Utafutaji watoto wa jinsi fulani unavyovuruga familia

Dar es Salaam. Mume amechepuka. Mchepuko ameshika ujauzito, hatimaye mtoto wa kiume amezaliwa.

Ni mume wa mke aliyefunga naye pingu za maisha miongo mitatu iliyopita na kujaaliwa watoto wanne wote wa kike.

Hatimaye siri imefichuka. Mke na watoto wamejua kwamba baba ana mtoto nje ya ndoa na familia imegeuka tanuru la moto.

Mume analaumiwa kwa kukosa uaminifu kwenye ndoa. Mke anabebeshwa lawama ya kushindwa kuzaa mtoto wa kiume. Hadi sasa hajapatikana mshindi.

Huo ni muhtasari wa machache kati ya mengi yanayoikabili familia ya Dionis Mandi, aliyeamua kuchepuka kusaka mtoto wa kiume, aliyemkosa kwa miaka 30 ya ndoa yake.
Kwa mujibu wa Mandi, hali ya ndoa yake ni mbaya na msimamo wa mkewe ni kutomsamehe, huku yeye akiamini aliyesababisha hayo yote ni mkewe kushindwa kupata mtoto wa kiume.

Kilichotokea kwa Mandi, kinawakilisha ndoa na jamii kadhaa zenye mtazamo kuwa, mwanamke ndiye anayeamua jinsi ya mtoto.

Mkasa wa Mandi, mbali na kuiweka rehani ndoa yake, pia unakaribia kumtenganisha na familia yake.

Tukio linalofanana na hilo, limemtokea Mensa Mbena, aliyejikuta na watoto watatu nje ya ndoa yake, kwa sababu ya kutafuta wa kiume.

Mbena, mwenye mke na watoto watatu wa kike ndani ya ndoa, tamaa ya mtoto wa kiume imemlazimu kumtafuta kutoka kwa wanawake watatu tofauti nje ya ndoa yake.
Kwa mujibu wa Mbena, hakuna mtoto wa kiume kwa kila mwanamke wa nje ya ndoa yake aliyejaribu kuzaa naye, hivyo kwa sasa ana watoto sita wote wa kike.

Licha ya kushindwa kufanikisha kile alichotarajia, kwa sasa ametengana na mkewe baada ya kujulikana alikuwa na watoto watatu na wanawake wengine.

Yote hayo kwa mujibu wa Mbena, yalichochewa na msukumo wa wazazi wake, waliomtaka kutafuta mtoto wa kiume, wakidai anahitaji mtoto huyo atakayemhudumia atakapozeeka.

Hata hivyo, anasema alijikuta ameingia kwenye mkumbo wa imani kuwa, aina ya mwanamke ndiyo inayoamua jinsi ya mtoto atakayezaliwa.

Mandi anasema anachokitaka mkewe kwa sasa ni kuuawa kwa mtoto aliyezaliwa na mchepuko ili wanandoa hao waendelee kuishi kwa amani.

Shinikizo la kuuawa kwa mtoto huyo linalotoka kwa mke, linachochewa na hofu kuwa pengine mumewe ataiacha familia yake na kuhamia kwa mchepuko kwa kuwa amemzalia mtoto wa kiume, lililokuwa tamanio lake la muda mrefu.

Mke wa Mandi, Janeth Mandi anasema kwa sababu mumewe amechepuka ili apate mtoto wa kiume na kwa kuwa amefanikiwa kumpata, ni wazi atahamisha mapenzi kwa mwanamke aliyempatia mtoto wa jinsi aliyoitamani.

Ili kujihakikishia mapenzi na mumewe, anasema ni vema mtoto huyo asiwepo duniani, waendelee kuishi kama familia isiyoingiliwa na yeyote.

“Kama alitamani mtoto wa kiume na amepata, hataweza kuachana na aliyempatia huyo mtoto aliyemtaka, ina maana mimi niendelee kukubali mume wangu aishi na mchepuko huku nami ni mkewe,” anasema.

Kwa upande wa Mbena, anasema kwa sasa imekuwa vigumu kuwaona hata wanawe watatu aliozaa na mkewe kwa kuwa hawataki tena kumwona baada ya kusikia alimsaliti mama yao.

“Mama yao aliwaambia nadhani, basi tangu nitengane naye mwaka 2021 hadi sasa watoto hawataki hata kunisikia, kifungua mimba nasikia amepata mchumba anakaribia kuolewa, lakini amekataa mimi kushirikishwa,” anasema.

Anasema ndugu waliokuwa wanamshinikiza atafute mtoto wa kiume kutoka kwa mwanamke wa nje, wanamtupia lawama kwa kutengana na mkewe na wanawe.

