Wajerumani wamjibu Musk akidaiwa kuingilia uchaguzi wao wa bunge 

Ujerumani. Wakati uchaguzi wa wabunge ukitarajiwa kufanyika nchini Ujerumani Februari 23, 2025, Serikali ya nchi hiyo imemshutumu bilionea wa Marekani, Elon Musk kwamba anajaribu kujiingiza kwenye uchaguzi huo kwa kukipigia debe chqmq kimoja wapo kati ya vinavyoshindana.

Musk anadaiwa kukipigia debe chama cha siasa cha mrengo wa kulia cha Alternative for Germany AfD), hata hivyo madai hayo yamekanushwa vikali na chama hicho. 

Kwa mujibu wa ripoti ya Washington Post, vyama vingine vinavyowania katika uchaguzi huo, pia, vimemkosoa bilionea huyo na mtaalamu wa teknolojia duniani.

Musk ambaye katika uchaguzi wa Marekani alijitosa kumuunga mkono Donald Trump wa chama cha Republican hadi kushinda kwake, anadaiwa kujitosa pia kwenye uchaguzi wa Ujerumani. 

“Ni kweli kwamba Elon Musk anajaribu kushawishi uchaguzi wa bunge,” Naibu Msemaji wa Serikali, Christiane Hoffmann aliwaambia waandishi wa habari.

Shutuma hizo zinafuatia chapisho la bilionea huyo katika mtandao wa X ambao anaumiliki akisema: “ni AfD pekee inaweza kuokoa Ujerumani.”

Akisisitiza zaidi Hoffmann alisema: “Uchaguzi Ujerumani unafanywa na wapigakura kwenye masanduku ya kura. Uchaguzi ni jambo la Wajerumani.”

Hoffmann alisema Musk ana uhuru wa kutoa maoni yake, lakini haimaanishi kwamba kila mtu atayaunga mkono.

Kiongozi mwenza wa chama cha Social Democrats (SPD) cha Scholz, Lars Klingbeil amesema Musk anajaribu kufanya kile kile ambacho Rais wa Russia, Vladimir Putin anajaribu kukifanya.

“Wote wanataka kuathiri uchaguzi wetu na kuunga mkono AfD, ambayo ni kinyume cha demokrasia,” amesema akiwashutumu Musk na Putin, kwa mujibu wa Citizen Digital.

Kansela Scholz apigilia msumari

Katika sakata hilo, Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz, katika mahojiano yaliyochapishwa Jumamosiamelaani matamshi ya Musk na msimamo wake wa wazi kukiunga mkono chama cha AfD.

Alipoulizwa kuhusu uingiliaji kati wa Musk, ambaye mwezi uliopita alimuita Scholz kiongozi asiye na uzoefu kabla ya kumuita Rais wa Ujerumani mkandamizaji wa demokrasia, Kansela Scholz aliliambia jarida la Stern kuwa ni muhimu kutulia kabla ya uchaguzi huo.

“Nchini Ujerumani, kila kitu kinakwenda kulingana na matakwa ya raia na sio maoni ya hovyo ya bilionea wa Marekani,” aliliambia jarida hilo katika mahojiano kama ilivyonakiliwa na tovuti ya VOA.

Imeandikwa na Sute Kamwelwe kwa msaada wa mashirika

Related Posts

en English sw Swahili