Fadlu ategua mtego wa kwanza Simba

Kocha wa Simba, Fadlu Davids amefanikiwa kuruka kihunzi cha kwanza kati ya viwili ambavyo viliwashinda makocha wenzake katika misimu mitatu iliyopita ambayo Yanga ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

Kigingi ambacho Fadlu amekimudu ni kuiwezesha timu hiyo kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa kileleni na ikiwa imekusanya idadi kubwa ya pointi katika mechi 15 kulinganisha na msimu uliopita wa 2023/2024, 2022/2023 na 2021/2022.

Katika msimu huu, Simba imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa imekusanya pointi 40 baada ya kupata ushindi katika mechi 13, kutoka sare moja na kupoteza moja huku ikifunga mabao 31 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano.

Msimu uliopita, Simba ilimaliza mzunguko wa kwanza ikiwa imevuna pointi 36 katika mechi 15 ambapo ilipata ushindi mara 11, kutoka sare tatu na kupoteza mchezo mmoja huku ikifunga mabao 31 na iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara 14.

Simba ilitimiza nusu ya msimu wa 2022/2023 ikiwa na pointi 34 ambazo ilizipata baada ya kupata ushindi katika michezo 10, ikitoka sare mara nne na kupoteza mchezo mmoja ambapo ilikuwa imefunga mabao 31 na nyavu zilifumaniwa mara saba.

Idadi ya pointi 31 ndizo zilikuwa zimekusanywa na Simba katika nusu ya kwanza ya msimu wa 2021/2022 ambao Yanga ilitwaa ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya kuukosa kwa misimu minne mfululizo.

Katika mechi 15 za mwanzo za msimu huo, Simba ilipata ushindi mara tisa, ikakutana na matokeo ya sare katika mechi nne na kupoteza michezo miwili ambapo ilifunga mabao 16 na nyavu zake kutikiswa mara sita.

Baada ya kufanikiwa kuruka kihunzi hicho cha kwanza, mtihani wa pili unaomkabili Fadlu ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao Simba imeukosa kwa misimu mitatu mfululizo iliyopita.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Musa Hassan ‘Mgosi’ alisema kuwa benchi la ufundi la timu hiyo linaonyesha muelekeo sahihi chini ya Fadlu Davids.

“Kocha amekuwa akifanya vizuri na mimi navutiwa kwa jinsi anavyotoa nafasi kwa wachezaji tofauti kikosini jambo ambalo linawafanya wachezaji wasipate uchovu mkubwa na kila mchezo wanaingia wakiwa vizuri.

“Naona msimu huu unaweza kuwa mzuri na jambo la msingi ni kocha na benchi lake la ufundi wapewe sapoti,” alisema Mgosi.

Related Posts