Ukali wa mzazi unavyoweza kuathiri uhusiano na mtoto

Dar es Salaam. Wanasema samaki mkunje angali mbichi, methali hii inashabihiana na aina ya jamii za Afrika na dunia kwa ujumla, ambapo moja ya majukumu ya mzazi katika familia ni kuhakikisha mtoto anakuwa katika maadili bora na upendo, huku mshikamo ukisimama kama nguzo muhimu katika familia.

Ni dhahiri kuwa baadhi ya tabia za watoto kama vile busara, upendo, uthubutu, kujiamini ni kati ya matokeo chanya ya malezi bora ya wazazi kwa watoto wao.

Hofu, kutojiamini na wasiwasi ni kati ya matokeo hasi ya malezi ya mzazi kwa mtoto, ambapo mara nyingi husababishwa na ukali wa wazazi kwa mtoto.

Mtaalamu wa ndoa na familia kutoka Chicago, Marekani, Dk Jennifer Litner kupitia utafiti wake wa mwaka 2022 ameonesha namna hasira za mzazi zinavyoweza kumsababishia mtoto kupata msongo wa mawazo na tatizo la ubongo.
Utafiti huo ulilenga kuangalia namna hasira za wazazi zinavyoathiri upendo wa watoto na familia kijumla.

Katika utafiti huo, Dk Litner ameeleza kuwa, kukulia kwenye mazingira ya woga na hasira hakusababishi hofu tu, bali huondoa upendo na mshikamano ndani ya familia.

“Hasira za mzazi zinaweza kusababisha unyanyasaji wa kihisia kwa mtoto, ikiwa atasema maneno ya kuumiza basi maneno hayo hayatasahaulika, kwa hasira, mtoto anaweza kudhani ni kosa lake na kuendeleza hisia za kutokuwa na maana au thamani kwenye maisha,” anasema Dk Litner kwenye utafiti huo.

Anasema hasira za wazazi mara nyingi huchochea tabia mbaya, ukaidi au jeuri inaweza kusababisha magonjwa ya kujitenga kwa mtoto, huku chanzo ikiwa ni aina hiyo ya wazazi.

“Ukali huu, ambao mara nyingi unajumuisha matumizi ya adhabu kali, ukosefu wa mawasiliano na kudhibiti kwa nguvu, unapoendelea, husababisha upungufu wa upendo na mshikamano ndani ya familia.

“Wazazi wanaposhindwa kuonyesha upendo na kujali kwa watoto wao, inakuwa vigumu kwa familia kudumisha umoja na ushirikiano, watoto wanaokuzwa katika mazingira ya ukali, wanapata changamoto ya uhusiano wa upendo na huruma”.

Mwananchi kupitia ukurasa wake Instagram iliposti mada iliyohoji “ni jina gani la utani ulilowahi mpatia baba yako kutokana na ukali wake”, baadhi ya waliojibu swali hili walieleza sababu za kutoa majina hayo.

Majina yaliyotajwa na wengi, kwa wao kuwapa wazazi wao, hasa baba ni pamoja Gadafi, Osama, Pilato, mkoloni, Idi Amini, mfarisayo, dingi, mjerumani, kaburu, mzee fokafoka, Adolf Hitler, brigedia na mengine mengi.

Katika majina yote ambayo watoto wamewapa wazazi wao, hasa baba, mengi ni ya wale watu wenye historia ya kuwa tabia mbaya, lakini pia wenye ukatili.
Hii inatafsiri tabia halisi ya wazazi kwenye familia.

Mwanasaikolojia Nyisambi Ndagamsu anasema kuna aina nne za malezi ambayo ni mabavu, kutelekezwa, kudekezwa na malezi ya mwafaka.

Anasema, katika aina hizo za malezi, wengi hulelewa kwenye mfumo wa malezi ya kimabavu (dikteta) ambayo hujenga chuki na kuondoa upendo kati ya mzazi na mtoto na wachache hulelewa malezi ya mwafaka ambayo ndiyo aina sahihi ya malezi kwa mtoto.

“Wazazi wengi wanaona kumlea mtoto kimabavu kwa kumpa sheria ngumu,ukali, kumpiga na kumfanya mtoto kuishi kama yupo utumwani ndiyo namna sahihi ya malezi.

