Mbeya. Hofu imetanda kwa wananchi katika Mtaa wa Isonta Kata ya Itende jijini hapa kufuatia uchimbaji wa kifusi unaoendelea katika Mlima Itende wakiomba kuwepo tahadhari ili kuepukana na majanga ya kuporomoka kama ilivyotokea kwenye Mlima Kawetele.
Hii ni baada ya kampuni ya CICO kufanya uchimbaji wa kifusi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Itende yenye kilomita 3.6 kwa kiwango cha lami unaoendelea kupitia mradi wa Benki ya Dunia (WB).
Wakizungumza katika mkutano wa dharura leo Jumapili Januari 5, 2025 baadhi ya wananchi wamesema pamoja na manufaa ya mradi huo lakini umeonekana kuwagharimu na kuhatarisha maisha yao.
Asubwisye Mwasamang’a amesema barabara iliyotengenezwa haikuzingatia usalama wa wananchi, lakini hata hivyo hawakushirikishwa kwenye mradi huo.
Amesema kutokana na hali hiyo, wanaomba kuwapo fidia kwa kuwa wasimamizi wa kampuni ya CICO wanalipwa hivyo na wananchi waliopata hasara walipwe kufuta maumivu yao.
“Hata kauli za mkandarasi si nzuri kwa wananchi, wameharibu nyumba, mazao, miundombinu ya maji hivyo tunaona mradi huu hauna afya kwetu.”
“Kwa sasa uchimbaji unaendelea kwenye huo mlima, hatujui kama umefanyiwa vipimo na wataalamu au tunasubiri yatokee ya Mlima Kawetele watu wapoteze maisha, kwa ujumla hatukushirikishwa wananchi” amesema Mwasamang’a.
Ericka Solo (92) amesema akiwa kikongwe anakabiliwa na majukumu ya kuwalea wajukuu lakini anasikitishwa kwa kuharibiwa mazao na nyumba yake, akiomba kutazamwa kwa jicho la tatu.
“Mimi ni kikongwe, mjane na nina majukumu mengi, wajukuu wananitegemea. Mazao yangu yameharibiwa na nyumba vilevile, sasa nifanye nini,” amehoji kikongwe huyo.
Naye Wedi Msawile amesema kama kampuni ya CICO ingekuwa na nia ya kusaidia maendeleo ya barabara, ingeweza kutengeneza njia ya muda kwenye barabara ya Itiji iliyo katika mpango wa kujengwa ili kurahisisha kazi bajeti itakapokuwa tayari.
“Hii ni manufaa kwa mtu mmoja aliyeuza eneo kwa ajili ya kuchimba kifusi, lakini kwa faida ya wananchi hakuna, hii kampuni ingeenda kuandaa njia ya muda kwenye barabara iliyo katika mpango kuliko ilichofanya katika makazi ya watu,” amesema Msawile.
Mwenyekiti wa Mtaa huo, Chiko Shongwe amesema ameshangazwa na mabadiliko ya ghafla kwa wananchi kwani walishatangaziwa uwapo wa mradi huo, akieleza anafikiria ni wivu kwa baadhi.
“Wengi wanaolalamika ni wale ambao hawatokei kwenye mikutano, muda mwingi wapo kazini wanaondoka asubuhi na kurudi usiku, nilimwaga kifusi kwenye hii barabara, wangeanza kulalamika mapema tofauti na sasa ilipofikia,” amesema Shongwe.
Akizungumzia kero hiyo, Diwani wa Kata hiyo, Julius Malonge licha ya kukiri kuwapo kwa uchimbaji huo wa kifusi, aliwaomba radhi wananchi walioathirika na mradi huo ambao hawakupewa taarifa akieleza hakuna kitakachoharibika.
Amesema pamoja na changamoto hizo, lakini mradi una faida kubwa kwa maendeleo ya kata na mtaa kwa ujumla, akiomba busara kutumika ili kutokwamisha shughuli hiyo akieleza kuwa dhamira ya Serikali ni njema.
“Tuliwataarifu wananchi japokuwa baadhi ambao wameathirika bila kutaarifiwa wanisamehe, lakini mradi una faida kubwa naomba muupokee busara itumike na sehemu inayohitaji fidia haki itatendeka.”
“Kama ambavyo sakata la umeme hapa nilivyolikabili haki ikapatikana, naomba muendelee kuniamini na nitaibana kampuni sehemu zinazopaswa kulipwa fidia watafanya hivyo baada ya tathmini ya wataalamu Jumatatu na kurejesha miundombinu ya maji,” amesema.
Mkandarasi wa mradi huo kutoka kampuni ya CICO, Mhandisi Robison Mushi amewatoa hofu wananchi kuwa mlima huo hauwezi kuporomoka kwa kuwa haufanani na Kawetele kwani udongo wake ni jiwe.
Amesema kuhusu miundombinu ya maji katika makazi, mafundi wanatarajia kuanza kazi haraka kurejesha huduma hiyo kwani walikuwa wakifanya tathmini ya jumla ili kujua wanaanzia wapi.
“Lakini niwatoe hofu, baada ya shughuli tutatengeneza pia mtaro kuzuia mmomonyoko wa udongo na kubaki makazi, tutafanya kitaalamu na isitoshe mimi ni mkazi wa hapa, kila kitu kitaenda sawa,” amesema.