Kipindupindu, ukosefu wa vyoo vyafunga mgodi wa dhahabu

Katavi. Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuf ameagiza kufungwa kwa shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu katika migodi ya Lumuka iliyopo Kijiji cha Dirifu kutokana na watu 17 kugundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa kupindupindu.

Hali hiyo imekuja baada ya kutembelea maeneo ya migodi leo Jumatatu, Januari 6, 2025 na kukuta watu wanaofanya shughuli kwenye eneo hilo la mgodi zaidi ya 3,000 wakiwa hawana vyoo na badala yake wanajisaidia vichakani.

“Niwape pole wananchi wa hapa Lumuka mnaofanya kazi katika machimbo haya kwa wenzenu 17 kugundulika na maambukizi ya kipindupindu. Idadi hii ni kubwa sana.

“Serikali inawapenda na inawajali wachimbaji wakubwa, wakati na wadogo, lakini haiko tayari kuona wananchi wake wanaathirika au kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huu wa kipindupindu. Kwanza ni aibu watu zaidi ya elfu tatu kukosa vyoo na mnajisaidia vichakani. “Nafunga shughuli zote katika maeneo haya ya migodi mpaka mtakapokamilisha ujenzi wa vyoo vya kisasa ndani ya siku saba viwe tayari, ili muendelea na shughuli zenu vinginevyo hatutaruhusu uchimbaji uendelee hapa,” amesema.

Amesema kulingana na idadi ya watu waliopo, inatakiwa vijengwe vyoo angalau vinne vya kisasa ili vitoe huduma inayostahili.

“Nimesikia mnajenga vyoo vya maturubai, hivyo haviruhusiwi kabisa kujengwa katika maeneo haya ya migodi.

“Hili hatutakuwa na huruma nalo, tutachukua hatua kali na stahiki kwa yeyote atakayekeuka maagizo haya. Hatuna uwezo wa kuhudumia mkiugua wote kwa pamoja, lazima tuwe wakali kwenye hili,” amesema.

Muonekano wa maeneo ya mgodi wa Lumuka uliofungwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu na ukosefu wa vyoo. Picha na Idd Mumba

Aidha, ameagiza wataalamu wa afya na maji kufanya ukaguzi wa visima vyote vinavyotoa huduma ya maji kwa wananchi wa wilaya hiyo na kuweka dawa ya kutibu maji pamoja na kufukia visima ambavyo havikithi vigezo.

Kwa upande wake, mganga wa Halmashauri ya Mpanda,  Dk Limbo Mazoa, amewataka watu kujilinda kwa kunywa maji yaliyochemshwa na kunawa mikono kwa maji tiririka na endapo mtu ataona dalili kama kuharisha, kutapika na mwili kuishiwa nguvu, ni vyema akawahi kituo cha afya.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpanda, Sophia Kumbuli amewataka wananchi kuchukua tahadhari na kwamba kila mtu awe mlinzi wa afya yake ili kuepusha ugonjwa huo kuenea kwa haraka katika familia na jamii kwa ujumla.

“Tumieni dawa zinazotibu maji ili kuepuka magonjwa ya mlipuko, kwani tunafahamu asilimia kubwa ya wananchi wetu mnatumia maji ya visima kwa ajili ya kunywa, kupikia na shughuli mbalimbali,”amesema Kumbuli.

Related Posts