KenGold yachafua hali ya hewa! watajwa Miquisone, Lwanga

KWA wanachoendelea kufanya KenGold kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo ni kama ‘kuchafua hali ya hewa’.

Hiyo inatokana na majembe inayoyashusha baada ya kutembeza fagio la nyota wanane ilioanza nao msimu huu ambao ni wa kwanza kushiriki Ligi Kuu.

Hadi sasa timu hiyo imetangaza kuachana na Poul Materraz, Asanga Stalon, James Msuva, Steven Mganga, Amir Njeru, Castor Posta, Adam Uled na Salum Idrissa.

Wakati ikiachana na hao tayari imemalizana na Bernard Morrison na Obrey Chirwa, huku hesabu zikihamia kwa Tadeo Lwanga, Luis Miquisone na Saido Ntibazonkiza ambao wote wamewahi kucheza Simba.

Pia imemvuta aliyekuwa beki wa kati wa Fountain Gate, Assi Serge raia wa Ivory Coast ambaye yupo mafichoni katika mitaa ya Isyesye jijini Mbeya.

Taarifa ilizopata Mwanaspoti ni kuwa, mabosi wa timu hiyo wameamua kuvunja benki kuingia sokoni kusaka mastaa wa kuinusuru na janga la kushuka daraja baada ya mzunguko wa kwanza kutofanya vizuri.

Katika michezo 16 iliyocheza timu hiyo ya wachimba dhahabu wa Chunya, imekusanya pointi sita na kuwa mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, ambapo inahitaji kurejea upya raundi ya pili Machi Mosi.

“Tunataka timu mpya, ndiyo maana mabosi wameamua kuweka pesa mezani izungumze. Tunayemtaka yeyote tutampata kwa gharama yoyote.

“Leo (jana) tumeanza mazoezi japokuwa mastaa wengi hawajafika ila hadi wiki ijayo kikosi kitakuwa kamili. Hawa waliopo wengine ni kwa ajili ya majaribio kuona nani atatufaa,” alisema mmoja wa vigogo.

Chirwa, Morison, Steven Dua, Erick Okutu, Robert Kayala ambao tayari wamemalizana nao, wiki ijayo wanatarajia kuungana na wenzao mazoezini kujiandaa na michezo ya ligi.

Related Posts