Dk Mwigulu: TRA msiwahurumie wakwepa kodi

Arusha. Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha kila anayepaswa kulipa kodi analipa kwa mujibu wa sheria, bila kuonesha huruma kwa wakwepa kodi.

Dk Mwigulu ametoa agizo hilo  leo Januari 6  2025 jijini Arusha, alipozungumza katika mkutano wa tathmini ya utendaji kazi kwa nusu mwaka wa 2024/25 wa TRA, unaolenga kujadili na kuweka mikakati mipya ya kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato kwa mwaka.

Amesema katika masuala ya sheria, utaratibu na kodi, watendaji wasiwe na woga wa kulaumiwa, ili mradi hawamuonei mtu yeyote.

Dk Mwigulu amesema maendeleo ya nchi yanategemea ukusanyaji wa kodi na uwezo wa Taifa kujitegemea.

Amesema kila mtu anapaswa kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na yeyote anayekwepa kodi akichukuliwa hatua, “hatupaswi kuwa na huruma naye.”

“Taifa haliwezi kuendelea bila kukusanya kodi stahiki. Kila anayepaswa kulipa kodi stahiki, alipe kodi hiyo. Tuendelee kuwa wakali katika kukabiliana na wakwepa kodi, tusioneshe huruma wala muhali kwa wanaokwepa kodi,” amesema Dk Mwigulu.

Aidha, amesema wakwepa kodi wanarudisha nyuma maendeleo ya Taifa na kusababisha ukosefu wa usawa katika jamii.

Dk Mwigulu  amesisitiza kuwa, hakuna aliye juu ya sheria katika suala la kodi, hivyo TRA inapaswa kufanya kazi bila woga, kwa kuwa sheria inawalinda.

Waziri huyo amesisitiza pia umuhimu wa matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki za utoaji risiti (EFD’s) na kuonya tabia ya baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia kodi ya Serikali kama punguzo la bei, akisema jambo hilo halikubaliki kisheria.

“Tuendelee kufuatilia mbinu zote za ukwepaji kodi, ikiwa ni pamoja na matumizi ya risiti feki, ili kuhakikisha mapato ya Serikali hayapotei. Matumizi sahihi ya EFD yatasaidia kuongeza mapato ya Taifa,” amesema Dk Mwigulu.

Kuhusu kushughulika na wadaiwa sugu, ameitaka mamlaka kutafuta mbinu madhubuti za kushughulikia wadaiwa hao bila kuathiri biashara zao.

Amesema kufunga biashara kunasababisha changamoto kubwa kwa wafanyabiashara na usumbufu wa kiuchumi.

“Najua tuna wadaiwa sugu, lakini ni muhimu tutafute mbinu bora za kushughulikia suala hili bila kuingilia moja kwa moja biashara zao. Tukishughulikia biashara zao moja kwa moja, tunahatarisha kutopata fedha tunazozidai. Lazima tuwe na utaratibu unaolenga kutatua tatizo hili kwa njia endelevu, kwani kufunga biashara si suluhisho lenye tija kwa Taifa,” amesema Dk Mwigulu.

Kuhusu suala la kukamata akaunti za wadaiwa, Waziri Mwigulu amesema licha ya maboresho yaliyofanyika, bado kuna haja ya kuendelea kufanya maboresho zaidi.

“Mtazamo wa Rais wetu ni kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kifedha ya kielektroniki. Hata hivyo, iwapo kila tunayemdai tunamfutia akaunti yake, watu wataacha kutumia benki. Katika uchumi usiotegemea mifumo rasmi ya kifedha, ukusanyaji wa kodi huwa mgumu sana,” amesema Dk Mwigulu.

Amesisitiza umuhimu wa kubuni mbinu bora za kushughulika na wanaokwepa kodi makusudi.

“Tuwe na utaratibu maalumu wa kushughulikia wale wanaokwepa kodi kwa makusudi. Lazima tuwe na wivu wa kulinda biashara, kwani biashara ni msingi wa uchumi. Hatupaswi kuruhusu hasira au haraka zetu kuharibu biashara zinazoweza kuchangia ukuaji wa uchumi. Jukumu letu ni kushiriki katika kujenga uchumi imara, siyo kukusanya kodi tu bila kuzingatia athari pana,” amesema.

Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema wanatambua uwepo wa baadhi ya watumishi wasio waadilifu.

Amesema mamlaka haitawavumilia wala rushwa, wanaoonea walipakodi na kwamba hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kukiuka taratibu na sheria.

Mwenda  amesema Julai 2024 hadi Desemba 2024, TRA imewachukulia hatua za kinidhamu watumishi saba huku mmoja wao akifukuzwa kazi.

“Ndani ya miezi sita iliyopita, watumishi wengi wamechukuliwa hatua za kinidhamu. Kwa mfano, mmoja tumemfukuza kazi, wengine tumewashusha vyeo, baadhi tumewapunguzia mishahara, na wapo waliokutwa hawana hatia baada ya uchunguzi kubaini walisingiziwa,” amesema Mwenda.

Amesema lengo ni kuhakikisha haki inatendeka, huku akisisitiza hawatawavumilia watumishi wala rushwa na wanaowaonea walipakodi.

Pia, amesisitiza umuhimu wa kuwalinda watumishi waadilifu na kuchukua hatua kwa wachache wanaokiuka utaratibu.

Kuhusu ukwepaji kodi, alisema licha ya mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato, mamlaka inaendelea kupambana na changamoto hiyo.

“Duniani kote, vita dhidi ya ukwepaji kodi ni mchakato na haina mwisho. Hata nchi zilizoendelea bado zinakabiliwa na changamoto ya wakwepa kodi. Pamoja na kukusanya Sh3.52 trilioni kufikia Desemba, hatuwezi kusema hakuna ukwepaji kodi, bado upo,” amesema Mwenda.

Kamishna huyo ameongeza kuwa, mkutano huo umeandaliwa kwa lengo la kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na ukwepaji kodi.

Akizungumzia makusanyo ya kodi tangu mwaka 2020, amesema ripoti ya tathmini inaandaliwa na itaonyesha ukuaji mkubwa wa mapato.

Mwenda amesema kati ya Julai 2020 hadi Desemba 2020, TRA ilikusanya Sh9.24 trilioni.

Pia,  kuanzia Julai 2024 hadi Desemba 2024, TRA imekusanya Sh16.52 trilioni, sawa na ukuaji wa takribani asilimia 78.

Amesema mafaniko hayo yametokana na sababu kadhaa, ikiwamo uhusiano mzuri kati ya TRA na walipakodi, usimamizi mzuri wa uchumi wa nchi, kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi licha ya idadi ndogo ya walipakodi, pamoja na kuongezeka kwa uingizaji wa mizigo nchini.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts