Uchaguzi Chadema: Ni vita ya wakubwa

Mwanza/Dar. Wakati dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu kuwania uongozi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) likifungwa, mchuano unasubiriwa baina ya Freeman Mbowe na Tundu Lissu na ule wa Ezekiel Wenje na John Heche kwa nafasi ya makamu mwenyekiti-Bara.

Miamba hao wa siasa ndani ya chama hicho, watamaliza ubishi wa nani zaidi Januari 21, 2025 katika mkutano mkuu wa uchaguzi utakaofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Mbowe anayetetea nafasi, anachuana vikali na Lissu aliyekuwa makamu wake-Bara, huku Heche akikoleza ushindani kwa kugombea nafasi ya makamu akimuunga mkono Lissu. Wenje anawania umakamu upande wa Mbowe.

Toauti na Wenje ambaye amekuwa akimrushia maneno Lissu ambaye naye hujibu tuhuma, Heche amekuwa tofauti wakati akitangaza uamuzi wa kuwania nafasi hiyo kwa kumpongeza Mbowe jinsi alivyokifikisha chama hapo kilipo.

Heche kwa maelezo yake amesema mwenyekiti huyo amewasaidia watu wengi, akiwemo yeye kufika alipo na kamwe hawezi kumsema vibaya, lakini ni wakati sasa wa kumpisha Lissu aendeleze jahazi.

Alichokisema Heche cha kutomsema Mbowe vibaya, ni sawia na alichokisema Mbowe hivi karibuni kwamba hulka yake ya uongozi si ya kumsema kiongozi wake hadharani.

Hatua hiyo ya Heche aliyewahi kuwa mbunge wa Tarime Vijijini kumuunga mkono Lissu, huku Mbowe akiwa na Wenje inakwenda kushuhudia uchaguzi wa ndani wa Chadema ambao haujawahi kushuhudiwa tangu kuanzishwa kwake.

Makada wengine wanaowania uenyekiti ni Romanus Mapunda na Charles Odero. Nafasi ya Makamu-Bara, yumo Francis Garatwa, aliyewahi kuwa diwani.

Kwa upande wa Zanzibar, wanaowania nafasi ya makamu mwenyekiti wako zaidi ya wanne, akiwemo Said Issa Mohamed anayetetea nafasi hiyo.

Mchuano huo hautaishia tu kwa nafasi ya uenyekiti na makamu, bali unatizamiwa kujitokeza pia kwenye mabaraza ya chama ya vijana (Bavicha), wazee (Bazecha), wanawake (Bawacha) pamoja na ujumbe wa kamati kuu.

Kwenye mabaraza na ujumbe wa kamati kuu, ukiacha Bavicha, wanasiasa mahiri waliowahi kuhudumu nafasi mbalimbali kama ubunge na makao makuu wamejitosa kuwania ama uenyekiti, makamu, katibu mkuu na naibu katibu mkuu.

Aidha, kwenye ujumbe wa kamati kuu ambapo ni nafasi tano za Tanzania bara, lakini waliojitosa kuwania ni 24, wakiwemo wanaotetea nafasi hiyo.

Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar, Salum Mwalimu amesema leo Jumapili ameongoza kikao cha sekretarieti kufanya uchambuzi wa fomu na kupitia kama ziko sawa baada ya dirisha kufungwa na wagombea zaidi ya 40 wamejitosa kuwania nafasi mbalimbali.

Amesema kesho Jumatatu kitafanyika kikao cha sekretarieti maalumu kupitia majina ya waombaji na kutengeneza mapendekezo ya kamati maalumu ya Zanzibar kwenda kamati kuu kwa ajili ya uteuzi wa mwisho.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema kwa sasa wanakusanya taarifa kutoka maeneo mbalimbali, kisha mchakato wa kupitia fomu kwa ngazi za mabaraza utaendelea na hatua za uteuzi zitakafuata.

Akizungumza mbele ya wanachama, wajumbe wa Chadema na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Jumapili, Heche amesema chama hicho kinahitaji watu waadilifu ili watimize malengo ya kuanzishwa kwake.

“Leo tuna watu wachache kwenye chama ambao wamepotoka, wameshindwa kutambua kwa nini chama hiki kilianzishwa.

“Na leo nasema rasmi kwamba mwenyekiti, Freeman Mbowe namheshimu sana, ni kweli amenilea kisiasa ila kwenye uchaguzi huu tutamshinda. Namuunga mkono Tundu Lissu na nimeamua kuchukua fomu baada ya kutafakari,” amesema Heche. 

“Nimekaa kimya muda mrefu, kutafakari mwenendo wa nchi na sababu ya kuundwa kwa chama hiki ndio maana nimeamua kugombea nafasi hiyo.

