Udhaifu katika ndoa ni sehemu ya ndoa

Kanada. Kwanza, kila binadamu ana ubora na udhaifu, hata awe mzuri au mbaya kiasi gani. Hivyo, wanandoa wanaposhughulikia ubora au udhaifu wao, wanapaswa kukumbuka kuwa wote ni binadamu wenye mapungufu.

Unaweza kuwa msomi mkubwa tu, tajiri, mwelewa si kawaida, mkarimu hata katili vipi, bado una ubora na udhaifu wako. Hivyo, tukubali na tujue haya yanatuhusu wote. Hivyo, kuwa au kuonyesha udhaifu katika ndoa, sawa na maisha, ni jambo la kawaida.

Kisicho cha kawaida ni namna ya kuukubali, kuurekebisha, au kuupunguza udhaifu huku wahusika wakijitahidi kuujua, kuutumia ubora wao huku wakijitahidi wawezavyo, kuishi na madhaifu yao.

Pili, udhaifu mwingine ima unaweza kuwa ubora au kuchochea ubora, hasa wahusika wanapoamua kuushughulikia. Hata hivyo, tukubaliane. Kuna udhaifu usiokubalika, hasa unapogeuka donda ndugu.

Kwa upande wa ubora, hauna tatizo katika ndoa. Kwani, unaweza kutumika kama kichocheo na nyenzo ya mafanikio ya ndoa.

Tutatoa mifano. Ni wanandoa wangapi wana wenzi wakoromao walalapo? Je, hufanya nini kupambana na kurekebisha udhaifu huu? Ni wangapi wana udhaifu wa kutosikiliza au kuwahukumu wenzao bila kuwasikiliza? Je, udhaifu huu hauna tiba?

Ipo tiba. Kama ukigundua au mkigundua kuwa kuna tatizo hili, kwanza, ni kuliweka wazi kwa lugha na namna nzuri inayojenga na siyo kubomoa. Badala ya kuitana wabishi na wasiojali, elezaneni hisia zenu kwa ukweli na uwazi kuhusiana na tatizo hili.

Kama mmojawapo ana tatizo la kutosikiliza, anapaswa kujifunza namna ya kumsikiliza mwenzake.Kila mnapoongea au kusemezana, mwishoni, ulizaneni kama mmesikilizana na kuelewana. Maana, kuna kusikiliza ilimradi kumridhisha mwenzako wakati ukweli ni kwamba unajua unafanya hivyo kumridhisha wala si kumsikiliza.

Kuna kusikiliza bila kuelewa ukutoa michango isiyotegemewa wala kuleta maana. Hivyo, hatua ya kwanza ni kuujua udhaifu. Hatua ya pili ni kuukubali na kuutafutia suluhu. Hatua ya tatu ni kufanya mazoezi ya kutatua tatizo. Na mwisho, ni kutathmiana kwa kuulizana na kutathmiana pasina kuridhishana au kudanganyana. Hili halihitaji shahada.

Kwani, binadamu yeyote amejaliwa uwezo wa kisaikolojia wa kumuelewa, japo wakati mwingine anaweza asimuelewe mwenzake kulingana na namna alivyopokea anachopokea. Hatutazama kwenye saikolojia.

Tumetumia mfano wa kusikiliza na kusikilizana kuwakilisha mifano mingine mingi. Mfano, mnaombana ushauri? Je, huu ushauri mnaufanyia kazi au kuudharau? Je, mnapoombwa au kuomba ushauri, mnaupokea na kuufanyia kazi?

Maswali haya hayawezi kupatikana au hata kufikirika kama mtakiuka hatua ya kwanza ya kukubali ubora na udhaifu wenu. Pili, lazima mjue kuwa mna uwezo na uelewa tofauti wa mambo. Wanandoa wengi wanaharibiwa na kidudu kiitwacho kujihami.

Linapotokea tatizo au kutoelewana, kinga ya kwanza ni kuepuka kujihami. Badala yake, mjitahidi kuelewa tatizo. Kama mna au mmojawapo ana wasiwasi wa kutoeleweka au kueleweka vibaya, amuulize mwenzake kama amemuelewa na amemuelewaje.

Baada ya kuomba maelezo, mhusika awe tayari kusikiliza maelezo, utetezi, au uelewa wa mwenzake. Mruhusu aseme bila kuingilia ili apate fursa ya kujieleza aeleweke nawe umwelewe.

Kama bado kuna kutoelewa/kueleweka au hofu ya kutoeleweka, si vibaya kuuliza upya ili kupata maelezo ya kina ili muweze kuelewa tatizo na kulisuluhisha.

Hapa, kuna ubora au udhaifu kimawasiliano. Katika maisha, mawasiliano ni muhimu na hayaepukiki. Si kila mawasiliano ni mawasiliano.

Hapa tunamaanisha mawasiliano chanya, si hasi. Mfano, mkisikilizana, kuheshimiana, hata kudharauliana, mnakuwa mnawasiliana ingawa matokeo yake yanaweza kukinzana hata kutofautiana.

Kwa vile nafasi haitoshi, tungetaka kumalizia kwa kuwapa nyenzo nyingine. Jengeni lugha maalumu ya mawasiliano. Wanandoa karibu wote wana aina fulani ya lugha, hata mawasiliano ambayo kwa wasiohusika ni vigumu kuielewa.

Kadhalika, hata namna yao ya kuwasiliana ni tofauti na ya pekee kulingana wanawasiliana vizuri au vibaya na kwa muda mrefu. Hakika, kila mtu ana ubora na udhaifu. La muhimu ni kutafuta na kuvijua vitu hivi na kuvifanyia kazi. Tunaishi mara moja.

Related Posts