Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA kwa kuongeza makusanyo ya kodi kutoka sh. trilioni 22.2 mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia sh. tril. 27.6 mwaka wa fedha 2023/2024 na kuvunja rekodi ya kukusanya sh. trilioni 16.528 katika kipindi cha Nusu Mwaka wa Fedha 2024/2025 kinachoanzia Julai hadi Desemba Mwaka 2024.
Dkt. Nchemba alitoa pongezi hizo, wakati akifungua Kikao Kazi cha siku 5 kinacho Tathmini Utendaji kazi wa Nusu Mwaka wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, kinachofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC), Jijini Arusha.
Alisema kuwa fedha hizo zimeisaidia Serikali kutekeleza miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha huduma za jamii kama vile Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere, Mradi wa Treni iendayo kasi (SGR), miundombinu ya barabara, huduma za jamii na mingine mengi
Dkt. Nchemba aliitaka TRA kuimarisha zaidi mifumo ya kisasa ya kielektroniki ya kukusanya mapato ya Serikali ili kuongeza uwazi, tija na ufanisi kwa kukusanya mapato pamoja na kuziba mianya ya maafisa wa TRA kukutana uso kwa uso na walipakodi.
Aidha, Dkt. Nchemba alirejea wito wake kwa Mamlaka hiyo kutofunga biashara za watu wanaowadai kodi badala yake waweke utaratibu wa kuzilea biashara hizo huku wakihakikisha kodi stahiki zinalipwa na wahusika kwa kuwa vitendo vya kufunga biashara vinaathiri uchumi wa nchi pamoja na kuvuruga mfumo wa biashara husika na kuwasababishia watu umasikini na kuwakosesha wananchi ajira.
Dkt. Nchemba alitumia wasaa huo pia kuwataka wafanyabiashara kuacha tabia ya kukwepa kulipa kodi, kutumia ipasavyo mashine za kukusanya mapato ya Serikali (EFDs) na kuwahimiza watoe risiti halali zinazoendana na thamani ya manunuzi yaliyofanyika huku wananchi kwa upande wao wakihimizwa kudai risiti halali wanaponunua bidhaa na huduma mbalimbali.
Kwa upande wake, Kamisha Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, alisema kuwa Kikao kazi hicho, pamoja na mambo mengine, kilikuwa na malengo kadhaa ya kuimarisha ukusanyaji wa kodi ili kufikia malengo waliyowekewa na Serikali ya kukusanya shilingi trilioni 30.449 katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Alimhakikishia Mhe. Waziri wa Fedha, kwamba Mamlaka hiyo itafikia malengo hayo na pengine kuzidi kidogo kutokana na viashiria vya ukusanyaji mapato katika kipindi cha Nusu Mwaka wa Fedha 2024/2025 ambapo hadi kufikia Desemba mwaka 2024, TRA imekusanya sh. trilioni 16.528, ikilinganishwa na makusanyo ya sh. trilioni 9.242, ya kipindi kama hicho Mwaka 2020/2021, ikiwa ni ongezeko la asilimia 78.78.
Bw. Mwenda alisema kuwa mafanikio hayo yanatokana na TRA kuendelea kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari, kuwasikiliza walipakodi na kutatua changamoto zao hatua iliyochangia kukua kwa uhusiano kati ya Mamlaka na walipakodi hususan kupitia viongozi wa vyama vya wafanyabiashara wote nchini wanaoendelea kuunga mkono kwa vitendo juhudi zinazofanywa na Serikali baada ya maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuboresha mazingira ya biashara na ulipajikodi nchini.
Aliwahimiza watumishi wa TRA kuendelea kufanyakazi kwa bidii, juhudi na maarifa ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kukusanya mapato yake kupitia kodi mbalimbali pamoja na kuzingatia weledi wanapotekeleza majukumu yao wakati Serikali kwa upande wake ikiendelea kuwajengea mazingira mazuri ya kufanyakazi.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) akizungumza wakati wa Mkutano Maalum wa Kamati ya Barabara ya Mkoa wa Arusha uliowashirikisha wadau wengine mbalimbali wakiwemo wabunge wa mkoa huo, ambapo walijadili namna ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya barabara mkoani Arusha ambao ni mkoa wa kitalii na unachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi kutokana na mapato yanayotokana na sekta mbalimbali za uzalishaji hususan utalii. Wengine katika picha ni Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kulia), Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda (wa kwanza kulia), Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour (wa pili kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta (wa kwanza kushoto)
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (kushoto), Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda, wakiteta jambo baada ya mawaziri hao kumtembelea Ofisini kwake jijini Arusha, wakati walipofanya ziara ya kikazi mkoani humo, ambapo pia walipata fursa ya kushiriki mkutano maalum wa Kamati ya Barabara ya Mkoa wa Arusha uliowashirikisha wadau wengine mbalimbali wakiwemo wabunge wa mkoa huo.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (Katikati aliyeketi), akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baada ya kufungua Mkutano wa Tathmini ya Utendaji Kazi wa Nusu Mwaka 2024/25 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC), Jijini Arusha, ambapo aliwapongeza kwa kuendelea kuongeza makusanyo ya kodi kila mwaka katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/22 TRA ilikusanya sh. trilioni 22.2, katika mwaka wa fedha 2022/23 ilikusanya sh. trilioni 24.1, katika mwaka wa fedha 2023/24, sh. trilioni 27.6 na katika kipindi cha mwezi Julai-Desemba ya mwaka wa fedha 2024/25, TRA imekusanya shilingi trilioni 16.528.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (Katikati aliyeketi), akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), pamoja na Wakurugenzi wa Mamlaka hiyo, baada ya kufungua Mkutano wa Tathmini ya Utendaji kazi wa Nusu mwaka 2024/25 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC), Jijini Arusha, ambapo aliwapongeza kwa kuendelea kuongeza makusanyo ya kodi kila mwaka katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/22 TRA ilikusanya sh. trilioni 22.2, katika mwaka wa fedha 2022/23 ilikusanya sh. trilioni 24.1, katika mwaka wa fedha 2023/24, sh. trilioni 27.6 na katika kipindi cha mwezi Julai-Desemba ya mwaka wa fedha 2024/25, TRA imekusanya shilingi trilioni 16.528.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Arusha)