
“Katika miaka michache iliyopita tumeliingiza Jeshi la Polisi kwenye siasa, linatoa matamko ya kisiasa na hii italeta mgawanyiko. Wananchi watagawanyika. Kuna wale watakaoona, Jeshi la Polisi ni adui, tusifike huko. Tuliache Jeshi la Polisi lifanye kazi zake za kawaida,” amesema.
‘Tanzania ina historia’
Katika mazungumzo yake na Mwananchi, Sumaye amesema Tanzania ni nchi ambayo ina histori ya amani kwenye chaguzi nyingi, akisisitiza amani hiyo kuendelezwa kwenye uchaguzi ujao unaotarajiwa kufanyika baadae Oktoba.
Amesema, wananchi wanapoona wameletewa mtu ambaye wao hawakumchagua na si yule waliyeamini ndiye atawafaa katika kuwaongoza, hali hiyo husababisha vurugu na uchaguzi kuchafuka.
“Ili uchaguzi ujao uwe mzuri na mambo yawe shwari inatakiwa hilo pia lizingatiwe, kila kitu kifanyike kwa haki na kuwepo kwa uwazi, haya yakifanyika nchi itatulia na yule atakayeshinda atakuwa ni chaguo la watu.
“Lakini ikitokea wanaosimamia uchaguzi, wasitoe haki au wale wanaoshindana mmoja wao kuhonga au kuiba kura, hizo ni mbinu chafu katika uchaguzi na zinapoteza haki na kusababisha manung’uniko na fujo,” amesema.
Sumaye amesisitiza Tanzania ni nchi ya amani na kila Mtanzania anapenda amani, hivyo nchi inapokwenda kwenye uchaguzi, isijekuonekana imeshindwa kusimamia misingi ya amani.
“Ninachokitamani ni Tume (Tume Huru ya Uchaguzi) isimamie uchaguzi kwa haki kama ambavyo taratibu za tume na sheria vinataka, isimamie bila kupinda pinda wala kupendelea,” amesema Sumaye ambaye mwaka 2015 alijiunga na Chadema kisha Februari 2020 akarudi CCM.
Jambo jingine alilolitaja waziri huyo mstaafu ni polisi kulinda amani kwa kila mtu bila kuonyesha kuwa na upendeleo upande fulani na mwingine kuonewa.
“Polisi nao wasimame kulinda amani kwa mtu yeyote, isionekanae upande fulani unaonewa na mwingine unapendelewa, kama wakisimamia haki na uwazi hakutakuwa na manung’uniko na atakayechaguliwa ndiyo atakuwa chaguo la Watanzania,” amesema.
Katika mchakato wa uchaguzi, kinachoendelea sasa kwa mujibu wa tume, ni shughuli ya uandikishaji ambayo awamu ya kwanza itafikia tamati Machi na awamu ya pili itakuwa Mei.
Tarehe ya uchaguzi itatangazwa Bunge litakapovunjwa baadaye mwaka huu, huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa kufanyika Oktoba kumchagua Rais, wabunge na madiwani.
Walichokisema wachambuzi
Wakiuzungumzia uchaguzi huo wa Rais, wabunge na madiwani 2025, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wamekoleza kauli ya Sumaye wakitaka haki na uwazi vitawale ili uwe uchaguzi huru.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie amesema kinachohitajika kwenye uchaguzi huo ni ushindani wa kweli utakaokolezwa na haki na uwazi.
Amesema, changuzi nyingi zilizopita ushindani ulikuwa ni wa ndani ya chama kupata wagombea wake na si baina ya vyama vya siasa.
“Mfano labda CCM, wenyewe kwa wenyewe kupata wagombea kunakuwa na ushindani mkubwa wa ndani, wakishapatikana wagombea wake ni kama uchaguzi unakuwa umeisha, huku baina ya vyama uchaguzi unakuwa wa upande mmoja jambo linaloondoa haki na usawa,” amesema Dk Loisulie.
Amesema hali hiyo, haipaswi kujitokeza katika uchaguzi ujao kwa kuwa husababisha mtu akishapita kwenye chama kutohangaika kwa kuwa anajiona kana kwamba kishamaliza uchaguzi, jambo ambalo si sawa.
“Hata uchaguzi wa juzi juzi (2024 wa Serikali za mitaa) ushindani haukuwepo, jambo lililosababisha demokrasia kukosa maana,” amesema.
Mchambuzi mwingine, Profesa Mohammed Makame amesema kwa uzoefu wa chaguzi kadhaa zilizopita huwa kuna viashiria vya wanasiasa kuzigeuza kama ni mali yao na kwamba chaguzi hizo zinawahusu wao wenyewe.
“Tunaelewa uchaguzi unahusisha vyama vya siasa na wananchi, bila kujali ana chama au la, anapaswa kushiriki hata hivyo huwa kuna mazingira ambayo wananchi wa kawaida wanakosa nafasi ya kutumia haki hiyo kutokana na joto linalotengezwa na wanasiasa,” amesema Profesa Makame.
Amesema mwaka huu ni vyema ukafanyika kwa haki, amani na uhuru na vyama vya siasa au wanasiasa kutotengeneza presha zisizo za lazima.
“Uchaguzi uliopita tulisikia malalamiko ambayo yalitoka kwa vyama vya siasa au wanasiasa, tunapokwenda kwenye uchaguzi mkuu ni vyema falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya 4R ikawa ni ya wananchi.
“Tukienda nayo kwenye uchaguzi mkuu bila kujali itikadi huku kukitengenezwa mazingira ya kila mmoja kuwa sehemu ya uchaguzi, Taifa libaki na utaifa wake na siasa zibaki kama siasa katika harakati za uchaguzi,” amesema Profesa Makame.