Dar es Salaam. Kiingereza ambayo ndiyo lugha ya kujifunzia kwa wanafunzi wa sekondari imeendelea kuwa mwiba, baada ya robo ya wanafunzi waliofanya mtihani wa majaribio wa kidato cha pili mwaka 2024 kupata alama F.
Jambo hilo linatajwa kuwa moja ya sababu ya wanafunzi wengi kupata F katika masomo mengine kutokana na kushindwa kuelewa lugha inayotumika katika kufundishia na kujibia mitihani, huku wakitaka tathmini ya kina kufanyika kujua lugha gani inafaa katika kufundishia.
Matokeo ya mitihani ya upimaji yaliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) Januari 4, 2025 yanaonyesha wanafunzi 202,448 kati ya 796,413 waliofanya mtihani wa Kiingereza walipata daraja F katika somo hilo huku 288,858 wakipata daraja D.
Hiyo ikiwa na maana kuwa ni asilimia 38.31 pekee ya wanafunzi ndiyo waliweza kupata daraja A hadi C ambayo kwa idadi yao ni 305,107.
Hiyo ni tofauti na somo la Kiswahili ambapo ni asilimia 8.26 pekee ya wanafunzi ndiyo walipata daraja F. Waliopata A hadi C katika somo hilo ni asilimia 63.2 zaidi ya waliokuwa na wastani huu katika somo la Kiingereza kwani walikuwa 498,003.
“Siyo tu wamefeli Kiingereza, inaonyesha hawana uelewa wa kutosha kusoma masomo yao ya sekondari kwa lugha ya Kiingereza,” amesema mwalimu Richard Mabala ambaye ni mdau wa elimu.
Amesema matokeo haya yanaonyesha ni kwa namna gani wanaofaidika na Kiingereza kinachotumika katika kufundisha ni wale waliosoma shule za michepuo ya Kiingereza kwa sababu kimekuwa kikitumika kwao tangu awali.
“Ili tufanikiwe katika hili labda tufanye shule zote ziwe za Kiingereza lakini haiwezekani kufanya hivyo kwa sababu hatuna walimu wa kutosha kufundisha lugha hiyo kama somo,” amesema.
Amesema umefika wakati sasa wa kufanyika kwa majaribio ili kuruhusu Kiswahili kutumika hata kwa nusu ya shule nchini, ili kujua kama waliofeli mitihani ilikuwa ni kushindwa kuelewa lugha au masomo.
“Tufanye kitu kuonyesha Kiingereza hakiwezekani na matokeo haya tunayaona ni ya wanafunzi ambao walipewa wiki sita za mwanzo kujifunza Kiingereza, lakini haileti mabadiliko makubwa.”
“Basi kama hatuwezi kubadilisha tutafute shule za mfano tugawanye, ndani ya shule moja nusu wajifunze Kiswahili nusu Kiingereza na wafanye mtihani tuone matokeo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mabala amesema suala la Kiingereza kuendelea kuwa lugha ya kufundishia ni mwiba, huku akieleza kuna wakati ambao aliwahi kusikia kuwa walimu wa shule ya msingi walipewa mtihani wa Kiingereza na wengi walifeli lakini walipopewa mtihani huo kwa Kiswahili walifaulu.
Alitumia nafasi hiyo kuitaka wizara ya elimu au taasisi za elimu wafanye hizi tafiti ili waone kama kuna tofauti.
Hili linasemwa wakati ambao kwa nyakati tofauti kumewahi kuwa na mvutano kati ya wadau mbalimbali wa elimu na Serikali kutaka lugha ya kufundishia shule za umma kuwa Kiswahili badala ya Kiingereza kinachotumika sasa.
Hiyo ni kutokana na wao kueleza ni ngumu kwa wanafunzi waliosoma Kiswahili kwa miaka saba kuhamia ghafla kujifunza masomo yote kwa Kiingereza wanapoingia kidato cha kwanza.
Hata hivyo, pamoja na kuwapo kwa majadiliano hayo, Serikali ilisisitiza kuwa Kiingereza kitaendelea kuwa lugha ya kujifunzia katika shule za sekondari huku ikitafuta namna ya kuwaandaa wanafunzi kumudu lugha hiyo kabla ya kuanza masomo rasmi wanapojiunga kidato cha kwanza.
Agosti 2022, Serikali ilikuja na mkakati wa makusudi wa kuboresha elimu ambao pamoja na mambo mengine ulilenga kuwaandaa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kujifunza na kuwa na uwezo wa kumudu lugha ya kujifunzia yaani Kiingereza.
Mkakati huo uliozinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ulitenga muda wa kuanzia Januari hadi Mei kuwa maalumu kwa wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza kujifunza Kiingereza ili waweze kumudu stadi za kuandika, kusikiliza, kusoma na kuwasiliana.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wakati somo la Kiingereza likiendelea kuwaumiza wanafunzi, kwa wale wanaosoma lugha za kigeni kama Kichina ni asilimia 9.18 pekee walipata daraja F.
Katika wanafunzi 1,841 waliofanya mtihani wa kidato cha pili upimaji katika lugha ya Kichina, 1,113 waliibuka na daraja A hadi C.
Akizungumzia ufaulu somo la lugha ya Kichina, Mkurugenzi wa Tanzania wa Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Aldin Mutembei amesema walimu wote wanaofundisha lugha ya Kichina wamesomea ufundishaji wa hiyo kama ya kigeni.
“Pia yapo masomo ambayo wanafundisha ikiwemo ufundishaji wa lugha hii kwa wazungumzaji wa lugha nyingine na ufundishaji lugha hiyo kama lugha ya kigeni. Hili halipatikani katika lugha nyingine za kigeni kama Kiingereza ambapo walimu wake hawafundishwi namna ya kufundisha somo hilo kama lugha ya kigeni na badala yake wanafundisha kama somo.
Amesema pia siku hizi kumekuwa na mtindo wa watu kusoma ili wafaulu na si kuelewa tofauti na Kichina unapofundishwa kukielewa ili ukitumie katika maeneo mengine.
“Hili jambo ni muhimu. Pia walimu wanaofundisha lugha ya Kichina hawaingiliwi na walimu wengine, tatizo hili lipo sana katika lugha ya Kiingereza, hata kama walimu hawa wangekuwa wamebobea kukifundisha lakini walimu wa lugha nyingine wanawaharibia kwa sababu kila anayekwenda kufundisha sekondari anatumia Kiingereza wakati si mwalimu wa Kiingereza,” amesema.
Amesema jambo hili limekuwa likifanya wanafunzi kuharibiwa bila kujua kama wanaharibiwa.
Akieleza mbinu zinazotumiwa kuhakikisha walimu wa Kichina wanakuwa na ubora unaotakiwa amesema wamekuwa wakiwapatiwa mitihani kila baada ya muda fulani, ili kujua ni kwa kiasi gani bado wana umahiri katika somo hilo na inapoonekana kuna kushuka wanapewa muda wa kujinoa kwa muda fulani.
“Kwa walimu wanaofundisha vyuo, kila baada ya miaka miwili wanafanya mtihani kupimwa kama apewe mkataba mwingine au ubongo wake bado uko vizuri, hii inafanya walimu kuweka bidii katika wanachokifanya,” amesema.