“Hii taasisi ni tegemeo kwa Watanzania…mimi John Heche nina uzoefu, nina uwezo, nina nguvu, nina maarifa ya kuwa makamu mwenyekiti wa hiki chama wa taifa…tuunde sekretarieti mpya ya chama chetu, tuunde na tuhuishe majimbo, tusimamie usajili wa chama na twende kwenye slogani inayosema ‘no reform no election,” na tutakavyosema hivyo hatutosema kwa maneno tu, bali kwa  vitendo na Watanzania watatuunga mkono.”

 “Kwa sababu tukiruhusu katika nchi hii viongozi wasitokane na kura za watu viongozi hawatowaheshimu watu …silaha pekee inayomsababisha mbunge akae jimboni apigane kwa ajili yako ni kama kura yako inaweza kumuweka na kumuondoa madarakani,” amesema Heche.

Akiendelea kumzungumzia Mbowe, Heche amesema:“Kama kuna mtu alikuja hapa anajua nitamshambulia mtu siwezi kufanya hivyo. Bado mwenyekiti wetu (Freeman Mbowe) atabaki kuwa mjumbe wa kamati kuu. Tumefika hapa tulipo kwa sababu yake. Kujenga mtandao wa chama kama hiki ni kazi kubwa. Ndio maana mimi namuheshimu sana Freeman.”

Amesema anaamini Lissu na yeye wakishinda chama hicho kitatimiza malengo ya kushika dola na kubadilisha maisha ya watu, akisisitiza wanahitaji mabadiliko ndani ya chama.

Amesema kwa sasa chama hicho mtu akikemea rushwa anaitwa mropokaji, lakini akishinda yeye na Lissu wataweka hadharani wala na wapokeaji rushwa kwa majina yao bila aibu, kama ambavyo wanawataja wala rushwa wengine nje ya Chadema.

“Chadema kilijijenga kwa kushambulia mafisadi. Ukila rushwa ndani ya chama tutakusema na tutakutaja jina kuwa wewe ni mla rushwa. Lissu ni mkweli na mwadilifu,” amesema.

Heche amesema: “Tunaweza kutofautiana mimi na yeye (Lissu) vitu vidogovidogo, ni wakati gani wa kusema, lakini Lissu ni mwadilifu, mkweli na msafi na huyo ndiyo anastahili kuwa kiongozi wetu kwa sasa.”

Heche amesisitiza ataibuka kidedea kwenye uchaguzi huo na hata akishindwa hatohama Chadema na endapo atashinda atafanya kazi na yeyote atakayeshinda kati ya Mbowe na Lissu.

Katika maelezo yake, Heche amesema Lissu atapata, “ushindi wa kimbunga” kwani dalili zote zinajionyesha.

Aidha, ametumia fursa hiyo kuonya makundi ya vijana kuacha kuwashambulia viongozi wao: “Naomba vijana wa chama wanaotukana viongozi wetu waache. Wanamshambulia na kumtukana Freeman Mbowe waache, mtu anakaa anamtukana Tundu Lissu, hebu tuache.”

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho mkoani Shinyanga, Erasti Kazinja amesema endapo Mbowe atashinda kwa haki watamuunga mkono na kumrekebisha pale wanapoona aliteleza, lakini kwa wakati huu wa siasa kuelekea uchaguzi mkuu wanamuhitaji Lissu na Heche kwa kuwa sio waoga.

Kwa upande wake, Michael Makenzi, Mwenyekiti Chadema Butiama amesema anamuunga mkono Heche kwa sababu ya misimamo yake na uadilifu wake, huku Neema Steven, Mwenyekiti Chadema Jimbo la Geita Vijijini amesema wajumbe wanatakiwa kupeleka dereva atakayeongoza jahazi kufikia nchi ya ahadi.

Mchuano mwingne unatarajiwa kushuhudiwa Bawacha ambapo vigogo watatu wataumana. Kaimu Mwenyekiti wa baraza hilo, Sharifa Suleiman anawania sasa nafasi hiyo akichuana na Spika wa zamani wa Bunge la Wananchi, Celestine Simba na Suzan Kiwanga, aliyewahi kuwa mbunge wa Mlimba.

Bavicha  hakutakuwa na shughuli ndogo. Wakili Deogratius Mahinyila atachuana vikali na aliyekuwa mwenyekiti wa umoja wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam -Chaso, Hamis Mambo. Wote wanataka kumrithi John Pambalu ambaye kwa mujibu wa katiba yao amekosa sifa.

Kwa upande wa Bazecha, nako kuna mvutano ambapo Hashimu Juma Issa anatetea nafasi hiyo akichuana na wengine.

Kamati Kuu wapo makada 24, wanaowania nafasi hizom, akiwemo Daniel Naftari, John Pambalu, Twaha Mwaipaya, Patrick Ole Sosopi na Joseph Mungai ambaye ni mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa.

Related Posts