Tanga. Mwaka 1961 Wilaya ya Tanga ilikuwa Halmashauri ya Mji ambayo ilipandishwa hadhi kuwa manispaa mwaka 1983 na kuwa Halmashauri ya Jiji mwaka 2005 mpaka sasa.
Wilaya hiyo ipo kwenye Jiji la Tanga na ndio makao makuu ya Mkoa wa Tanga, ikiwa na jumla ya tarafa nne, kata 27 na mitaa 181, huku jiji hilo likigawanyika katika maeneo ya mjini na nje ya mji ambapo jumla ya kata 16 ziko mjini, na kata 11 zipo nje ya mji.
Wilaya ya Tanga ni miongoni mwa wilaya zilizoanzishwa wakati wa ukoloni, ikiwa chini ya Jimbo la Kaskazini Mashariki ambalo makao makuu yake yalikuwa Tanga. Awali, wilaya hiyo ilijumuisha wilaya za Muheza, Mkinga na Tanga yenyewe.
Asili ya jina la Tanga imetoka katika kisiwa cha Toten kinachopatikana katika jiji la Tanga kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi, kikiwa kina ukubwa wa takriban hektari 16 karibu na ufukweni. Watu waliishi katika kisiwa hicho na walikuja upande wa pili nchi kavu kwa shughuli za kilimo na baadaye kurudi kwenye makazi yao.
Mkazi wa Jji la Tanga, Uliza Ali Simba (75) anasema historia ya jina la kisiwa hicho linalotoka katika lugha ya Kijerumani katika neno “Toteninsel” kwa maana ya “Kisiwa cha Wafu” kwamba Wajerumani walitumia jina hilo walipofanya Tanga kuwa bandari muhimu ya koloni lao la Afrika Mashariki ya Kijerumani.
Anasema Waingereza walipochukua utawala kutoka kwa Wajerumani, walikiita kisiwa hicho Toten Island wakichukua
“Toten” kama jina, hawakutafsiri maana yake ya awali ya wafu kutoka kwa Wareno na badala yake wakaendelea kulitumia kama walivyolikuta.
Simba anaeleza watu wengi wanakifahamu kisiwa hicho kwa jina la Toten, ila jina lake la asili ni Changa.
Kwamba kuna wakati Mjerumani alikitumia kisiwa hicho kama eneo la kutenga watu waliokumbwa na magonjwa ya kuambukiza yasiyo na kinga wala tiba kwa kipindi hicho, walitengwa wafie hukohuko ili wasiambukize wengine. Ndio maana kikaitwa Toten Island ‘Kisiwa cha Wafu’.
Anasema kwa miaka hiyo, kisiwa hicho waliishi wakazi wenyeji wa Wilaya ya Tanga ambao ni kabila la Wabondei na mapokeo ya historia yanaonyesha kuwa karne ya 14 Wareno walifika eneo hilo, walikuta watu wakiishi na mila na taratibu zao.
Hata hivyo, anasema walipofika walikuta watu wachache, hasa wanawake wakiwa na watoto, Wareno waliwauliza kwa lugha yao, ni wapi walipo wengine? Wananchi hao walijibu “Waita N’tanga” kwa lugha ya kibondei wakiwa na maana wamekwenda shamba.
Baadaye ikabainika kuwa Wareno walinakili neno Tanga wakidhani sehemu waliokwenda wenyeji inaitwa hivyo, ila Wabondei walimaanisha ‘N’tanga’, kwa maana ya “shamba” na wala si jina la sehemu.
Nani mwenyeji wa Tanga kati ya kabila la Wabondei na Wadigo?
Inaelezwa tangu karne ya 14, Mbondei alikuwa akiishi katika eneo hilo la kisiwa cha Changa maarufu kama wengi wanavyofahamu Toten, na ndio mwenye asili ya mji huo.
Mkazi wa Tanga mjini, Abubakar Ahmad Lwendo, anasema wenyeji wa Tanga ni Wabondei na si Wadigo kama wengi wanavyosema, ila kulitokea sintofahamu iliyosababisha Wabondei kwenda Muheza na mji kuuacha chini ya Wadigo baada ya mapigano.
Anasema mwaka 1800 kulikuwa na koo tisa kutoka mashariki ya mbali ambazo zilikimbia vita na matukio mengine kutokea nchi ya Misiri, waliingia Kenya wakashuka mpaka Mombasa na wengine kuja Tanga.
Katika koo hizo nyingi zilibakia njiani, hivyo mzee Digo na koo yake ndio walifika mpaka Tanga na baadaye kuanza kutafuta wapi wataweka makazi yao waishi, kwani hawakuwa na mpango wa kurudi Misiri.
“Wadigo ambao asili ya hilo jina ni mzee Digo aliyeongoza hilo kundi kutoka Misiri, walipofika Tanga kwenye kisiwa hicho walikuwa wanahitaji eneo la kuishi, hivyo mwaka 1800 ilitokea vita ya Wadigo na Wabondei na mwenyeji alipigwa na kukimbilia bondeni Muheza,” anasema Abubakar.
Abubakar anaeleza ili kuthibitisha kwamba Mdigo si mwenye asili ya Tanga, wao ni mashombe shombe kwa maana ni weupe na muonekano wao ni kama waarabu, ila asilia ya watu hao ni kutoka bara la Asia.
Anasema mpaka sasa kabila la Wadigo na Wabondei ni watani kila wanapokutana kwenye shughuli zao za kimila, yote inatokana na vita waliopigana wazee wao miaka hiyo.
Vitu vilivyopo kisiwa cha Toten
Ndani ya kisiwa cha Changa au Toten kama kinavyofahamika na wengi, shughuli kubwa inayofanyika ni watalii kutembelea kuona mabaki ya vitu vya zamani hasa magofu ya majengo na miti mikubwa.
Amour Said, mvuvi anayetembelea kisiwa hicho mara kwa mara anaeleza kwa sasa ndani ya kisiwa kuna magofu ya msikiti na kanisa yaliojengwa kipindi hicho, kuna makaburi ya watu wa kale waliozikwa enzi za wakoloni.
Anasema mpaka sasa ndani ya kisiwa hicho kuna magofu ya msikiti na kanisa ya karne ya 17 na makaburi ya karne za 18 na 19. Pia kuna vipande vya vyungu vilivyotumika zamani.
“Kuna mabaki ya jengo la msikiti na kanisa ambayo yalijengwa karne ya 17 na wageni walikuwa wanaishi humo na kuna makaburi zaidi ya 70 ya Wajerumani na Wareno na kuna wakati ndugu zao wanakuja kuyasafisha na wanawafahamu watu hao,” anasema Amour.
Anasema hakuna shughuli nyingine ya kijamii inayofanyika huko, kama kilimo au kujenga makazi kwa kuwa Serikali imezuia na kisiwa hicho kipo chini ya mamlaka ya bandari.
Said anaeleza kuwa pia ni gharama kuvuka kwa wakati huu kwenda kisiwani, kwani kwa kutumiwa ngalawa ambayo haina mashine ni Sh30,000 ila ukitumia boti ya kukodi kutoka upande wa Tanga mjini ni Sh70,000 mpaka 100,000.
Mitaa ya zamani iliyokuwa ikitambuliwa kwenye Wilaya ya Tanga ilikuwa ni barabara ya kwanza mpaka 21, Mwamboni, Nguvumali, Majani Mapana, Ngamiani, Chumbageni, Mwakizaro, Kisosora na Makorora, huku mitaa mipya ikitajwa kama Donge, Kange, Sahare, Mikanjuni, Mchukuuni na mingine inayoendelea kujengwa.