Maafande waingilia dili la Mpepo

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Eliuter Mpepo ambaye aliwahi kufanya vizuri katika Ligi Kuu Zambia akiwa na Trident FC anajiandaa kutua Tabora United kwa mkataba wa mwaka mmoja, lakini pia Tanzania Prisons ikimpigia hesabu.

Mpepo ambaye amefunga mabao saba na kutoa asisti tano kwenye Ligi Kuu Zambia, ameonekana kuwa chaguo muhimu kwa timu hizo zinazohitaji kuboresha eneo la ushambuliaji.

Licha ya mkataba wa awali kusainiwa, bado kuna baadhi ya vipengele muhimu vinavyohitaji kukamilika, jambo ambalo limechelewesha utambulisho rasmi wa mchezaji huyo kama mchezaji wa Tabora United na kuchelewa kwa dili hilo kumetoa mwanya kwa timu yake ya zamani, Tanzania Prisons.

Timu hizo ambazo zimekuwa zikipambana kutafuta mshambuliaji mwenye uwezo wa kumalizia nafasi za mabao, zimetajwa kufanya mazungumzo na menejimenti ya Mpepo ili kumaliza suala la uhamisho wake.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani, maafande Prisons wanapanga kumshawishi Mpepo kujiunga nao kutokana na uhitaji wao wa mchezaji mwenye kasi na ufanisi wa kufunga.

Pamoja na hayo, Mpepo mwenyewe ameweka wazi akisema kwamba menejimenti yake inafanya juhudi ya kumaliza vipengele vyote muhimu kwa ajili ya uhamisho wake.

“Kuna mambo ambayo bado yanahitaji kukamilika, lakini tunafanya kazi ya kuhakikisha kila kitu kiko sawa. Natumai tutakuwa na majibu mazuri siku chache zijazo katika kipindi hiki cha dirisha la usajili,” alisema Mpepo, akionyesha matumaini kuhusu mustakabali mpya.

Related Posts