Usichokijua matokeo ya la nne, kidato cha pili

Dar es Salaam. Wakati Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) likitangaza kuendelea kuimarika kwa ufaulu wa matokeo ya darasa la nne na kidato cha pili, Mwananchi imebaini somo la fikizia, kemia na  hisabati bado ni mwiba kwa wanafunzi wa sekondari.

Pia, imebaini idadi ya wanafunzi wanaorudia kidato cha pili imeongezeka kwa mwaka 2024 ikilinganishwa na waliokuwapo mwaka 2023 huku shule za sekondari ambazo zimepata wastani wa daraja D na F zikiongezeka kutoka 4,183 mwaka 2023 hadi 4,330 mwaka 2024.

Uchambuzi wa Mwananchi  umefanyika ikiwa ni siku moja baada ya Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohamed kutangaza matokeo ya mitihani ya darasa la nne na kidato cha pili iliyofanyika mwaka jana.

Alisema wanafunzi 1,320,227 kati ya 1,530,805 wa darasa la nne wamefaulu kuendelea na darasa la tano mwaka 2025 huku wanafunzi wa shule 680,574 kati ya 796,825 wakifaulu kwenda kidato cha tatu.

Mbali na ufaulu huo ambao umeongezeka kwa asilimia 2.90 kwa darasa la nne na asilimia 0.10 kidato cha pili,  bado kuna vitu vinapaswa kufanywa zaidi na Serikali katika kuboresha hili.

Fizikia, kemia, hesabu mwiba

Wakati somo la fizikia na kemia ufaulu wake ukionekana kuimarika katika mitihani ya mwaka 2024 ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2023, uchambuzi unaonyesha masomo hayo bado ni mwiba kwa wanafunzi wa sekondari  kwa kuwa, wengi wanaangukia daraja F huku kiduchu wakipata daraja A hadi D.

Uchambuzi unaonyesha, katika wanafunzi 793,765 waliofanya somo la fizikia, 608,897 sawa na asilimia 76.71 walipata daraja F na waliobakia ndiyo walikuwa katika daraja A hadi D.

Waliopata F ni pungufu kidogo ikilinganishwa na asilimia 80.94 ya waliokuwapo mwaka 2023.

Somo la kemia, wanafunzi 523,116 kati ya 796,098 waliofanya mtihani huo walipata F huku wachache waliobakia wakipata A hadi D. Mwaka 2023 waliopata F somo hili walikuwa asilimia 71.84.

Tofauti na masomo hayo ambayo ufaulu wake umeonekana kuimarika, hali ni mbaya kwa hisabati kwa kuwa, imeendelea kutumbukia shimoni.

Hiyo ni baada ya walipata F katika somo hilo sasa kufikia asilimia 81.15 ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 78.92 iliyokuwapo mwaka 2023.

Hii inafanya sasa waliopata daraja A hadi D kufikia asilimia 18.85 mwaka 2024 kutoka asilimia 21.08 iliyokuwapo mwaka uliotangulia.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati nchini, Dk Saidi Sima amesema katika hisabati kilio kikubwa ni upungufu wa walimu jambo ambalo inafanya hata waliopo kushindwa kufanya kazi ipasavyo kutokana na mzigo wa kazi wanaobeba.

“Kwenye hisabati kuna upungufu mkubwa wa walimu ukizingatia hata usahihishaji wake ni tofauti kwani mtu atatakiwa kuanzia hatua ya kwanza hadi ya mwisho sasa hii inaweza kuwa changamoto kwa walimu waliopo,” amesema Dk Sima.

“Kitu tunachoweza kufanya kupunguza uhaba huu ni kufanya tathmini kila halmashauri iseme kuna wanafunzi wangapi na walimu wa hisabati wako wangapi na mikakati yao ikoje katika kupunguza uhaba huu, hii ndiyo namna tunayoweza kupata matokeo chanya.”

Kuhusu fizikia na kemia, mdau wa elimu, Neema Kitundu amesema ufaulu huu mbaya unasababishwa na kukosekana kwa walimu na maabara.

“Shule nyingi hazina maabara, baadhi wametenga vyumba vya madarasa lakini hawana vifaa vya kutosha kwa ajili ya kufanyia vitendo na unakuta shule nzima ina mwalimu mmoja ni ngumu kupata matokeo mazuri,” amesema.

Katika mitihani ya kidato cha pili licha ya ufaulu kuongezeka kiduchu, uchambuzi unaonyesha shule zinazoangukia katika wastani wa daraja D na F zimeongezeka kadi kufikia 4,330 mwaka 2024 kutoka shule 4,183 zilizokuwapo mwaka uliotangulia.

Kuongezeka kwa shule katika kundi hili huenda imetokana na ongezeko la shule za sekondari nchini kwani mwaka 2024 wanafunzi waliosajiliwa walitoka shule 5,900 ikilinganishwa na shule 5,115 zilizokuwapo mwaka 2023.

Licha ya ongezeko hilo, Neema amesema ufaulu hafifu wa shule unatokana na mbinu za ufundishaji zinazotumiwa na walimu kutokuwa rafiki: “Walimu si wabunifu kumfanya mwanafunzi kuelewa, kukimbia kumuadhibu mtoto kupitiliza kunamfanya anachukia somo lako.”

