Watengeneza maudhui yasiyofaa mitandaoni wanyooshewa kidole

Dar es Salaam. Ukiwa mtumiaji wa mitandao ya kijamii bila shaka utakuwa unafahamu mizaha (Pranky) ya watengeneza maudhui yasiyofaa kwa lengo la kupata ufuatiliaji kwa watumiaji.

Hivi karibuni kumekuwa na maudhui yenye kuzua taharuki kwenye jamii ili mradi muhusika afuatiliwe katika mtandao ya kijamii ikiwemo Instagram, Facebook, X  na TikTok.

Mfano juzi tumeona video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha kijana mmoja aliyembeba mtoto akitangaza kumuuza Sh1.6 milioni, jambo lililozua taharuki na kuibua hasira kwa jamii.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilitangaza kuanza msako wa kitaifa kumtafuta mtu huyo. Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa jeshi hilo kutoka Makao Makuu, Dodoma Ijumaa Januari 3, 2025 ilieleza,  “msako huo ni wa kuhakikisha mtuhumiwa anakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yake. Jeshi la Polisi limeeleza kuwa kitendo hicho ni cha kikatili na kinyume na sheria na limekemea vikali tabia hiyo.

Mbali na video hiyo imetajwa kwamba dhumuni la watengenezaji maudhui ni kupata wafuatiliaji wengi kwa mara moja, hivyo wanajaribu kufanya kila liwezekanalo ili watimize lengo hilo.

Hata hivyo akirejea video ya kijana aliyetangaza kumuuza mtoto, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amekemea watengeneza maudhui wa namna hiyo huku akisema wamefikia hatua mbaya.

Kupitia video ya kijana aliyetangaza kumuuza mtoto Waziri Gwajima alisema: “Watanzania salaam. Kijana huyu anatangaza eti tajiri apeleke Sh1.6 mil mtoto aliyembeba anazo figo 2.”

“Baadhi content creator (watengeneza maudhui) kama @jideboy_tz mmefikia hatua mbaya. Nakemea vikali, tayari nimewakabidhi polisi wamtafute huyu, Watanzania tusaidiane kumjua huyu ni nani na aliko,” aliandika Waziri Gwajima.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Januari 5, 2024 wadau mbalimbali wameonya kuhusu tabia hiyo wakisihi ikomeshwe mara moja kwa kuanza kuwafuatilia wanaoiendeleza.

Askofu wa Kanisa Katoliki, Methodius Kilaini amesema kitendo cha baadhi ya watumiaji kutumia mitandao bila kuwa na utambulisho sahihi ni miongoni mwa changamoto inayosababisha kutengeneza maudhui ambayo baadhi yanakiuka maadili.

“Watumiaji wanapokuwa wanatumia utambulisho usio wa kwao wanakuwa huru kwa kuwa wanaamini hakuna anayewajua,” amesema Askofu Kilaini.

Ameongeza maudhui ya namna hiyo yanakiuka hata ubinadamu wenyewe kwa sababu watu wanatumia bila kujulikana.

“Cha kufanya kwanza tutengeneze udhibiti wa watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao utasaidia katika ufuatiliaji kwa yeyote atakayetengeneza maudhui ya namna hiyo,” amesema.

Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya maaskofu na mashekhe ya maadili amani na haki za binadamu kwa jamii, Askofu William Mwamalanga ameonya watengeneza maudhui kutumia mitandao ya kijamii kueneza hila ikiwemo matusi.

“Ujumbe wangu kwao waache kabisa na vijana msije kuiga maudhui ya namna hii. Kila mtu ageuke askari wa kumlinda mwenzake eneo husika ili kila atakayeona achukue hatua ikiwemo ya kutoa taarifa mahali husika,” amesema Askofu Mwamalanga.

Amesema mitandao itumike katika mambo ya manufaa ikiwemo kufundishana biashara na malengo ya kutokomeza umasikini.

Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Nuru Mruma ametaka udhibiti na ufuatiliaji kwa wanaokiuka maadili kupitia utengenezaji wa maudhui.

“Maudhui yakitumika vibaya yana haribu jamii yetu. Watu wanaingia tamaa kwa kutafuta wafuasi bila ya kujali kile wanachofanya, tunapaswa kukemea haya,” amesema Mruma.

Amesema kwa sasa tupo kwenye ulimwengu wa mitandao ambayo ina faida na hasara ila ni vyema watu wakakumbatia faida ikiwemo kusambaza habari za kweli kufikia watu wengi.

“Wanachangia uharibifu wito wetu ni kuwa kwa sasa wazidi kuchunguzwa maudhui yao na wanaokiuka wafungiwe haraka sana na wachukuliwe hatua kali za kisheria,” amesisitiza,

Mwanasaikolojia, Charles Nduku amesema lazima kuwe na ukomo na kwamba sio kila kitu lazima kiende mtandaoni kwa sababu kikienda huko kinaenda kukaa muda mrefu.

“Mfano mtu huyo akitaka kuwa kiongozi hapo baadaye hata rais wa nchi maudhui ya namna hiyo yatakuja kugeuka kuwa ushahidi na kumuharibia ndoto yake,” amesema na kuongeza.

“Cha kwanza watu wafahamu matumizi ya mtandao na athari za mambo hayo kwa sababu baadaye itatumika kama ushahidi. Sasa hivi watu wana njaa ya maudhui jambo ambao linavunja hata faragha ya watu kiasi cha kuleta taharuki.”

Mwalimu Alawi Ally kutoka Kigoma amesema Serikali iangalie namna ya kudhibiti maudhui yanayotolewa mitandaoni kwani yamekuwa ni moja ya sababu za kuharibu jamii.

 “Watengeneza maudhui wapewe elimu ya kutosha ili kupunguza maudhui yasizofaa katika jamii,” amesema Mwalimu huyo.

Related Posts