“Malezi kwa watoto ni mchakato wa muda mrefu, na malezi hayo ndiyo huchagua aina ya maisha ya mtoto hapo baadaye,” anasema na kuongeza:

“Kuna baadhi ya watoto huishi kwa amani na furaha pale mzazi anapokuwa nje ya nyumbani, ila huingiwa na huzuni na hofu wazazi wanaporejea nyumbani.”

Anasema malezi hayo si salama, na humwathiri mtoto kisaikolojia kwa kumjengea taswira kuwa yeye ni mkosefu wakati wote na hakuna kilicho kwake.

“Hali hii, humfanya mtoto kuishi kwenye woga na hofu, huku akiamini muda na saa yoyote ataadhibiwa kwa kutukanwa au kupigwa,” anasema.

Aina ya maisha ya mtoto kumkimbia mzazi wake na kunyong’onyea pale anapomuona mzazi si aina sahihi ya malezi.

Anasema hali hiyo huathiri afya ya akili ya mtoto na kisha kumsababishia ugonjwa wa wasiwasi, kukosa kujiamini, kushindwa kujitetea na kuwa, hali hii huendelea kumuathiri hata akiwa mtu mzima hapo baadaye.

“Mtoto huyu aliyeathirika kiakili, madhara yake hujitokeza hata katika ndoa, hali ya kujiamini hupotea na kisha hushindwa kujizungumzia mema na kujitetea katika mabaya, yote haya ni matokeo ya malezi ya kidikteta aliyopitia alipokuwa mtoto,” anasema.

Anasema wazazi wamekuwa na tabia ya kuona mtoto asiyeuliza wala kuhoji na kuchangia chochote kimawazo ndiyo matokeo bora ya malezi yao na kuwa hawajui hali hiyo ni ishara ya woga na hofu aliyojijengea mtoto.

“Wazazi kufikisha ujumbe kwa njia ya ukali mara nyingi inaharibu afya ya akili ya mtoto,” anaeleza.

Madhara mengine ni watoto kupoteza uthubutu wa kuingia kwenye ushindani wa soko la ajira, na ukuaji wa maisha yake ya kila siku.

“Mzazi unapaswa kufahamu kuwa, malezi ya mtoto yanatofautiana kulingana na ukuaji na nafasi ya mtoto katika familia, unapaswa kumwandaa mtoto kwa njia chanya na si hasi, njia bora ya malezi ni kumwandaa mtoto kuwa mama bora, baba bora na kiongozi bora katika jamii, huku nguzo iliyomjenga ikibakia kuwa malezi bora kwenye ngazi ya familia,” anaeleza.

Ndagamsu anasema malezi bora humfunza mtoto kuishi vizuri na watu hata kipindi anapoondokewa na wazazi wake, na kuwa ukali utamjengea kiburi na jeuri na hata kukosa msaada anapokuwa na matatizo.

“Malezi mazuri au mabaya, ukali na urafiki wa mzazi kwa mtoto mara nyingi hutachagua aina ya maisha ya mtoto hapo baadaye.

Aina nyingine za malezi yanayoweza kumuathiri mtoto kwenye ukuaji na maisha yake ya baadaye ni malezi ya kudekezwa.

“Mtoto anayekua kwa kulelewa kama yai mara nyingi hukosa ujasiri wa ushindani katika maisha, hushindwa kujisimamia katika shughuli zake za kila siku, mara nyingi watoto hawa wanapokosa wazazi, maisha yao huwa magumu na hushindwa kuishi na watu,” anaeleza.

Mwanasaikolojia huyo anabainisha kuwa watoto wa aina hii, hujiona wako kwenye mateso anapokosa yale malezi aliyoyazoea.

Aina nyingine ni malezi ya kutelekezwa, baadhi ya wazazi huwapa watoto kile anachostahili akiamini ndiyo namna sahihi, huku malezi wakiwaachia wafanyakazi na walimu.

“Wazazi wengi huamini malezi ni kumpeleka mtoto shule nzuri na kumtimizia mahitaji yake kwa wakati, huku wakisahau kuwapa muda wa kukaa nao na kuongea machache na kisha kutengeneza urafiki baina yao.