Amesema mbinu nyingine zinazoweza kufanya ufaulu kuwa chini ni kukosekana kwa ujumuishaji kwenye kufundisha kwa kulipa kundi fulani kipaumbele au kutumia maneno yanayoweza kuwafanya watoto wengine kuhisi kushushwa chini.

“Wakati mwingine lugha tunazotumia zinawaumiza wanafunzi, mtoto anaweza kuwa si anayejibu maswali mara nyingi, siku akipatia ukamuambia kipofu kaona mwezi hatokuja kujibu tena,” amesema Kitundu.

Kutokuwapo kwa miundombinu rafiki ya kujifunzia na kufundishia inayokwenda sambamba na wanafunzi walipo pia ni sababu nyingine ya wanafunzi kushindwa kufanya vizuri darasani.

“Pia, walimu wapewe mafunzo endelevu kazini ili kuhakikisha wanafundisha ipasavyo na kujua mbinu tofauti za ufundishaji,” amesema.

 Watakorudia wanafunzi ngazi tofauti

Kushindwa kuendelea kutokana na matokeo mabaya bado ni jambo linaloaendelea kuwasumbua wanafunzi wengi katika ngazi tofauti zinazokutana na mitihani ya upimaji.

Kwa mujibu wa taarifa ya Necta, mwaka 2025 wanafunzi 210,578 watalazimika kurudia darasa la nne baada ya kufeli mitihani ya upimaji huku upande wa sekondari wanafunzi 116,251 wakirudia darasa hilo.

Akizungumzia hili, mdau wa elimu, Ochola Wayoga amesema kwa upande wa darasa la nne idadi ya waliofeli inaonyesha ni kiasi gani kama nchi imewekeza kwenye elimu.

“Katika hatua za awali ndiyo kunatakiwa kufanyiwa uwekezaji zaidi lakini huku huko ndiyo unakuta wanafunzi 300 kwa darasa au walimu watatu shule nzima, madarasa yana wanafunzi wengi. Namna tunawekeza katika madarasa ya awali bado sana,” amesema Wayoga.

Amesema mtihani wa darasa la nne ni upimaji ili kuona uelewa wa mwanafunzi tangu ameanza shule darasa la kwanza hadi alipofikia, siyo maswali magumu huku akiweka bayana kuwa kama watoto zadi ya 200,000 walishindwa kujibu maswali hayo basi kuna kuna shida ya ufundishaji na vitendea kazi.

“Kuna  shule ambazo ziko pembezoni unaweza kukuta mtoto hajawahi kusoma hata kitabu, anawezaje kufaulu nadhani umefika wakati sasa, Serikali ifanye mikataba na walimu na kuwapatia KPI. Lakini hii inaweza kuwa ngumu kwa shule za Serikali kwani wakifelisha unaweza kukuta mkurugenzi anachachamaa lakini huwezi kumchachamalia mwalimu ambaye hujamuwezesha vitendea kazi,” amesema Wayoga.

Ameonesha wasiwasi kuwa, hali hii isipofanyiwa kazi huenda matokeo ya mwakani yakawa mabaya zaidi kwani mtihani utakaofanywa utakuwa ni wa mtalaa mpya, hivyo ni vyema uwekezaji ukafanyika vya kutosha.

Miongoni mwa maeneo ambayo amependekeza kuangaliwa zaidi ni utoaji wa ruzuku kwa shule za msingi kwa kuwa, kiasi kinachotolewa hasa kwa wanafunzi wa msingi ni kidogo ikilinganishwa na nchi nyingine.

“Bajeti ya mtoto inayotengwa kwa shule za msingi unakuta ni Sh6,000 wakati nchi za Ulaya wenzetu mtoto anatengewa hadi paund 100,000, bajeti ya elimu iongezwe, hakuna nchi inayoweza kuendelea kama hakuna uwekezaji kwenye elimu,” amesema Wayoga.

Kuacha shule pia ni jambo linalopaswa kuangaliwa kwa umakini kwa kuwa, idadi ya wanafunzi wanaosajiliwa na kuacha shule kabla ya mtihani bado ni kubwa.

Kwa takwimu za mwaka 2024, wanafunzi 102,368 wa darasa la nne na 72,179 wa kidato cha pili hawakukaa katika chumba cha mtihani licha ya kusajiliwa.

Kwa kidato cha pili, idadi hiyo ni ongezeko kutoka 64,160 iliyokuwapo mwaka uliotangulia.

Wayoga amesema katika suala la mwanafunzi kubaki shuleni linahitaji jitihada za pamoja hasa katika ufuatiliaji na tathmini kwa kuwa, si suala la mtoto kwenda darasani na kurudi pekee.

“Mfano hadi tunakwenda kwenye mtihani watoto zaidi ya 100,000 hawajulikani walipo hii inaonyesha kuwa hakuna ufuatiliaji, kwa kawaida mtoto akikaa nje ya shule kwa siku 90 amejitoa nje ya shule na hawa unakuta wengine wamehamia maeneo ya ufugaji au kuhamia sehemu ambazo hakuna shule, hivyo ni jitihada za pamoja zinahitajika ndani ya jamii katika kukomesha hili kuanzia jamii hadi ngazi ya Serikali za mitaa.”

Related Posts