“Hao hao waliokuwa wananishinikiza nitafute mtoto wa kiume nje ya ndoa, sasa mke wangu amegundua tumetengana na watoto wangu wa ndoa hawataki kuniona, wao wananilaumu mimi tena.

“Kwa kuwa ni wazazi wangu na wengine dada zangu sina cha kuwafanya, lakini wameniweka kwenye wakati mgumu,” anasema.

Akizungumzia hilo, Mhadhiri kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Colman Msoka anasema uamuzi wa mtu kwenda kutafuta mtoto wa jinsi tofauti na aliyonayo kwa mwenza mwingine ni matokeo ya ombwe la elimu ya dhana ya mtoto.

Kukosa elimu hiyo, anasema kunasababisha mzazi ahisi jinsi fulani ya mtoto itamsaidia jambo fulani, ilhali uhalisia ni kinyume chake, kila mtoto ana tija sawa kwa mzazi.

“Ukiwa na mtoto wa kike au kiume, akifikia umri wa kuoa au kuolewa ataondoka nyumbani na kukuacha, kama kukusaidia yeyote atakusaidia, awe wa kike au kiume,” anasema.

Hata hivyo, anaweka wazi si jambo jipya wenza kupata watoto wa jinsi moja pekee na kuna uhusiano wa suala hilo na sababu za kibaiolojia.
Lakini, Dk Msoka anasema suala hilo halipaswi kutiliwa maanani kwa sababu si hasara kupata watoto wa jinsi ya kike au kiume pekee na hakuna faida ya kupata watoto wa jinsi mchanganyiko.

Kwa upande wa wanaume, anasema mara nyingi wanaamua kwenda kutafuta mtoto wa jinsi tofauti nje ya ndoa zao, kwa sababu ya woga wa kuonekana wana matatizo.

“Mwingine anajua kuwa yeye mwanamume ndiye mwenye mchango katika kupatikana kwa mtoto wa kiume, anaogopa kwenda kupata ushauri wa kitaalamu, anaishia kutafuta namna mbadala itakayompa uhalali wa kumbebesha lawama mwanamke,” anasema.
Katika mazingira hayo, anasema ndipo wanaume huchepuka kusaka mtoto wa jinsi tofauti, ili wajisafishe na kuhamisha lawama kwa wanawake.

Dk Msoka anasisitiza familia inapaswa itambue dhana ya watoto ni nini, ili iondokane na mtazamo wa kutamani jinsi fulani ndiyo muhimu kuliko nyingine.

“Huduma na faraja utakayoipata kwa watoto wa jinsi zote ni ile ile. Ni kazi ya watu wa ustawi kutoa elimu ya dhana ya mtoto ni nini ili ieleweke,” anasema.

Anasema wanachopaswa kukielewa wazazi ni kwamba unapokuwa na watoto wa kike pekee, kuna familia yenye watoto wa kiume pekee, hatimaye wataungana na kukuza ulimwengu.

Nani anayeamua jinsi ya mtoto

Ingawa mzigo wa lawama kuhusu jinsi ya mtoto anayezaliwa aghalabu humwangukia mwanamke, kibaiolojia mwanaume ndiye anayeamua jinsi hiyo, kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa Afya ya Jamii wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Cresensia Masawe.

“Hii ni baiolojia ya kidato cha tatu. Jinsi ya mtoto inaamuliwa na baba kwa kuwa anachangia ama kromosomu X au Y kwa mwanamke, ambaye huchangia kromosomu XX,” anasema.

Mwanazuoni huyo amekwenda mbali zaidi na kufafanua, kromosomu Y inayochangiwa na mwanamume ndiyo inayoamua mtoto wa jinsi ya kiume, huku X inayotoka kwa mwanamke ni kwa mtoto wa kike.

“Sasa hapo mwenye Y kwa ajili ya mtoto wa kiume ni mwanamume mwenyewe na mwanamke ana X inayotoa mtoto wa kike.

“Kabla hujamlaumu mwanamke, kwa nini wewe mwanamume hujatoa ile Y yako ili mpate wa kiume,” anasisitiza.

Sambamba na Dk Cresensia, mtaalamu mwingine wa masuala ya afya, Dk Deusdedith Ndilanha anasema hata hivyo jinsi ya kiume au ya kike kwa mtoto ni bahati nasibu.

“Huwezi kuwa na uhakika kwamba utapata mtoto wa kike au kiume, kiimani tunasema ni mpango wa Mungu. Si mwanamume au mwanamke anayepaswa kulaumiwa kwa jinsi ya mtoto,” anasema.

Related Posts