Anasema hali hiyo, husababisha mtoto kukosa uhuru wa kumshirikisha mzazi kwenye magumu anayopitia, hata kukumbwa na madhara makubwa zaidi pindi anapotunza siri hiyo bila kumwambia mzazi.

Mtindo mwingine wa malezi ni malezi ya mwafaka, mtindo huu ni sahihi kwa mtoto na mzazi kuishi kwa Amani na upendo bila kutumia ubabe, kipigo wala kumkaripia.

“Mtoto anayelelewa kwenye aina hii ya malezi mara nyingi huwa na uthubutu wa kujipambania katika hali zote za maisha,” anaeleza.

Ndagamsu anasema, kwenye baadhi ya familia suala la malezi, wazazi wengi, hasa wa kiume hulea watoto bila malengo, huku namna sahihi kwao ni vile walivyolelewa wao wakiwa watoto.

“Mtoto anapaswa kulelewa bila kuharibiwa saikolojia wala kuharibiwa afya ya akili, watoto waliolelewa kwa namna isiyo sahihi, mara nyingi hukumbwa na msongo baada ya tukio (trauma) ambapo hali hiyo huwaathiri siku zote za maisha yao kila wanapokumbuka matukio ya nyuma,” anaeleza.

Mwanasaikolojia Jacob Kilimba anasema malezi ya ukali kwa mtoto si salama na kuwa hupoteza uaminifu kwa mtoto.

“Kwenye ukuaji wa mtoto umri wa miaka 0-2 ni muda wa mtoto kutengeneza watu anaowaamini, mtoto anapokutana na mzazi mwenye hasira na ukali kwa kipindi hiki, huanza kuwaamini watu baki kuliko wazazi wake,” anaeleza.

Kilimba anasema, wazazi wengi wamejijengea imani kuwa, kumgombeza mtoto na kuwa mkali na mwenye hasira muda wote ndiyo malezi bora.

“Malezi unayompa mwanao sasa, ndiyo huchagua maisha ya baadaye ya mtoto huyo, katika maisha, watoto wanaokosa upendo wa wazazi na kuambulia ukali na hasira mara nyingi huwa na tabia ya uwongo mpaka ukubwani,” anasema.

Anasema, mtoto anapogundua kuwa mzazi wake anaridhishwa na kitu gani, ili asigombezwe mara nyingi hutengeneza uwongo wakati wote ili kumridhisha mzazi wake.

Mwanasaikolojia huyo anasema umri wa miaka 0-11 ni umri wa mzazi kumlea mtoto kwa upendo na maadili.

“Mtoto anapofikisha miaka 12 ni umri wa yeye kujilea mwenyewe, huku akitumia ile misingi ya malezi ya miaka 0-11, na pia, wakati huu ndio wakati wa mzazi kuona matunda ya malezi yake kwa mtoto,” anaeleza.

Anasema watoto waliowahi kukumbana na malezi ya ukali na hasira wakati wote, ni watu wasio na moyo wa kusamehe katika maisha yao ya ukubwani.

“Mtoto aliyelelewa bila upendo mara nyingi huwa ni watu wasiosamehe, iwe mwanamke au mwanamume, ila kwa wanawake mara nyingi, hushindwa kujitetea hata katika manyanyaso ndani ya ndoa na popote pale, wao huona kila anachofanyiwa amehurumiwa na si haki yake, hii yote ni kutokana na kushindwa kujiamini kutokana na malezi kipindi cha utoto,” anaeleza.

Kadhalika Kilimba anasema ikiwa mzazi mmoja ndiyo mkali, watoto hujenga ukaribu na mzazi mwingine mwenye upendo, kitu ambacho ni hatari zaidi.

“Ikiwa kwenye familia baba ni mkali, watoto wote huwa karibu na mama wakati wote, hali hii humfanya mtoto wa kiume kuiga tabia za mama na si baba, vivyo hivyo kwa mtoto wa kike, anapopewa malezi yenye upendo na baba yake, huanza kuiga tabia za baba yake, kitu ambacho ni hatari,” anaeleza.

Related Posts